Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi ili niweze kuchangia katika mapendekezo ya bajeti ambayo yamewasilishwa kwetu kwa nafasi ya pekee nikushukuru kwa nafasi lakini pia nimshukuru Rais wetu, Mama yetu mpendwa, Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuja na bajeti yake ya kwanza ya Awamu ya Sita ambayo kwa kweli inalenga kabisa katika dhima ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, salamu hizi za pongezi zimfikie Rais, lakini ziwafikikie wasaidizi wake askari wake wa miavuli ambaye ni Waziri wetu wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mwigulu Nchemba Madelu, lakini pia na msaidizi wake Mheshimiwa Masauni Masauni na watendaji wengine wa Serikali bila kusahau michango ya Waheshimiwa Wabunge, Kamati ya Bajeti ambayo inaweza kuboresha mpaka bajeti yao inakuja imesheheni maono mazuri kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia katika maeneo mbalimbali, nikaona kwamba bajeti yetu hii inaakisi na imeweza kugusa katika makundi mbalimbali ya wananchi ndani ya nchi yetu na hakuna kundi lilobaki. Tumeona katika maeneo ya watumishi ni maeneo mengi ambayo yameguswa kwa ajili ya kuhakikisha sasa watumishi wanakuwa na ari ya kazi kwa kuweza kutenga fedha kwa ajili ya kuwapandisha vyeo, zaidi ya bilioni 449 zinatengwa katika bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sisi wote tuunge mkono Serikali kwa kuzipitisha kwa kishindo. Pia tunaona, PAYE, kodi ya mshahara wa mtumishi inapunguzwa kutoka 9% kwenda 8%. Ni mambo mengi mazuri kwa watumishi ambaye tumeona katika Jeshi letu la Polisi, muda wa kuajiriwa katika mkataba wa kudumu unapunguzwa kutoka miaka 12 kuja miaka sita. Tunaona Watendaji wa Vijiji wakipewa posho na Maafisa Tarafa Sh.100,000 kila mwezi. haya ni mambo ya kumshukuru Rais wetu mpendwa, lakini na maono mazuri ya wasaidizi wake, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuja na mambo mazuri ambayo yanagusa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika eneo hilo tumeona kundi la wanasiasa nalo limeguswa kwa kuona kwamba wawakilishi wa wananchi ambao ni Waheshimiwa Madiwani, na wenyewe posho zao zitoke Mfuko Mkuu wa Serikali Hazina. Mtu ambaye hawezi kuelewa umuhimu wa suala hilo, mimi katika wakati wangu wa maisha niliwahi kutumika kama Mkurugenzi. Nilipoenda kwenye Halmashauri hiyo, nilikuta Waheshimiwa Madiwani hawajawahi kulipwa posho zao kwa miezi 12. Kwa hiyo, ilikuwa ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naona Serikali imekuja na njia Madhubuti ya kuweza kutatua tatizo hili ambalo lilikuwa la muda mrefu, kuhakikisha Madiwani wetu wanalipwa kwa wakati. Kwa hiyo, niendelee kumpongeza Rais wetu, Waziri pamoja na Naibu Waziri na watendaji wengine ambao wamewezesha hili suala kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa ajili ya vijana wetu. Vijana hawa tunawawezesha kupitia asilimia nne za Halmashauri; tunawapa mikopo wananunua bodaboda na wengine wanaajiriwa na wenye bodaboda. Kwa siku moja, kijana wetu anayeendesha bodaboda kipato chake ni shilingi 7,000 mpaka shilingi 10,000. Akikutana na faini ya shilingi 30,000 aidha bodaboda hii anaitelekeza au anaiacha hapo kwa siku nne anakimbia kazi. Kwa hiyo, kwa shilingi 10,000 hata akikopa, maana yake anajua ndani ya siku mbili anaweza kurudisha hizo fedha. Tuendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais na Wizara kwa michango mizuri ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa kundi la wananchi ambalo Serikali imeliona hasa kwa kuangalia yale maeneo mahususi kwenye maeneo ya maji, barabara, afya na Bima ya Afya kwa Wote pamoja na uboreshaji wa elimu. Katika eneo hili tunaona tunakwenda kuchanga shilingi mia moja, mia moja katika kila lita ya dizeli na petroli. Ni suala ambalo ni zuri. Naiomba Serikali iendelee kulisimamia ili sasa wenzetu wanaomiliki vyombo vya usafiri wasije wakaona ni sababu ya kupandisha gharama za usafirishaji. Kwa hiyo, Serikali iweze kutoa bei elekezi za nauli na gharama za usafirishaji ili isije ikawa ni mzigo tena kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili, tunaona tozo ya shilingi 10 mpaka shilingi 10,000 kwa muamala wa fedha wa kutuma na kutoa, lakini tozo ya shilingi 10 hadi shilingi 200 kwa laini ya simu ambayo tutaweka fedha; eneo hili niseme, Waheshimiwa Wabunge huku sisi wote ni mashahidi. Wote katika eneo hili tunakubali kuchangia kwa kuwa kila Mbunge hapa leo anaweka na kutoa fedha. Kwa nature ya wateja wetu tulionao, kwa siku wanapiga simu nyingi kulingana na wateja wetu tulionao katika majimbo yetu, lakini kila Mbunge hapa yuko tayari kutoa hizo fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuwasihi na wananchi wetu wapendwa, suala hili ni zuri. Tunachoomba sasa Serikali iendelee kusimamia vizuri katika eneo hili, barabara zijengwe, maji yafike kwa wananchi, umeme ufike, lakini pia na bima kwa afya kwa wote iweze kufika kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)