Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Niipongeze Serikali kwa mpango mzuri ambao imetuletea. Pamoja na kuipongeza kwa sababu imekuwa ni bajeti ambayo imekwenda kugusa maeneo muhimu sana ya wananchi wetu na kutatua changamoto za wananchi wetu, lakini bado nina mchango katika sehemu tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwenye suala linalohusu elimu, kwa kuwa ili tuendelee tunahitaji tupate watu ambao watakuwa na elimu bora. Niombe sana katika mabadiliko ya mtaala wenzetu watu wa elimu waangalie na kuzingatia mazingira yetu ya Tanzania na kuona namna gani vijana wetu watafundishwa ili waweze kupambana na mazingira ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia na elimu yetu imekuwa nadharia sana, sio ya vitendo. Watoto wanakaa darasani muda mwingi sana, hawana practical, kwa hiyo wanapotoka inakuwa ni shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipo kipengele cha ujasiriamali, ni cha muhimu sana, mtoto lazima ajifunze kuwa ana maono au ana vision tangu kwenye elimu ya msingi. Kwa hiyo lazima tuangalie namna gani tutaingiza kipengele hicho kwenye elimu yetu ili tuwe na watoto wenye mipango kuanzia wadogo watengeze road map ya maisha yao kuanzia shule ya msingi mpaka watakapomaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno niende kwenye suala lingine linalohusiana na masuala ya miundombinu, leo tunajadili bajeti ya Serikali, lakini zamani wakati Taifa letu linaanza kwenye nchi hii tuliwahi kuwa na program ya vijiji vya ujamaa. Nia ilikuwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii katika mipango yetu ya ardhi hata tunapokuwa kwenye shughuli zetu za kisiasa kutafuta kura, unaweza ukaona kwamba tumeacha sasa ile program atuangalii ni namna gani tunawapanga watu wetu kwa makazi na namna gani tunaigawa ardhi yetu kwa ajili ya masuala ya kilimo na kazi zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanaondoka, anakwenda anahamia kwenye mlima alikuwa mwindaji, anahamia huko analeta na mke wake na watoto wanazaliana wako mbali juu ya mlima na hakuna mamlaka yeyote iliyowaambiwa jamani hapa sio sehemu ya makazi, mrudi mkakae na wenzenu. Hii inazidi kutuongezea gharama na ndio maana sasa kumfuata yule mtu ili umpelekee huduma ya barabara, maji, afya ni mbali, yuko mbali na wenzie lakini tayari anataka kupata huduma kutoka kwenye Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweka bajeti ya kujenga barabara kumfuata mtu au kuwafuata watu 600 ambao wako mbali, unatumia zaidi ya bilioni sita au nane na wale watu wamekaa kule wanalima mbogamboga, ukiangalia return kiuchumi pale ni hasara. Kulikuwa kuna sababu gani hawa watu wajitenge na wenzao waende mbali wakaishi peke yao, wakati wangeweza kuishi na wenzao, tukaweza kuwahudumia vizuri pale, wakiwa wamekaa pamoja. Kwa hiyo tunaomba wenzetu hawa wa ardhi waliangalie hilo na mipango yetu iwe hivyo makazi lazima yaimarishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, duniani hawafanyi mambo mapya ila wanafanya mambo yaleyale katika ubora zaidi. Leo hapa tumevaa nguo lakini ni sawa tu na Adam na Eva walivyokuwa wanavaa nyasi, wao walivaa nyasi direct, magome ya miti na walivaa ngozi moja kwa moja, lakini sisi tunavaa ngozi zilizokuwa processed, vinakuwa viatu. Leo tunavaa magauni kutoka kwenye mimea ya pamba. Hicho ndicho tunachosema hatukutakiwa kuacha zile program za Vijiji vya Ujamaa, lakini kuitengeneza ile program iwe ya kisasa na kutusaidia zaidi kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, point yangu nyingine naomba leo kidogo tukumbushana na maneno ya Mungu humu ndani. Kwa sisi wa kristu wenye biblia ya Isaya 32 mstari wa 17 unasema: “Haki kazi yake duniani imetumwa kuleta amani, haki kazi duniani imetumwa kuleta utulivu na matumaini.”

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndio kazi kubwa ya haki tunaomba sana wenzetu hawa walioko Serikalini, tunapoongea watusikie na wafanyie kazi. Yapo mambo waliyofanyiwa Watanzania wenzetu kwenye nchi yetu hayana tija na yamewajeruhi na hayana tija kwa maendeleo na mustakabali wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tumeongelea sana hapa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni. Wenzetu wale wengine ukiangalia ni wajane, wenzetu wale wengine ukiwaangalia walianzisha zile biashara baada ya kupata viinua mgongo vyao, wengine walianzisha zile biashara mitaji waliipata kwa shida. Ni kweli kama Kamati ya Kudumu ya Bunge inavyosema katika Sura ya 56 ya bajeti yake na mapendekezo yake, kile kipengele cha 8.4, kwamba kulikuwa na lengo la Serikali la kuhakikisha kwamba haya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yanafuata sheria za Serikali na kanuni za Benki Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, operation iliyofanyika kwenye yale maduka, watu hawa bado hawakutendewa haki, tunaomba haki itendeke kwa sababu mwenye kuhukumu kwenye suala la haki ni Mwenyezi Mungu. Nchi yetu tumejipambanua sana kwamba tunamtegemea Mungu na hatuna ubishi kwenye hili. Ni kweli Mwenyezi Mungu ametusaidia na tumeona alivyotupigania hata wakati wa janga la corona, sasa basi sisi kama viongozi tufanye hiyo practice kwa matendo, kama tunamheshimu Mungu tuheshimu na watu aliowaumba sisi tuwaongoze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwatendee haki wale watu wanaolia kwa ajili ya vitu vyao walivyochukuliwa, fedha zao zilizochukuliwa, mali walizochukuliwa warudishiwe. Wenzetu TRA tunawaomba sana, wakati fulani unakuta Mheshimiwa Rais namshukuru sana, kwa sababu alitoa kauli mwenyewe, kwamba kweli tunahitaji kodi, lakini hatuhitaji kodi ambayo ni ya dhuluma. Tunahitaji kukusanya mapato, lakini hatuhitaji ya dhuluma ndani yake. Tukusanye mapato ambayo hata tunapokwenda kumwomba Mwenyezi Mungu atusaidie, atatusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaomba wenzetu wa TRA kwanza wawe wanaelewa, leo hii Mheshimiwa Rais anatoa kauli kwamba sasa kodi zote za miaka ya nyuma, miaka sita au saba iliyopita jamani basi, ukienda TRA ndio kwanza wanatoa demands note za kuwadai watu kodi miaka nane au tisa iliyopita. Unawauliza hili likoje, wanakuambia sisi tupo tunafuata maelekezo na sheria, ni kweli kauli ilitolewa kisiasa, lakini sisi tunafuata mwongozo, tunataka maelekezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Rais anapokuwa anatoa, ameshafanya uchunguzi wa kina, kwa sababu yeye ana milango mitano ya fahamu ana vyombo vimeshamsaidia mpaka anafikia hatua ya kutoa tamko. Kwa hiyo wenzetu wafuate mambo ambayo tunawaambia tutende haki kwenye Taifa letu, tuwatendee haki, hii iendane na kesi zingine za biashara. Wapo wafanyabiashara wengi waliofanyiwa vitu vingi ambavyo havikuwa sahihi. Tunaomba sana kero zao zitatuliwe kesi zao na mashtaka yao yaangaliwe kwa kina ili kama kuna uonezi wowote uliofanyika, watu hawa waweze kusaidiwa na warudishwe kwenye hali ya kawaida ili tuendelee kujenga imani kwa wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la elimu, tumejipambanua kwamba elimu yetu haina ubaguzi na mimi hapa naomba niseme tumesema tunataka Watanzania washiriki kwenye uchumi, lakini wapo wawekezaji waliowekeza kwenye nchi hii kwenye sekta ya elimu, wamejenga shule, wamejenga vyuo, lakini namna ambavyo wakati mwingine tunawachukulia, hatuwachukulii kama ni watu ambao wanatusaidia kama Serikali kutoa huduma kwa jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuwachukulie kama ni watu ambao wamechukuwa nafasi ya Serikali kuwahudumia wananchi na wao wana-feel gap ya kutoa elimu kwa wananchi. Kwa hiyo suala la kutoa elimu bure, tuwasaidie basi hata hawa private pamoja na kwamba wao au shule binafsi wanachaji ada, leo Serikali inashindwa nini hata kuwachangia gharama za mitihani tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale ni Watanzania wanaolipa kodi na walikuwa na haki ya kusoma kwenye public schools au kwenye shule zetu za Serikali, lakini wameamua kusomesha watoto wao kwa gharama na ndio walipa kodi wazuri wa nchi hii. Kwa nini leo shule ina wanafunzi 10 kwa sababu haijafikisha wanafunzi 35 inatakiwa ilipie wale wanafunzi 25 ada za mitihani hata kama hawapo. Kwa hiyo, katika nchi hii bado tuna malipo hewa kwenye elimu, imefanyika michakato ya wafanyakazi hewa, lakini sisi kwenye sekta ya elimu na Wizara ya Elimu bado watu wanalipa ada za mitihani hewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisema hivi namaanisha kwamba, ikiwa huna watoto 35, una watoto 10 unachajiwa fedha ya watoto 35. Hawa watu wanawekeza return on investment kwenye elimu inachukua miaka 10, ndio mtu aanze kupata faida kwa hiyo tunawaomba wenzetu wa Wizara wajue hawa ni partners wetu, hawa ni Watanzania, wamewekeza kwenye elimu, tunaomba wasaidiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyaraka za elimu pia ziangaliwe. Tuna tatizo kubwa sana tunaweza kuona la kawaida, leo tunatangaza shule zote zitafunga tarehe 30 mwezi wa Sita, tunaomba tuulizane maswali, je, miundombinu ya kuwasafirisha wale watoto wetu kutoka kwenye mashule kwenda kwa wazazi wao tuna uhakika ipo?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto kubwa unakutana na watoto wamelala stendi, Mbunge unapigiwa simu sijui watoto wa shule gani wamekosa basi wamelala stand au mabasi ndio yametolewa mabovu wakati ule, wamepakiwa watoto wetu wanalala njiani unapigiwa, usalama wao unakuwaje? Kwa sababu mabasi yanayotumika ni yale yale ambayo siku zote ndio yanasafirisha abiria. Yakitoka mengine ni mabovu kwa sababu hakuna mtu atakayenunua basi asubiri tu msimu wa shule kufunga asafirishe tu wanafunzi. Kwa hiyo watu wa wizara tunaomba watusaidie katika waraka mbalimbali wanazozitoa na maelekezo wanayoyatoa, basi wawe wanaangalia na mazingira na hali halisi ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno haya, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)