Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii tena ili kuweza kujumuisha yale yote ambayo yamechangiwa na Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati yetu tumepata wachangiaji 13. Kwa haraka haraka naomba niwataje, Mheshimiwa Londo, Mheshimiwa Shangazi, Mheshimiwa Sanga, Mheshimiwa Migilla, Mheshimiwa Jacqueline, Mheshimiwa Mwakamo, Mheshimiwa Tunza, Mheshimiwa Saasisha, Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, Mheshimiwa Kanyasu, Mheshimiwa Dkt. Alice na Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Wabunge wote waliochangia katika Kamati hii, michango yao inaendelea kutuimarisha sisi kama Kamati ili kuweza kuisimamia na kuishauri Serikali katika mambo kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michango yote yapo mambo muhimu ambayo Waheshimiwa Wabunge waliyagusia na walitoa msisitizo na sisi kama Kamati tunaendelea kutoa msisitizo kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zile za asilimia 10 endapo Serikali itazisimamia vizuri zitaweza kuondoa umaskini katika nchi yetu. Ukifuatilia takwimu, zaidi ya bilioni 70 zinatolewa kila mwaka kwa kuwakopesha vijana, kina mama na watu wenye ulemavu. Fedha hizi zikitungiwa sheria na kanuni madhubuti pamoja na mifumo thabiti ya kudhibiti vikundi visiweze kukopa kiholela, vikundi viweze kurudisha, nina hakika fedha hizi zitamkomboa Mtanzania kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge pia walizungumzia sana kuhusu fedha za maendeleo. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri wangu hapa, ameelezea namna ambavyo atatuletea kwenye Kamati. Kiukweli kama Kamati tumeona ipo haja ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ziende zikatekeleze miradi ya maendeleo. Takwimu zinaonesha kwamba bado kuna upungufu mkubwa wa madarasa kwa wanafunzi ambao watamaliza darasa la saba mwaka huu. Sasa fedha zile tutakapoamua kuzibadilishia matumizi, tukazipeleka kwenye matumizi mengine ambayo si ya miundombinu ya elimu na wala si ya miundombinu ya afya; tatizo hili tutaendelea kuwa nalo. Hivyo basi, kama Kamati tunaendelea kusisitiza kwamba, fedha hizi ziendelee kutumika katika miradi ya maendeleo hasa miundombinu ya elimu na miundombinu ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamezungumzia sana suala la Walimu wastaafu, Walimu waliofariki na kada nyingine mbalimbali zilizostaafu na kufariki. Kamati tutaendelea kusisitiza, nafasi hizi za watu ambao wamestaafu na kufariki ziweze kujazwa mara moja. Kwa maana nafasi hizi zikijazwa tunaendelea kuondoa upungufu mkubwa wa Walimu na kada mbalimbali ambazo zinatokana na mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa sana suala la majanga ya moto. Tumeona, majanga ya moto yamekuwa kizungumkuti sana nchini kwetu, hasa katika maeneo ya masoko. Kamati itaendelea kusimamia na kuishauri Serikali namna bora ya kufanya ili majanga haya ya moto yasiendelee kutokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuatilia majanga haya ya moto utaona kila mahali ambapo moto umetokea tunaambiwa chanzo ni umeme. Tunajiuliza, je umeme huu unatoa hitilafu usiku tu na mchana unakuwa haupo? Sasa, ni moja ya majukumu ya Kamati hii kuona ni namna gani tutaendelea kufuatilia na kuikomesha hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala la mifumo mbalimbali, hivyo basi Mamlaka yetu ya Serikali Mtandao (eGA) tutaendelea kuisimamia na kuhakikisha maeneo yote ambayo mitandao ya kielektroniki inatakiwa iwekwe, basi eGA ishiriki katika kuweka mitandao hiyo ili kuepusha mitandao isiendelee kutosomana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu ina mambo mengi na kwa sababu ya muda, naomba sasa Bunge lako lipokee taarifa hii na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati hii ili iweze kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.