Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza ninarejea hotuba ya Waziri ambapo katika ukurasa mmojawapo ulihamisha jukumu la uwekaji vinasaba kwenye mafuta ya petroli kutoka kwa Mkandarasi binafsi na jukumu hili ukalipa Shirika la Viwango la Tanzania. Sasa Mheshimiwa Waziri nataka wakati unajibu utueleze namna gani fikra kama hii ambayo kutokana na mikata mibovu na hovyo kabisa ilisababisha Mkandarasi binafsi kwa mwaka kupata zaidi ya bilioni 68 kwa miaka nane aliyokuwepo zaidi ya bilioni 490. Umefanya jambo la busara kuondoa hilo jukumu kuipa taasisi ya Serikali ili haya mapato basi yaweze kuingia Serikalini na hata mkipunguza gharama yakiwa kwa kiwango kidogo vilevile yaweze kuingia Serikalini, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka uniambie Mkandarasi huyu ambaye amepewa jukumu la kubandika stempu za ki-electronic ama ETS, kwenye bidhaa zinazozalishwa Nchini kwa ajili ya kutoza ushuru wa bidhaa mkataba wake utakoma lini ili hili jukumu ambalo amepewa Mkandarasi huyu kipewe ama chombo cha Serikali ama mfanye ushindani upya aweze kupatikana Mkandarasi kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza juu ya mafuta, sasa nitazungumza juu ya ETS. Kwa maelezo ya Serikali huu utaratibu ulianza mwaka 2018, maana tunaofikiria kipindi kile mambo yalikuwa perfect sana, lakini siyo kila kitu ni perfect kuna sehemu tunakosea na lazima tujirekebishe. Lengo lake lilikuwa ni jema kuweza kutambua bidhaa, kuzuia watu wasikwepe kodi, Serikali iweze kupata kodi yake stahiki, jambo ni jema. Lakini gharama, tunaambiwa mpaka sasa hivi wazalishaji ambao wamefungiwa hizo mashine wako 245, waagizaji 86. Sasa mafanikio ni nini! Kwa sababu kwa petroli ilikuwa akiweka kale kadude lita moja shilingi nane, huku kwenye bidhaa za vinywaji, vinywaji vikali na vyepesi na masigara na kadhalika kuna shilingi nane kwa mantiki ya dola nane na dola 20 kutegemeana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mafanikio ni nini kabla ya ETS na baada ya ETS. Kwa maelezo ya TRA kabla ya ETS tulikuwa tunakusanya shilingi bilioni 237 baada ya ETS tumekusanya shilingi billioni 246. Tafsiri yake ni nini, tofauti ninyi mnajua bilioni 46 toa bilioni 37 ni bilioni nane. Sasa gharama ambazo Makampuni yetu yanaingia kutokana na huu mchakato ni nini? Taarifa ya TBL ambao ni walipa kodi wakubwa nchini, wanasema katika kipindi cha miaka mitatu wanatarajia, kuanzia mwaka 2019 mpaka 2021 watamlipa Mkandarasi shilingi bilioni 94 kampuni moja, hapo nimesema makampuni ambayo ama viwanda viliunganishwa ni zaidi ya 250, wakati TRA nyongeza yao ni kutoka bilioni 237 mpaka bilioni 246 different ya eight billion. TRA wakatupa data zao za mvinyo wa ndani, kabla mtambo wa ETS shilingi milioni 657 baada ya ETS on average imeongezeka mpaka bilioni 3.4. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha pili ni cha sigara, mmeshataja TBA hapo. Mkandarasi binafsi kalipwa na TBA bilioni zaidi ya 90. Serikali nyongeza mlifikiria kuna cheating kubwa mmepata shilingi bilioni nane. Hivi, tukisema hii ni busara, hii ni busara…

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa, taarifa!

MHE. HALIMA J. MDEE:… TCC...

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee kuna taarifa kutoa kwa Mheshimwa Kenneth Nollo.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, mi nataka nimpe taarifa mzungumzaji. Nadhani anajaribu kutoa opinion, tangu kule alivyosema kwenye mafuta na hata huku. Na kitendo cha kuanza kutaja kampungi hii inalipa this amount, this amount ni kama anataka kusema kama kuna uonevu. Kwa hiyo hoja yake ya msingi hapa angejaribu kusema hapa labda alternative kwamba tutafute kampuni nyengine lakini anachokifanya hapa ni kwamba hawa wanalipa kiasi hiki, as if watu wanaonewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nimpe taarifa, anajua mchakato mzima tulivyompata mtu wa kuweka stamp za TRA na lilivyokuwa jambo gumu. Kwa hiyo kinachotakiwa aelewe kwamba hiyo opinion anayoitoa ni kutafuta suluhu ya namna nyingine na asifanye kama kuna kuibiwa. Ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee unaipokea taarifa hiyo?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokizungumza hapa sina tofauti na alichokizungumza Mheshimiwa Tabasam the other day kuhusiana na utaratibu huu huu kwenye mafuta; hakuna tofauti na alicho zungumza mbunge wa Gairo, kuhusiana na utaratibu huu huu kwenye mafuta. Na tunazuzngumza hapa ili kuiambia Serikali kupitia wataalamu wetu; na nilisema hapa, dhamira ya ilikuwa ni nini njema, kuweza kujua bidhaa zinazozalishwa, lakini dhamira njema mkijua kwamba mlichemka mnatakiwa mnakaa mnajitathmini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoa mfano kwamba, tulimchukua mkandarasi …

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee kuna taarifa kutoa kwa Mheshimwa Stanslaus Nyongo.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimwai Naibu Spika, napenda tu kumtaafu Mheshimiwa Mbunge, kwanza kabisa yeye mwenyewe ni mjumbe wa Kamati ya Bajeti, na haya yote yamepita kwenye kamati ya bajeti. N kuhusu suala la ETS imekuwa raised kwenye Kamati ya Bajeti na Serikali imekuwa ikisimamia na kupambana na suala hili ili kuhakikisha kwamba inakuwa na faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine na cha mwisho, ameonesha kama kuna difference ya eight billion, difference ilikuwa ni kubwa, nia ilikuwa ni njema kama anavyosema, sema kiwango kimekuwa kidogo. Yeye akubali, na yeye ni mjumbe wa Kamati ya Bajeti aendelee kuishauri Serikali vizuri kuliko kushutumu watu wengine wamechemka ilhali na yeye mwenyewe ni sehemu ya kuchemka. Ahsante sana. (Makofi/ Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee unaipokea taarifa hiyo?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mimi sikuchemka kwa sababu mimi sikuwa sehemu ya mkataba uliotengenezwa wala hata siujui. Pili kuwa mjumbe wa Kamati ya Bajeti hakunizuii mimi kuchangia bungeni, na nimelichangia hili ili kutambua hatua ambayo Serikali imechukua kwa kuondoa jukumu la vinasaba kwa mtu binafsi, imerudishwa Serikalini, kwa hiyo pesa inarudi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ninaitaka Serikali; na uzuri Mheshimiwa Mwigulu anasikiliza, nataka Mhesnishiwa Mwigulu hili la ETS ulitoe huko kwa mkandarasi aliyepo sasa, kwa sababu tumeshapigwa vya kutosha, turudishe ama Serikalini, na kama Serikali haina teknolojia ya kutosha tufanye ushindani watu waje tupate mtu mwenye gharama nafuu. (Makofi)

Meshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha pili cha sigara, kwa mwaka mmoja kimelipa bilioni 14, kiwanda kimoja. Tukizungumza hivi viwanda vidogo vidogo ni bilioni tatu biloni nne, bilioni nane; ukijumlisha unaweza ukakuta wakati TRA mmeongeza si pungufu ya bilioni 20, mwenzenu huku kwa vile viteknolojia vya kudonoa donoa tu na kuweka nembo, amepata bilioni 400 labda, hivi hii ni busara. Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, nitakuomba tu unijibu kwa sababu kiukweli tunapigwa pigwa sana, na si busara kukubali kuendelea kupigwa pigwa, na mimi najua wewe hupendi tupigwe pigwe. (Makofi)

Meshimiwa Naibu Spika, la pili. Mpango wa kwanza na wa pili tulifeli kwa sababu, kwanza hatukuwa na mtiririko wa fedha za kutosha, pili hatukuwa na takweimu za kutosha. So, mimi ninasikiliza ndugu zangu Wabunge hapa, kila mtu anasema Bungeni hapa, ooh sijui jimboni kwangu inakuja milioni 500, tunapiga makofi, yaani tunawahisha shughuli. Lakini Nheshimiwa Mwigulu unajua, kwamba kwenye bajeti yako wewe ambayo tunaimaliza sasa ni ya mtangulizi wako. Tulipanga kwa miaka hii yote kwa mikopo kwa mambo yetu yote ya ndani tuweze kukusanya trilioni 34. Juzi hapa unatusomea hotuba yako umeweza kukusanya trilioni 24, kuna deficit ya trilioni 10. Hivi kweli nisaidie; ni muujiza gani huu utakufanya Mheshimiwa Mwigulu na Serikali muweze kukusanya 10 trillion ndani ya miezi miwili? Pili, kama unajua ulishindwa mwaka jana hivi kweli ni busara kwenda kusema kwamba unaweza kukusanya trilioni 36, hivi ni busara?

Meshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu Wabunge wadogo zangu asilimia 70 hapa ni wageni, hizo 500 msipige kofi, tutakutana mwakani hapa tutaanza kutoana macho. Kwa sababu kwa mtindo wa ukusanyaji wa aina hii, naomba Waziri uje utuambie kuna miujiza mengine itakayokuja, lakini kwa utaratibu huu, siku zote nawaambieni tukiwa wakweli kama unauwezo wa shilingi mia, jipangie kwa shilingi mia yaki ili sasa tuendelee kuishi kwa matumaini, sio unaweka shilingi mia unakusanya buku unasema mimi naweza kukusanya elfu moja, wakati unajua ndugu yangu mia ndio saizi yako…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: haya ahsante sana Mheshimiwa Halima Mdee muda wako umeisha ahsante sana.

MHE. HALIMA J. MDEE: …. Kwa hiyo tuwe wakweli tuweze kulisaidia taifa hili. Nitaomba majibu mahsusi kwa ETS…

NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa Halima Mdee, ahsante sana, shukran.

MHE. HALIMA J. MDEE:… nashukuru sana. (Makofi)