Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RIZIKI S. MNGWALI. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze nami kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia hiki alichotujalia ambacho hatukukipata kwa ujanja wetu, bali matakwa yake. Pia nikishukuru chama changu kwa kuniamini na kunifanya na mimi kuwa miongoni mwa wawakilishi wake hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pale ambapo aliishia au point ambayo aliisema Mheshimiwa Jesca kuhusu suala la utawala bora, lakini naongeza pale kwamba huu Mpango wote umejiegemeza kwenye hali ya utulivu na amani. Sasa hili ni jambo ambalo tumekuwa tukiliimba sana Watanzania. Wataalam wa masuala ya amani wanatuambia negative peace siyo peace ya kujivunia. Kwamba kusema nchi haina vita, halafu mkajidai kwamba mna amani, nchi hii haina amani ya kuweza kuhimili mipango kama hii. Hiyo inawezekana imechangia kushindwa kwa hiyo mipango ambayo tulikuwa nayo huko nyuma ambalo si tatizo kuwa na mipango Tanzania bali ni utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukawa na mipango kama huna utawala bora. Suala la Zanzibar tumelisema humu, nalisema na tutaendelea kulisema, si sahihi Serikali ya Muungano kukaa kimya wakati inaona hali ya usalama Zanzibar inazidi kudidimia. Tunarushiwa taarifa kila siku, watu sijui wanaitwa mazombi, kule nyuma mnakumbuka kulikuwa na kitu kinaitwa janjaweed, wana-terrorize watu katika mitaa ya Zanzibar, Serikali ya Muungano imekaa kimya, tunaimba tuna amani, hatuna amani kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora hauendi, labda mtueleze Serikali Kuu, kwa nini hatuna Meya Jiji la Dar es Salaam mpaka leo? Kwa nini mnashindwa kuthamini mapenzi na mapendekezo na maamuzi ya wananchi? Hilo ni kwamba nasema mpango wote huu umejiweka mahali sipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala maalum machache ambayo pia ningependa kuyazungumzia. Suala la miundombinu kwa mfano, kumetajwa humu bandari na niliwahi kusema hapa wakati ule wa semina, kwamba tunajivunia vipi sisi bandari zetu au tunazitumia vipi sisi bandari zetu kuonesha kwamba kweli, tunanufaika na eneo letu au kuwepo kwetu kijiografia. Nchi ambayo ina pwani ndefu tu, lakini pia tumezungukwa na majirani wengi ambao ni land locked countries. Sasa hii economic diplomacy yetu inakwenda wapi ikiwa tunashindwa kutumia fursa hata hizi ambazo tunazo kihistoria. Nchi zinazotuzunguka tuna historia nazo ndefu za mahusiano, lakini tumeshindwa kutumia nafasi yetu hii ya kijiografia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miundombinu pia wakati mwingine naona kwa mfano, kwenye mwelekeo; kama kunazungumziwa au kunatajwa variables mchanganyiko. Kwenye eneo la anga wakasema katika mambo yaliyofanyika ni kujenga uwanja wa ndege wa Mafia. Sasa ule uwanja wa ndege wa Mafia ni kwa ajili ya watu wa Mafia au wale watalii wanaokwenda kule na ni ndege gani hizo hizi za tropical sijui za watu 12, 13 hizi. Ndiyo kweli tunaeleza kama ni success story! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mafia wanaendelea kudhalilika na usafiri, usafiri wa maji ni mbovu kabisa, wala hatujui kwa nini Serikali bado inaendelea kuangalia hali kama ile. Ndege siyo ile inayozungumziwa hapa na kiwanja cha Mafia kile siyo kwa manufaa ya watu wa Mafia. Kwa taarifa yenu tulishaahidiwa uwanja wa Kimataifa wa ndege na wala hatujauona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukusanyaji wa mapato. Ukiangalia sioni jipya, mpaka wanazungumzia sasa kuhakikisha, kuorodhesha ile, kwamba majengo yote, sasa haya mambo mbona ni yale yale tu, hakuna jipya kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, specifically pia nataka kuzungumzia hili suala la kuondoa utaratibu wa retention. Jamani tunataka kuua na hizi Taasisi. Sasa Serikali hii ya Awamu ya Tano ni mabingwa wa kushtukiza, sasa nawaomba wazee wa kushtukiza, msishtukize kwenye retention. Taasisi hizi zilipokuwa zina-retain some money, angalau zilikuwa zinajiendesha jamani, OC haiendi kwenye taasisi hizi miezi mitatu, minne mpaka mitano. Sasa mnatarajia ziende vipi hizi Taasisi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kuna mwalimu alirudisha watoto wa boarding nyumbani, akasema hana chakula, wakamjia juu hapa, ndiyo hali halisi. Hizi taasisi za umma, kikiwemo Chuo cha Diplomasia, mimi nimetoka kule na tulikuwa tuna hali ngumu, OC haziji halafu mnaondoa na retention, naomba mkae makini kabisa, msije mkaziua na hizi taasisi, mkazikosesha uwezo wa kufanya kazi na kutimiza majukumu yao ambayo mmewapa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya. Orodha hii hapa inasema lakini sioni wapi wamezungumza specifically kuweka wafanyakazi wenye sifa vile inavyopaswa. Huwezi tu ukazungumzia kwamba nitahakikisha dawa zinapatikana. Hivi mnajua kuna zahanati ambako wale watoa dawa hawana sifa za kutoa dawa na siyo tu kwamba anatoa dawa yeye ndiye anamwona mgonjwa halafu yeye ndiye anasema wewe mgonjwa ukapimwe nini, halafu yeye anainuka anakwenda kumpima mgonjwa na kisha anasoma kile kipimo alichopima mwenyewe, halafu anakuja kuandika dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suala si dawa tu, hizi dawa nyingi kwenye zahanati zetu huko kwingine, ni sumu kwa sababu zinatolewa na watu ambao si wenye sifa. Zahanati kadhaa Mafia zinahudumiwa na wahudumu wa afya, sio hata matabibu au wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jamani tuwe makini, kwa sababu huu mpango wenyewe wote unasema pamoja na yote lakini unataka maendeleo ya watu. Maendeleo ya watu gani hayo ambao wale tulioko pembezoni, Mkoa wa Pwani pembezoni, sasa Mafia pembezoni mwa pembezoni. Haitufikii mipango kama hii, haionyeshi kwamba humu kweli yale masuala mahususi yanayotajwa au yanayogusa au yanayoathiri maisha ya wale maskini zaidi au walio pembezoni zaidi yanabebwa katika mipango kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie labda la mwisho, nizungumzie suala ambalo niliacha kulitaja pale kwenye miundombinu, kwamba tunaposoma watu wa Mafia kwamba kinatafutwa kivuko cha Dar es Salaam – Bagamoyo, wakati sisi hatuna meli ya kututoa Mafia kutuleta Dar es Salaam, tunaona tunazidi kunyanyasika katika nchi yetu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yenu tu niwaambie kwamba kuna gati kule limejengwa la mabilioni na limekamilika toka mwaka 2013 lakini mpaka leo hii wananchi wa Mafia hawana usafiri wa kuaminika wa meli na humu sioni ile investment yote ile imetajwa itashughulikiwa vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana mwanafunzi wangu mwema wa Chuo cha Diplomasia. (Makofi)