Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

Hon. Maryam Omar Said

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Pandani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwanza kwa kupata nafasi hii niweze kuchangia hoja zilizopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi moja kwa moja nitakwenda kwenye miradi ya maendeleo ambayo bado ni changamoto kubwa kwa miradi yetu kusuasua na kuchukua muda mrefu na kwa upande huo nitakwenda moja kwa moja kwenye miradi ya Muungano ambapo nitazungumzia Mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi uliopo Kaskazini A, Unguja.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mradi ulianza mwaka 2018 na tulitegemea mwaka 2022 mnamo mwezi wa saba tuwe tayari tumekamilisha mradi huu, lakini mpaka sasa huu ni mwezi wa pili tuna miezi mitatu tu mbele tuwe tumemamaliza. Mpaka sasa katika eneo lile kinachoonekana ni nyasi tu, hakuna chochote kinachoendelea, jambo ambalo ni changamoto kubwa, hivi Serikali hebu tujitathmini kwa nini tunakwama? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuseme labda ni wawekezaji wetu, kama hawana uwezo si lazima tumng’ng’anie mtu mmoja, wawekezaji ni bora tutangaze kwa tender kwa watu wengi, halafu tumuangalie ni nani mwenye uwezo kuweza kukiendesha kitu na kikafikia kwa wakati. Hatupati tija, tunawazuia wananchi maeneo kwa maelezo kuwa tunafanyia kitu fulani. Inafikia muda, muda unamalizika; mwananchi alikuwa akilima pale halimi tena anakaa nyumbani, anakufa njaa, hatumlipi mafao yoyote na bado tunakaa na lile eneo hatulitumii kwa kazi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani Serikali ni muda sasa wa kukaa chini tukatafakari tunapokwama na tukaendelea na miradi yetu jamani. Haya mambo ya kila siku miradi yetu kuwa wimbo wa Taifa humu ndani si sahihi. Wimbo wa Taifa ndio kila siku ni ule ule haubadiliki, mpango kila unapopita ukija miradi ni ile ile, mpango mwingine ukija miradi ni ileile, sio sawa, si haki hii, Serikali kaeni chini tutatue tujue kwamba, tukiendesha mradi hata kama ni mmoja sawa. Sekta tunamaliza muda wetu lakini tunajua kitu hiki kimefikia hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitoa mfano, Liganga na Mchuchuma ni mwaka wa ngapi? Toka enzi za mababu zetu, wamekuja wazazi wetu, tumekuja sisi, watakuja watoto wetu bado tunaonesha tu mlima uko pale, faida yake ni ipi kwetu sisi? Wote tuliowazuwia kwamba shughuli zote pale zisiendelee, tumemaanisha nini kama Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtatukosesha kura zetu tusirudi humu ndani, Mbunge akitoka huko anaahidi kwamba, ndani ya miaka yangu mitano nitahakikisha jambo hili limemalizika, tunamaliza miaka mitano hakuna chochote, tunarudi kwenda kusema nini kwa wananchi? (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tulifikirie hili, tusaidiane ifikie mahali tufanye jambo moja lionekane kwamba tumefanya hiki kuliko kwamba, kila mahali, kila mahali, tunaacha mapengo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye Kiwanda cha Viuadudu; nimesikia hapa taarifa ya Mwenyekiti, ameelezea kiwanda cha viuadudu, lengo kilipoanzishwa kile kiwanda; kilianzishwa kwa madhumuni ya kumaliza malaria nchini kwetu. Leo hapa kumeelezewa nchi takribani saba hizi zinachukua dawa kutoka kwenye kiwanda chetu hiki, lakini Tanzania bado, kitu ambacho kwa tathmini ya mwisho huku walisema kwamba zilinunuliwa lita 560,308 tena ziliponunuliwa hizo wameweka msisitizo ni kwa maelekezo ya Rais wa Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tujiangalie, malaria nchini kwetu bado ni tatizo tena ni tatizo sugu. Sisi kule Zanzibar tulikuwa na mradi wa kupigiwa dawa majumbani kila miezi mitatu, ikaja mpaka sehemu igundulike na malaria ndio inakuja kambi tunapigiwa dawa, ikafikia muda tukaambiwa mradi umeisha, sawa, malaria imerudi tena upya. Kama tukishirikiana hii ni nchi moja, kwa nini tusitumie rasilimali zetu zilizomo ndani na tukamaliza malaria? Hiki kiwanda kimeelekea kabisa madhumuni yake ni kumaliza malaria Tanzania, tunakwama wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ni zetu, pesa ni zilezile za Serikali, hivi kwa nini tusizoshawishi hizo Halmashauri kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakanunua hizi dawa na tukamaliza malaria nchini, lakini pia kiwanda kikawa kina- survive vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)