Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Kwanza nianze kusema tunaipongeza sana Serikali kwa vile ambavyo wameandaa bajeti yao kwa kuzingatia maoni mengi ya Wabunge na wamewatendea haki kwa sababu kazi za Mbunge ni pamoja na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana mama kwa namna ambavyo anaendelea kusikiliza na kupokea michango ya vijana wa Tanzania. Tarehe 22 mwezi wa Tano nilisimama kwenye Bunge hili Tukufu na kuchangia kuhusiana na mambo ya blockchain technology, cryptocurrency na digital currency na tarehe 13 mwezi huu mama aliweza kutoa kauli na kuwaomba BOT waweze kuendelea kufuatilia teknolojia hii kujifunza ili nasi tusiweze kupitwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wito huu wa mama umepelekea kufanya aingie kwenye orodha ya marais wachache ambao wameonyesha kuongea kitu kikubwa sana duniani na kuunga teknolojia mpya ambayo inaweza ikaleta uchumi mkubwa lakini kuongeza ajira kwa vijana lakini na kuchochea uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya kufupisha muda naomba niendelee kuiomba Serikali na kuishauri kwamba, BOT whether taasisi zozote za kifedha kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, watakapokuwa wanaunda Kamati zao tunaomba ushirikishi kwa vijana wa Kitanzania ambao wanauelewa ili waweze kuwasaidia, lakini elimu iendelee kutolewa kwa sababu elimu ni bure itawafanya Watanzania hawa waweze kuelewa na wasiendelee kudanganywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo naomba, wakati tunaendela kusubiri BOT waendelee kuamua na kujifunza kwamba uko mfumo ambao unatumika kwenye hizi online business, unaitwa PayPal. Ikiwa kama BOT imekubali kwamba Watanzania hawa waweze kulipa kwa kutumia PayPal, lakini wao hawawezi kupokea malipo kwa kutumia PayPal, tunaomba basi BOT tena waone namna gani watawasaidia hawa vijana wa Kitanzania ambao wanalazimika kutoa hela nje ya nchi, lakini wao hawawezi kupokea na wanalazimika kutumia nchi za jirani kulipwa na hivyo kupoteza mapato yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri wangu mwingine kwa Serikali kuhusiana na teknolojia ya miundombinu. Hapa nataka kuongelea nanofiber technology, kwa ajili ya muda nitafupisha tu, kwamba, teknolojia hii ina faida nyingi sana na ina faida nyingi sana especially kwa barabara ambazo zinatusumbua vijijini sisi Wabunge ambao tunatokea vijijini. Hata hivyo, teknolojia hii inaweza ikatumika hata mjini nanofiber technology wataalam wanasema kwanza ina PSI 11,000, kwa hiyo ina maana kwamba ina uwezo wa kuhimili kiwango ambacho lami haiwezi kuhimili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lami jua linapowaka magari makubwa yanapopita inatengeneza vitu kama mbonyeo. Kwa hiyo inapelekea Serikali kupoteza hela nyingi inapokuwa ina-maintain zile barabara, lakini nanofiber technology, Serikali itakapoamua kuitumia inaendana na mazingira yote hata kwenye zile mbuga zetu za wanyama ambako hatuwezi kuweka lami kwa sababu tunaogopa teknolojia ambayo tunatumia sasa ina emission, lakini teknolojia hii iko vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii nanofiber technology ina uwezo wa ku-save gharama ambazo zinatumika kujengea lami za sasa kuanzia asilimia 25 mpaka asilimia 50. Kwa hiyo unaweza ukaona ni kwa kiasi gani Serikali itakapoamua kutumia teknolojia inaweza ika-save mapato yake, sitaweza kuendelea nitaandika andiko kwa ajili ya muda ili niseme vitu vingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba kuchangia kwenye suala la miradi hii ya kimkakati na nifupishe. Kwenye hii miradi ya kimkakati naomba niongelee mradi wa kimkakati ambao uko ndani ya Jimbo la Mwomba mradi wa chumvi. Kwenye soko letu la Tanzania inaonyesha kwamba kiwango cha chumvi ambacho Tanzania inahitaji ni tani milioni moja na laki tatu na kuendelea, lakini viwanda vyetu vya ndani kwa mfano Uvinza; viwanda vilivyoko Pwani au viwanda viliko huko Lindi vina uwezo wa kutengeneza tani za chumvi 270,000 tu. Kwa hiyo Serikali inapelekea Serikali kuangiza chumvi nyingi kutoka Nchi za Kenya na zingine ili tuweze kutosheleza soko la ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ikiwa miradi hii ya kimkakati tuliileta kwa lengo tu kwamba iweze kuzisaidia halmashauri kuongeza mapato yake, lakini iweze kutoa ajira kwa Watanzania na tuweze kuimarisha viwanda vyetu vya ndani, tunaomba Serikali irudi na kupitia tena kuangalia miradi hii ya kimkakati ikiwa ni pamoja na hiki Kiwanda cha Chumvi ambacho kipo Ivuna kwenye Jimbo la Momba. Wakati kiwanda hiki kinaendeshwa na TRC kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani mpaka 25,000, lakini toka kiwanda hiki kimerudi kwenye mradi wa kimkakati kinazalisha chini ya tani 100. Kwa hiyo tunaomba Serikali ipitie tena ili tuweze kunufaika na miradi hii ya kimkakati, iweze kwenda kutimiza lengo ambalo lilikusudiwa kwa Watanzania hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)