Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu wa mawazo kwa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2022/2023. Ni ukweli usiopingika kwamba suala la mafanikio ya Mpango wowote ule ni uhakika wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia mpango husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha Waziri ameonyesha kabisa kwamba Mpango huu utagharamiwa na vyanzo vingi ambavyo vimetajwa ikiwemo mapato ya ndani, mikopo, misaada na kadhalika. Sasa ni vema Serikali ikajipanga kuhakikisha mapato ya ndani au makusanyo ya ndani yanaimarishwa na ili tuondokane na mawazo ya kukopa kupitiliza, tafsiri yake ni nini? Ni kwamba kukopa hakukatazwi, ni kawaida, lakini tusikope kupitiliza mwisho wa siku mzigo unauelemea Serikali na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kwamba ni lazima tuweke mikakati ya kuimarisha mapato ya ndani kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi, kuhakikisha ulipaji wa kodi unafanyika kwa uhakika na kuondoa misamaha ya kodi isiyokuwa ya lazima. Kwa kufanya haya na mengine mengi, tutaenda kuimarisha makusanyo ya ndani na hatimaye haya ambayo yametajwa katika Mpango yatafanikiwa kutekelezwa kwa kutegemea kiwango kidogo cha mikopo, lakini kikubwa kitatokana na uhakika wa mapato yetu ya ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia ripoti ya CAG na tafiti mbalimbali zilizofanywa, hapa Tanzania tuna upotevu mkubwa wa mapato katika mambo tisa kwa uchache nikiyataja. Jambo la kwanza, kwenye sekta isiyo rasmi au wengine wanaita uchumi holela, tunapoteza takriban shilingi trilioni 2.8. Hoja ya pili, kukosekana kwa ufanisi kwenye Serikali za Mitaa katika ukusanyaji wa mapato, tunapoteza shilingi bilioni 50. Mamlaka za Umma kushindwa kutoa risiti za kielektroniki tunapoteza shilingi bilioni sita. Kama haitoshi, upungufu katika kufuata taratibu za kodi kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa na sekta za Umma, tunapoteza shilingi bilioni 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ya tano ni kutokulipwa kwa malimbikizo na madeni mbalimbali, inaifanya Serikali ipoteze shilingi bilioni 113. Hii ni kwa mujibu wa ripoti za CAG na research zilizofanywa Action Aid ambao wametumia takwimu mbalimbali ikiwemo NBS. Kama haitoshi, kuna rufani za kodi ambazo hazijaamuliwa. Kuna hizo ambazo ziko za Barrick na wengineo, lakini mbali na hiyo, kuna shilingi trilioni tatu ambayo tunaipoteza ambayo maamuzi yake hayajaamuliwa. Kama haitoshi, kuna marupurupu ya kodi yenye madhara ya shilingi bilioni 153 ambayo nayo hayakusanywi. Kama haitoshi kuna mzunguko wa fedha haramu au illicit financial flows, tunapoteza shilingi trilioni 2.7 na la tisa, ni mapungufu ya makusanyo ambapo tunapoteza shilingi trilioni 1.4. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa takwimu hizi na figure nilizozitaja, ni kwa hakika kama Serikali ingeweka mkazo katika maeneo haya na mengine mengi ambayo sijayataja, kwa hakika suala la kukopa ili kuhakikisha mipango yetu inatekelezwa, tusingeliona kama ni jambo kubwa au la muhimu sana. Ni kwa kufanya mipango madhubuti, mipango sahihi sera sahihi, sera rafiki mambo yote ambayo yatahakikisha makusanyo ya ndani yanafanyika ipasavyo na haya ambayo tumeyaweka kwenye mipango na ugharamiaji wa Mpango kwa ujumla wake, unafanikiwa kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanasemwa muda mrefu hapa Bungeni na sijui kwa nini Serikali inakuwa nzito kutekeleza au kuyasimamia baadhi ya mambo.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Halima.

T A A R I F A

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nampa Mheshimiwa Paresso taarifa tu kuwa hoja yake hiyo ya mapato na kutoa ushauri kwa Serikali kuweza kupata vyanzo vingine mbadala; kwa taarifa ya Wizara ya Fedha kwa mfano, inasema kwa mwaka 2020/2021 huu mwaka ambao ndiyo tunamalizia, Serikali imeweza kukusanya kwa vyanzo vyote yaani ukizungumzia TRA, ukizungumzia Halmashauri zetu, ukizungumzia makusanyo yasiyo na kodi, yote yaani lile kapu lote, ni shilingi trilioni 20 tu ambazo zinaweza zikafanya mambo basically matatu; kulipa deni la Taifa shilingi trillioni 10, kulipa mishahara shilingi trilioni nane na vipesa vile vi-OC vile Other Charges.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, anachokizungumza ni sahihi kwamba basically miradi yetu yote ya maendeleo pamoja na kununua yale madege tunanunua kwa pesa za mikopo. Kwa ushauri wako, inakupa taarifa ili u-boost pale ambapo unashauri, vyanzo vingine tunaweza tukapata wapi? Ni hilo tu. (Makofi)

MWENYEKITI: Ilikuwa ni taarifa Mheshimiwa Cecilia, unaipokea?

MHE. CECILIA D. PARESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naipokea taarifa hiyo. Naamini kabisa kwamba…

MWENYEKITI: Ngoja kidogo Mheshimiwa Cecilia, unapewa taarifa nyingine pia.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Nilitaka niwape taarifa kwamba ni utaratibu wa uendeshaji wa kiuchumi hata ngazi ya familia; unachukua kipato chako kile, unakifanyia simulation, unakichukua kwa mkupuo, halafu unatekeleza jambo kubwa; unaanza kurejesha kupitia jambo kubwa ulilotekeleza na jambo kubwa lile ambalo unakusanya. Kwa hiyo, siyo jambo la kwamba hakuna mapato ndiyo maana tunakopa. (Makofi)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kwa Waziri.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Cecilia ndiyo mchangiaji, endelea. (Kicheko)

MHE. CECILIA D. PARESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Taarifa yake siipokei. Ni hivi, yaani kukopa siyo dhambi na wala haikatazwi, lakini unakopa kwa ajili ya nini? Unakopa uende kufanya nini ili utakachokopa kirejeshe on time na ili uendelee kukopa na hicho utakachokifanya, matokeo yake yaonekane? Mbona ni kitu rahisi tu hiki na kinaeleweka tu. Mimi sio mchumi, lakini naielewa tu kwa namna hiyo, kwamba ni kitu ambacho kinaeleweka tu. Sasa… anyway, usinitoe kwenye hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi, mambo yote ambayo nimeyashauri hapa, ya kuimarisha makusanyo ya ndani na yawe endelevu, kudhibiti upotevu wa mapato, kuiwezesha TRA kwa maana ya rasilimali watu na vyote vinavyowezekana ili waweze kwenda kuhakikisha ukusanyaji wa kodi na mambo mengine yanafanyika, lakini pia kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara. Kwa sababu ukiweka mazingira rafiki, mwisho wa siku kodi inalipika bila kuwa na nguvu au kushurutishana, bila kuwa na hiyo kwamba nikupe risiti au nisikupe risiti. Haya yote yanafanyika kwa kuhakikisha kwamba huu udhaifu tuliouataja unaenda kuimarishwa ili tukuze ukusanyaji wa mapato ya ndani tuepukane na kukopa kunakopitiliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo napenda kuchangia kwa haraka haraka ni suala la deni la Taifa. Hapa tunapoongea, mpaka Septemba mwaka huu 2021, taarifa za BoT zinaonyesha kwamba kuna ongezeko la deni la Taifa ambapo mikopo kwa deni la Taifa la nje imefikia shilingi trilioni 59 na deni la ndani imefikia shilingi trilioni 18. Kwa hiyo, jumla yake inafanya deni la Taifa kufikia shilingi trilioni 78. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hali ambayo inatisha, ni lazima tuhakikishe tunakopa kwa vitu ambavyo kwa kweli ni lazima sana tukope na siyo vinginevyo. Kwa sababu tunakoelekea sasa hivi, hii mikopo yote ikiiva, maana yake makusanyo yote tutakayoyapata ya kwanza tunaanza kulipa madeni. Tutafika mahali hata mishahara tutashindwa kulipa kwa sababu madeni yameiva kila kona tulikokopa. Hii ni hatari sana kwa uhai wa nchi na wananchi kwa ujumla. Sasa Awamu ya Tatu iliacha deni la shilingi…

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

SPIKA: Taarifa, nakuruhusu mtoa taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Paresso kwamba usiwe na hofu na kukopa. Tunapanga kukopa ili kuwekeza na kutokana na kuwekeza tupate na matokeo yake. Unapozungumza miundombinu wezeshi na saidizi inaleta tija kwa maendeleo ya nchi. Wale wasiozijua ndege wanaweza kuzibeza, lakini sisi tunaosafiri na ndege, tunajua maslahi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu ya Ardhi inaandika paper kuja Serikalini, tunataka Serikali ikope shilingi trilioni mbili iweke kwenye sekta za kiuzalishaji, the productive sectors tuweze kuuza chakula dunia nzima na kufuga samaki na kuuza dunia nzima, ambapo soko la samaki ni dola bilioni 235. Tunataka tuingie kule. Kwa hiyo, kama fursa ipo, usiogope kukopa. Kampuni zote zinakopa na nchi zinakopa. (Makofi)

MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa Cecilia Paresso.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Taarifa yake siipokei na narudi kule kule na napenda anielewe vizuri na Serikali inielewe, kwamba kukopa siyo dhambi na haikatazwi, lakini unakopa ufanye nini ili kuwepo na mapokeo ambayo utaweza ku- service mkopo ule ili mambo mengine yasikwame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongelea habari ya Deni la Taifa na tena nafikiri mliite Deni la Taifa siyo la Serikali, kwa sababu kwenye vitabu humu wameandika Deni la Serikali, ni Deni la Taifa ili Watanzania wajue. Deni la Taifa leo tunapoongea ni shilingi trilioni 78, sijui ni bajeti za Wizara ngapi tulizonazo, sijui ni bajeti ya nchi yote kwa ujumla.

Sasa ninachoshauri ni kwamba, tuangalie tunakopa kwa ajili ya nini, kwa masharti yapi, kwa kufanyia nini na kwa matokeo yapi? Haya ni mambo ambayo tunayasema, tutashauri, na tutaendelea kushauri utekelezaji…(Makofi/ Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili, Ahsante sana.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji na kufanya maamuzi kwenye mambo haya siyo Biblia wala siyo Quran ni mambo ambayo yanabadilika kulingana na wakati na kulingana na uhitaji husika. Ahsante sana. (Makofi)