Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Najma Murtaza Giga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa ni lazima nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ananiwezesha kila jambo. Hata hivyo, pia sina budi kuushukuru Umoja wa Wazazi Tanzania kwa imani yao juu yangu kwa kunikubalia na kuniwezesha kuwa Mbunge ninayewawakilisha kupitia Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile sina budi kukushukuru wewe pamoja na Wabunge wote kwa imani yenu juu yangu ya kunikubalia kuwa miongoni mwa Wenyeviti wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee kabisa lazima nizipeleke kwenye uongozi mpya wa Awamu hii ya Tano unaoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli dhamira yao njema imeshaanza kuonekana, kwa hiyo tuwaombee tu Mwenyezi Mungu azidi kuwaendeleza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia sina budi kabisa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Ummy pamoja na msaidizi wake, Naibu Mheshimiwa Kigwangalla kwa kazi nzuri waliyoanza nayo. Sina haja ya kuwalaumu kabisa, ni lazima niwapongeze. Changamoto ndiyo sehemu ya maisha na kazi yetu ni kuwashauri.
niongelee kwenye suala zima la ukatili wa kijinsia ambalo Mheshimiwa ameainisha humu katika kiambatanisho namba 10.
Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumza hapa kuhusiana na suala hilo kwa maoni tofauti, lakini naomba nielekeze moja kwa moja kwenye ushauri kwenye mambo sita tofauti ambayo ameainisha.
Suala la kwanza ni ukatili wa kingono. Hilo limezungumzwa, lakini nasema, pamoja na elimu ambayo itatolewa ambayo wamejipangia katika Wizara hii lakini ushirikiano wa karibu kabisa ni lazima kwa vitengo vya sheria. Mwanasheria Mkuu atanielewa nikisema zaidi kwamba ushahidi katika suala hili la hao wahalifu ni mgumu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bila ushirikiano wa karibu na vitengo vya sheria na kuhakikisha kwamba tunapunguza masharti ya sheria za ushahidi ili tuwadhibiti hao wenye vitendo vinavyofanya mporomoko wa maadili katika nchi yetu na kusababisha idadi inayoripotiwa kwa mwaka 2015 kufika 6,722 ambapo naamini kabisa idadi hii ni ya wale walioripotiwa tu, lakini kuna wengine huku ambao hawakuripotiwa wapo wanaathirika na janga hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukaribu baina ya Wizara pamoja na Wizara nyingine, ukajenga mnyororo madhubuti, tutaweza. Naamini kabisa mkituletea hapa Wabunge tujaribu kurekebisha hizi sheria za ushahidi wa jambo hili, basi hawa watakamatwa na watadhibitiwa na hivi vitendo vitapungua, vinginevyo tutaongeza vitendo hivi jamani. Kwa sababu hata Mwenyezi Mungu kwenye kitabu chake kitukufu cha Qurani amesema tusikaribie zinaa, hakusema tusifanye, amesema, tusikaribie kwa maana, tusipokaribia hatutofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ikiwa tutawadhibiti hawa kwa ushahidi mwepesi wakapatikana, wataacha na wao watakoma na Taifa letu litanusurika na janga la huu ukatili wa ngono kwa akinamama na watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakuja suala la pili, utupaji wa watoto na wizi wa watoto, vitu viwili sambamba. Kuna watu wanahitaji watoto hawana, wanaiba. Kuna watu wanapata watoto wanatupa na wanakufa. Kwa hiyo, nashauri kwa Wizara hii hebu tujaribu, kama Wizara itakuwa ni vigumu labda kifedha, basi hebu tutoe uhamasishaji kwa wananchi waweze kujitolea kujenga vituo vya kulelea yatima ili wale akinamama ambao wanaona watoto wale hawawahitaji, wawapeleke wakalelewe kule na wale wezi waache kuiba wakachukue kule. Kwa hiyo, huo ni ushauri ambao pengine Serikali inaweza ikashindwa lakini wadau wengine watakubali. Kwa hiyo, naomba sana hilo tulifanye.
Mheshimiwa Spika, katika hilo hilo kuna suala la utoaji mimba. Hili naomba pia Wizara ilishughulikie, baadhi ya mimba zinazotolewa wanashirikiana na wakunga na manesi. Kwa hiyo, sasa hawa manesi wenye tabia hizi wadhibitiwe kwa sababu ni watu wachache wenye ujasiri wa kutoa mimba wenyewe, lazima wasaidiwe na wanaoelewa wanakuwa ni wakunga ama manesi. Kwa hiyo, sasa Wizara hii inabidi katika upande wake, katika sera zake na mambo yake, ihakikishe kwamba hao wanaofanya vitendo hivi wanadhibitiwa ipasavyo na kuadhibiwa ili kuondoa tatizo la utoaji mimba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiondokana na hayo nakuja kwenye mauaji ya vikongwe. Ni kweli inawezekana hawa vikongwe wanatuhumiwa, inawezekana ni kweli lakini kwa nini tuchukue sheria mkononi? Kwa nini, hakuna Serikali za vijiji? Hakuna uongozi wa vijiji? Kwa nini tusiende tukatoa taarifa kule. Kwa hiyo Wizara hii naomba sana kwa kushirikiana na vitengo vya sheria, narudia tena tudhibiti jambo hili kwa kuhakikisha tunatoa elimu tosha ya kuelekeza wananchi wetu vijijini ili waende wakatoe taarifa wanapoona kwamba kuna wazee wanahatarisha jamii yetu, basi waende wakashughulikiwe kisheria kuliko kuchukua hatua au sheria mkononi ya kwenda kuwaua wazee wetu, inawezekana wengine si kweli. Kwa hiyo, naomba sana hilo nalo tulifuatilie kwa uzuri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija suala la nne, mashambulio ya kudhuru na lugha za matusi. Hii zamani ilikuwa haipo kabisa jamani. Utamaduni wetu sasa unaporomoka, ni tatizo kubwa. Naomba sana niwashauri Wabunge wenzangu humu ndani, tuanze sisi na lugha nzuri. Sioni sababu ya kutoa lugha ya matusi wakati tunaambiwa maneno mazuri humtoa nyoka pangoni. Kwa hiyo, sasa wale wanaotusikia nje au wakihadithiwa nje kwamba Wabunge ndani wanazungumza lugha mbovu, tutakuwa hatuna mfano mzuri kwa wananchi wetu. Haya matendo yanazidi, idadi yake ni kubwa mno hapa tunaambiwa 14,561 mashambulio ya kudhuru pamoja na lugha za matusi. Kwa hiyo, naomba sana sisi Wabunge tuwe mfano ili image yetu iwe reflected nje, watu waweze kuwa na adabu nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la tano ni utelekezaji wa familia. Naunga mkono kweli elimu ni ndogo, pengine vijana wetu wengi hawajui nini maana ya familia, lakini bado narudi tena pamoja na kutoa elimu kuna akinababa wengine wazima zaidi ya miaka 40, anatelekeza familia yake anakwenda kutafuta mwanamke mwingine. Hili ni baya sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri kabisa hii Wizara inayohusiana na jinsia jamani Mheshimiwa Ummy, hawa akinababa wenye tabia hizi na wana uwezo wao wengine wanafanya kazi na wana uwezo tuwadhibiti, tukiwajua wakatwe baadhi ya mshahara wao ama vipato vyao viende kwenye familia zile.
Mheshimiwa Spika, pia sisi akinamama nao wake wa pili, nyumba za pili, tusiwe na roho mbovu, tusidhibiti kila kitu. Tuwaachie akinababa wawashughulikie na akinamama wenzetu wengine na familia zao. Hili ni jambo zuri sana, naomba jamani kwa heshima kubwa sana hili tulifikirie na tulizingatie, litaondosha kabisa tatizo hili jamani.
SPIKA: Mheshimiwa Najma, sijakusikia vizuri. (Kicheko)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, nasema kwamba kuna tabia ya akinababa hawa ambao ni watu wazima zaidi ya miaka 40, wanaacha familia zao za kwanza, yaani nyumba ya kwanza wanatafuta nyumba nyingine, ile wanaitelekeza. Kwa hiyo, hili ni jambo baya. Hawa wadhibitiwe na kama wanafanya kazi wana uwezo basi kile kinachopatikana wagawiwe familia ya kwanza.
Pia na akinamama hawa wa nyumba za pili, tuwe na huruma kwa akinamama wenzetu wa nyumba za kwanza. Nafikiri hili limeeleweka vizuri na naamini kabisa utelekezaji huu utapungua, tukifanya hivyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, namalizia kuhusu mimba za wanafunzi. Mimba za wanafunzi zinaweza kuleta madhara kwa wasichana wetu na kuwayumbisha kimaisha jamani! Hapa tunaambiwa idadi ya ripoti ni 412 lakini naamini ziko nyingine ambazo hazijaripotiwa. Kwa hiyo, hili suala nalo tulidhibiti vizuri kwa kushirikiana tena na vitengo vya sheria. Ikiwa ni mtu mzima amempa mimba mwanafunzi, basi huyu asiachiwe, adhabu iwe kali. Vilevile ikiwa ni mwanafunzi na mwanafunzi waadhibiwe wote wawili ikiwezekana, kwa sababu wengine wakome. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yangu kwa kweli yalikuwa ni hayo. Nakushukuru sana kwa muda huu. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Najma….
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja wala sina haja ya kupinga.