Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon Norah Waziri Mzeru

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali. Kwa dhati ya moyo wangu nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu kipenzi Mama Samia Suluhu Hassan, nampongeza Rais kwa juhudi zake anazozichukua siku hadi siku pamoja na kutupa kipaumbele hasa sisi wakina mama wa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza tena Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua Dkt.r Philip Mpango kuwa msaidizi wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ninampongeza Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge hili kwa kutuendesha vizuri katika shughuli zetu za Bunge.

Nampongeza pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa umahiri wake wa utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, namuombea kwa Mwenyezi Mungu aangalie uzima wa afya yake na amani katika maisha yake ya kila siku pia nampongeza Waziri wa Fedha – Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake Engineer Masauni pamoja na Katibu Mkuu na viongozi wote waandamizi wa Wizara hii ya Fedha na Mipango na pia naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa kushirikiana na Wizara kwa kutuleta bajeti ambayo imekidhi kiwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imegusa maslahi mapana ya Taifa letu, naamini itawanufaisha Watanzania kwa ujumla, sina budi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kiujumla, lakini naomba kuchangia kwa ufupi kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini bado hairidhishi. Maji hayana mbadala, maji ni uhai, maji ni maisha kwa viumbe hai vyote, bado vipo vijiji ambavyo havina kisima hata kimoja cha maji safi na salama na badala yake hutumia maji ya mapalio, maji ya madimbwi, maji ya mito wanayochangia na Wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina vyanzo vingi vya maji mfano Mkoa wa Morogoro kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, lakini vyanzo vingi vya maji vimeanzia Mkoa wa Morogoro na kutumika katika baadhi ya mikoa mingine na si kuwasaidia wakazi waliopo vijijini ndani ya Mkoa wa Morogoro; kwa mfano Bwawa la Kidunda liliopo Wilaya ya Morogoro Vijijini nalo lingekuwa msaada mkubwa kwa wanakijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu iweke nguvu katika sekta ya maji ili tuweze kumtua ndoo ya maji mama kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa ufupi niongezee katika upande wa elimu; kuna changamoto kubwa katika upande wa madarasa na madawati, madarasa mengi yamekuwa chakavu na mlundikano wa watoto katika darasa moja linakuwa na wanafunzi zaidi ya 100 na Serikali imeona muitikio mkubwa wa wanafunzi kusoma kutokana na elimu bila malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu naomba kuwe na mkakati maalum kwa watoto wanaohitimu darasa la saba kwenda kidato cha kwanza kuhakikisha wanakuwa na madarasa na si kuanza ujenzi wa madarasa kipindi watoto wanataka kuingia shuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja Ahsante.