Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipatia nafasi hii kuweza kuchangia kwenye mpango huu wa maendeleo wa Tatu wa Taifa.

Nheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo analifanyia Taifa letu. Majuzi hapa tumeona tumepokea fedha Trilioni 1.3 ambazo fedha hizo zimegawanywa katika kila Jimbo la Mbunge aliyemo humu ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunakwenda kujenga madarasa kila Jimbo, kulikuwa na kero kubwa sana ya madarasa na ilikuwa ni hoja ya kila mwaka inajirudia madarasa, madarasa ambapo ilikuwa wakati mwingine tunachangisha wananchi wetu. Michango hii tulikuwa tunachanga wananchi kule kijijini wakati mwingine walikuwa wanakimbia kijijini. Mwingine alikuwa anaamka saa nane usiku anamkimbia Mtendaji wa Kijiji/Kata kwa sababu ya mchango wa kujenga madarasa. Kupatikana kwa madarasa haya imekwenda kuondoa adha ya michango ilikuwepo utitiri wa michango kwenye ujenzi wa madarasa, nampongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia mmoja wa Wabunge wakati anachangia jana akasema tunapiga makofi kwa Trilioni 1.3. Kwa historia yetu toka tupate uhuru hatujapata fedha za kujenga madarasa mengi kwa kiwango hiki, haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha Mheshimiwa Mbunge yule kubeza fedha hizi hakikuwa cha kiungwana. Fedha ni nyingi, tunajenga madarasa kila kata na kama unavyojua, kila Kata katika nchi hii tuna shule za sekondari. Kwa hiyo tunakwenda kujenga haya madarasa na mpaka kwa huyo Mbunge tunaenda kujenga madarasa, tunajenga madarasa kila kona na pembe ya Nchi hii. Huwezi kubeza,
1.3 Trilioni zilizokuja kumwagika kwenye Majimbo yetu. Mimi hapa Jimboni kwangu natembea navimba, navimba kwa madarasa haya ya Mama Samia Suluhu Hassani, kwa hiyo nampongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikuishia madarasa, tumepata fedha kila Mbunge hapa milioni 500 za maji. Unabeza vipi Trilioni 1.3 ambazo hazijawahi kutolewa kwa kipindi kifupi tunakwenda kujenga ndani ya miezi sita mpaka tisa kukamilisha project hii kubwa. Tumepata fedha za kununua mitambo ya kuchimba mabwawa makubwa kila Kanda ya nchi yetu imepata, unawezaje kubeza Trilioni 1.3 za Corona. Lugha iliyotumika kwenye hii fedha 1.3 kwa yule Mbunge kwenye hii ya Corona haikuwa lugha nzuri. Fedha hizi tunatakiwa tutembee kifua mbele, tuzinadi na tuhakikishe wananchi wetu wanapata uelewa wa fedha hizi katika kutekeleza miradi na hizi fedha tuliomo humu wengine zinaweza zikatuokoa kurudi hata katika kipindi kijacho. Leo unawezaje kubeza hizi fedha, tena tunahitajiwa tuzisimamie kwa ukaribu ili zisichakachuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Trilioni 1.3 haijawahi kutokea. Fedha hizi za Corona binafsi na wananchi wa Jimbo la Manonga tunawapongeza sana, tunampongeza Mama lakini tunawapongeza Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri, Waziri wa TAMISEMI kwa uchambuzi mzuri na mgawanyo ulio sawa Majimbo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hizi zimetoka kwa wataalam walioajiriwa na Serikali katika kila Halmashauri, kwa hiyo kila Halmashauri imepata mgao, tunakwenda kujenga madarasa 12,000 nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi napongeza na pongezi hizi zinakwenda sambamba na ile project ya kwenye mpango wetu tumeona Mheshimiwa Waziri umewasikia Wabunge hapa kila mmoja akizungumzia na tumekuwa tunazungumzia juu ya kuboresha sekta ya kilimo. Sekta ya kilimo imepigiwa kelele miaka nenda miaka rudi na mpango wetu huu ni wa tatu, tumekuwa na mpango wa kwanza wa 2011/2012, umezungumzia kilimo. Mpango wa pili wa Taifa wa 2016 kuja 2021 umezungumzia kilimo, tumekuja na ppango wa tatu wa maendeleo wa Taifa unazungumzia kilimo lakini hatujaona bado hatujawekeza vya kutosha kwenye kumkomboa mkulima kutoka pale alipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa katika mpango huu tunaotaka kwenda kupitisha bajeti ya 2022/2023 ielekeze fedha kuwekeza kwenye kilimo. Tutenge fedha kama tunashindwa kuweka Trilioni Moja basi tuweke Bilioni 500 mpaka 700 kwenye sekta ya kilimo. Kama tunaweza wananchi mmoja mmoja akaweza kuchangia Pato ya Taifa mpaka asilimia 26 na Serikali haijawekeza vya kutosha. Je, tukiwekeza kwenye Bilioni 500 – 700 tutawezaje kupindua maendeleo ya wananchi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mataifa yote duniani, narudia kusema biashara ya utumwa ilikuwa ni kilimo, maendeleo ya viwanda ilikuwa ni kilimo, kule Brazil, Marekani ilikuwa ni kilimo. Tuwekeze kwenye kilimo, tuwekeze kwenye kutafuta masoko, pia tuweke fedha za ruzuku kusaidia mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mbolea ni shilingi 100,000 kwa mkulima. Bei ya mbolea inazidi kupanda na hatujawekeza mikakati ya kumsaidia mkulima katika kuhakikisha kwamba anapata mbolea kwa bei rahisi, kwa sababu tunategemea mvua ambazo zinaweza zikaja chache au pungufu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti inayokuja kupitia mipango yetu hii tunayoweka, lazima tuweke fedha ya ku- support mbolea, kuhakikisha kwamba tunaweka ruzuku kupunguza bei ya mbolea kutoka bei iliyopo sasa, kushuka chini hata shilingi 40,000 au shilingi 30,000. Tukifanya hivyo tutaongeza production katika nchi yetu. Pia tuhakikishe wakati tunafanya haya, tutafute masoko ya wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunalima kwa wasiwasi, bado tuna mazao ya kutosheleza na yamebaki kwenye maghala, na bado Serikali haijaonyesha njia ya kusukuma haya mazao yatoke: Je, tukienda kwenye kuwekeza zaidi, tutapata zaidi? Tumezungukwa na Mataifa ambayo wakati mwingine yana njaa; tumezungukwa na Sudan Kusini, tumezungukwa na nchi ya Kenya, tumezungukwa na nchi kama Burundi, Msumbiji na Zimbabwe. Tuna uwezo wa kupeleka mazao yetu kwenye Mataifa haya tukitengeneza miundombinu mizuri kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mpango wako uwekeze zaidi kwenye sekta ya kilimo, kama kweli tunahitaji kuleta mapinduzi katika Taifa letu. Tumeona mikakati mingi ilikuwepo, ni hatua nzuri sana kupata miundombinu ile, wanasema zana za uchimbaji wa mabwawa. Ni nzuri na tunapongeza sana Serikali. Itasaidia ujenzi wa mabwawa, lakini pia tukajenge sasa schemes za umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi jimboni kwetu pale Manonga, tuna maeneo mengi ya kujenga schemes za umwagiliaji. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, sasa muda hauko upande wako.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi uliyonipatia, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)