Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai siku ya leo tukakutana kwenye Bunge hili. Napenda kuunga mkono hoja ya Kamati kwa sababu nami ni Mjumbe wa Kamati hii ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu ni machache. La kwanza, hoja ya asilimia 10; ukiangalia karibia kila Mjumbe aliyesimama kuchangia ameiongelea. Ukiona watu wengi wanaongelea jambo moja, ujue aidha jambo hilo limefanyika vizuri ama jambo hilo limefanyika vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya asilimia 10, pamoja na lengo lake jema, hatuwezi kuisema vibaya moja kwa moja. Ina lengo jema na kuna baadhi ya watu wamefaidika na wanaendelea kufaidika; hilo tunalifahamu. Tatizo linakuja kwenye uendeshaji wake, kuna konakona nyingi sana. Kuna matatizo mengi sana hizi fedha, unapozungumzia mapato ya ndani maana yake ni kodi za wananchi. Serikali inakusanya kodi, inapata mapato, inatenga asilimia 10. Tunachotarajia ni kwamba zile fedha ziende zikatumike kweli kuwakwamua wananchi kiuchumi kama lengo au makusudi tuliyoyakusudia sisi Wabunge au Wawakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo inakuja tofauti; tunapokuwa kwenye Kamati tukihoji, tupate vikundi vingapi vimekopeshwa? Wamekopeshwa fedha kiasi gani? Wamerudisha fedha kiasi gani? Je, huu mfuko kila siku tutakuwa tunatoa tu fedha asilimia 10 hazirudi zikaenda kuzunguka? Zile za mwanzo ziko wapi? Hatupati majibu ya kueleweka. Unaambiwa mara kumbukumbu hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha zinatolewa benki, yaani ili mwanakikundi apate fedha, lazima wasajili. Sasa fedha imepitia benki, inakuwaje leo mtu anakwambia hakuna kumbukumbu? Kwa sababu, kumbukumbu ingekuwa ni fedha tu ambayo mtu anatoa mfukoni, haina maandishi, haina nini, tungeelewa. Maana yake kuna tatizo. Kwa hiyo, naiomba Serikali, tunajua hili jambo ni zuri, lakini uzuri huu unakwenda kutiwa dosari na watendaji ambao sio waaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongelea kwa mwaka, kwa mfano huu mwaka wa fedha 2021/2022 karibia shilingi bilioni 70, ambapo zingeingia kwa wananchi ipasavyo, tulitegemea tuone mabadiliko kwa wale wananchi wetu katika Halmashauri. Kuna Halmashauri, mfano zile za Jiji la Dar es Salaam, kawaangalie kwa mwaka mapato yao ya ndani asilimia 10 ni fedha kiasi gani? Hata hivyo, ukienda kuangalia ufanisi, haupo. Kwa sababu gani? Ni kama kijiwe, watu wamekaa kupiga fedha. Serikali inabidi iangalie suala hili kwa jicho la tatu. Fedha hizi ni nyingi, zingekwenda kubadilisha uchumi wa haya makundi ambayo tumeyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko yanaungua. Limeanza kuungua Soko la Kariakoo; tukakaa kidogo tukasikia Moshi soko limeungua; hatujatulia, Karume likaungua; hatujatulia Mbagala soko limeungua. Wakati soko la Kariakoo linaungua mpaka Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kipindi kile alikuwa Waziri wa TAMISEMI, alikwenda. Tukaambiwa imeundwa Tume, watatupa majibu. Naomba niwaulize Wabunge wenzangu, hivi ninyi wenzangu mlisikia majibu ya uchunguzi uliofanyika Soko la Kariakoo? Mimi binafsi sijasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kulisema hili ni nini? Unapofanyika uchunguzi, mimi nafikiri lengo; tujue kwa nini soko limeungua, ni sababu gani zimepelekea soko kuungua na kuna utaratibu gani wa kuzuia masoko mengine yasiungue? Kwa sababu, hizo fedha za asilimia 10 zinazochukuliwa mikopo nyingine zinaingia kwenye masoko humo; bidhaa/mali za watu zinaungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanakwenda kuchukua fedha benki wanakwenda kufanya biashara, mtu hawezi kurudisha kwani mali zake zimeungua. Maana yake kule nyumbani sisi tunasema ni sawa na unasuka ukambaa jikoni; huku unasuka, huku unaungua. Mwisho wa siku ukiinuka pale ukindu wako umeisha, hauna chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukisema hapa, haya masoko ndiyo wananchi wetu wanafanya biashara zao huko. Tuangalie namna ya kuyaweka katika hali ya usalama. Yanapoungua, wanaoathirika ni wengi. Hizo fedha za Halmashauri kwani leo mtu kama ulimpa asilimia 10, kama mtu leo alikopa benki halafu bidhaa zake zimeungua, analipa kutoka wapi wakati yeye alitegemea auze pale halafu akalipe? Wewe utamfanya nini? Kweli soko limeungua; kwani hata huyo wakimwongezea muda wa kulipa miaka mitano kama hana biashara, atalipa kutoka wapi? Kwa hiyo, suala hili la kuungua masoko liangaliwe kwa jicho la tatu; hii trend siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sitaki kuongea sana. Jambo langu lingine ni kuhusu Sekretarieti ya Ajira. Tungekuwa serious hii nchi sasa hivi ilibidi itangaze janga la wafanyakazi kwenye sekta ya afya na kwenye sekta ya elimu. Leo tunakaa hapa tunasema ufaulu kwenye hisabati asilimia 19, wakati kwenye sayansi huko nako hakueleweki, lakini Serikali inataka viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mtu anakwenda kuchanganya chemical kama hajasoma physics, hajasoma chemistry na kadhalika? Sasa Sekretarieti ya Ajira Mheshimiwa Jenista iko chini yako; tunafanya kazi na wewe vizuri tu, janga la walimu mashuleni, janga la watumishi wa afya; umejenga vituo, hakuna watoa huduma, yatageuka magofu. Kila kitu inabidi kiende kwa plan. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tunza Malapo ni janga ama ni upungufu wa hao watumishi?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa asilimia 19 ufaulu, utasemaje upungufu? To me, hilo ni janga tu, yaani hakuna namna ya kuisema. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, hiyo siyo tafsiri ya janga. Haya malizia.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwambia dada yangu Mheshimiwa Jenista, wakae wajipange. Tunataka tuone walimu na watumishi wa afya ili iendane na ile nguvu na jitihada za fedha za walipa kodi ambazo zimekwenda kujenga yale majengo ya vituo vya afya na madarasa, yatufae katika kuendeleza vizazi vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)