Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia sekta hii muhimu sana. Kwanza kabisa kwa moyo wa dhati nichukue fursa hii kumpongeza Waziri, dada yangu Ummy Mwalimu kwa uteuzi wako. Tunaamini mwanamke akipewa nafasi hasa katika sekta ya afya ambayo ina changamoto kubwa sana zinazowagusa wanawake, sisi tunakuombea ili uingie katika historia ya kuondoa matatizo ya wanawake. Pia nichukue fursa hiyo kumpongeza kijana mwenzangu kwa uteuzi Dkt. Kigwangalla, naamini usipofuata siasa, ukifanya kazi kwa profession yako ya Udaktari utasaidia sana kuboresha sekta ya afya katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, niwapongeze Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushiriki zoezi la kutoa damu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuwasaidia watoto waliokuwa wamekosa damu wakati wa kufanyiwa upasuaji wa moyo ili waweze kufanya hivyo. Tunaamini bila kujali itikadi zetu, tukifanya hivyo tutasaidia sana kuchangia kwenye benki ya damu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ningependa unipe ufafanuzi kwa nini fedha za methadone zinapitia MDH (Management and Development for Health)? Nauliza hivyo kwa sababu mwanzo zilikuwa zikienda Tume na ilikuwa rahisi sana kufika katika hivi vitengo ambavyo wanatoa hizi dawa kwa ajili ya kuwasaidia wale walioathirika na dawa za kulevya. Sasa hivi imeenda MDH na nafikiri ni mlolongo mkubwa sana kuliko ilivyokuwa mwanzo.
Mheshimiwa Spika, pia hivi sasa hawa watu wa drugs wana mkakati maalum ambao nchini Italia watu wanaouza dawa za kulevya waliutumia. Baada ya kuona kwenye mianya mbalimbali wameanza kuziba na nichukue fursa hii kuwapongeza Kitengo cha Usalama wa Taifa wanaoshughulikia dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuziba hiyo mianya, sasa hivi wana mkakati wa kwenda kuuza dawa za kulevya katika hivi vitengo vya kutoa dawa za kuwarudisha wale vijana. Sasa tunataka kujua kama mnajua mna mkakati gani wa kudhibiti ili hii methadone iwasaidie vijana siyo wanatoka kunywa dawa wanarudi katika chemba za kuwarudisha tena katika kutumia dawa za kulevya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kitengo cha magonjwa ya watu wenye matatizo ya akili pale Muhimbili, hakuna wodi ya watoto wa matatizo ya akili, wanakwenda kuchanganywa kwa wagonjwa wengine, moja wanaweza wakaumiza wenzao au wao wakaumizwa, kwa hiyo, ni changamoto kubwa sana hakuna wodi ya watoto.
Mheshimiwa Spika, kingine hata katika hiyo wodi ya watu wazima tunajua watu wenye matatizo ya akili, ambao wanakwenda hawajawahi kutumia dawa, wako active zaidi kuliko wale ambao wameshaanza kutumia dawa.
Serikali ina mkakati gani wa kuongeza wodi na kuwagawa, wale walioanza kutumia dawa, wanaoanza kupona wanakuwa kwenye wodi zingine na hawa ambao bado hawajaanza kutumia dawa wawe kwenye wodi zao ili tuepushe madhara ya kuumizana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ukipitia taarifa ya CAG, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), mwaka jana kuna mzigo wa shilingi bilioni 4.6 umeingia bila kukaguliwa, hapo ndiyo zinaingia cerelac fake, zinaingia S26 fake, maziwa ya kopo, zinaingia sorry pads fake, zinaingia pampers fake, zinaingia juisi fake na kadhalika. Mwisho wa siku tunawaona kwenye TV wanakwenda kusema tumekagua vitu fake vilivyoingia, je, ni jitihada gani ambazo zimefanywa kudhibiti kwanza visiingie kabla ya kusubiri vinafika dukani na kuleta madhara kwa watoto na kuleta madhara kwa Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nililotaka kulizungumzia hapa kuhusiana na hospitali yetu ya Ocean Road, nakumbuka mwaka jana nilileta hoja binafsi na Mheshimiwa Waziri aliyekuwa Naibu Waziri Dkt. Kebwe alijibu yafuatayo; “tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua mashine.”
Mheshimiwa Spika, leo napongeza taarifa ya Kamati imeeleza ni uzembe umefanywa na Serikali, ile mashine haijaja, mbali na kutambua jitihada ya kujenga maeneo ambayo zitakaa zile mashine. Mheshimiwa Waziri mashine zilizokuwepo, zile mbili ni mbovu, zinafanya kazi kupita uwezo wake. Kwa siku zinahudumia wagonjwa zaidi ya 300 na tunajua ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi unavyomsumbua mwanamke na tunajua matibabu ya kansa yalivyo ya gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Ocean Road waliomba Bohari ya Dawa, dawa tofauti tofauti 53 wamepata 17 tu, sawa na asilimia 35. Tunaomba kuwe na mkakati maalum wa kuhakikisha fedha zinazokwenda Ocean Road ziwe ring fenced ziende zote, pamoja na dawa zinapotengewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine tuwe na mkakati sasa wa kutanua wigo wa matibabu katika kanda zetu ili ile Ocean Road isielemewe. Hata katika takwimu ukiangalia wengi wanaopata hayo magonjwa ni watu maskini wanaotoka kwetu kule Manyamanyama na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuchangia, nimelizungumzia sana nikiwa Mbunge wa Viti Maalum kuhusiana na kupandishwa hadhi Kituo cha Afya cha Manyamanyama kuwa Hospitali ya Wilaya. Hili ni jambo la muda mrefu, tunajua kuna changamoto ya kukosa chumba cha kuhifadhi maiti, lakini kama unavyojua Halmashauri yetu bado changa, tunaomba Wizara mtusaidie na uingie katika kumbukumbu. Hili ombi tangu enzi za Mama Anna Abdallah na wengine, naamini kwako wewe ni jambo dogo halitakushinda. Tunaomba utusaidie wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini, akinamama wasihangaike sana iwe Hospitali ya Wilaya kwa sababu inahudumia hata Wilaya ya jirani pamoja na mikoa mingine.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine natambua umuhimu wa Mfuko wa Afya, ni kuboresha sekta ya afya na kuboresha vituo vya afya na natambua kuna ufadhili wa DANIDA pamoja na fedha za Serikali, kuna Halmashauri 23 hazifanyi vizuri, natambua zingine zilizokaguliwa kati ya 160, 138 zinafanya vizuri. Hizi 23 kutofanya vizuri na kufuata masharti zimesababisha hasara ya bilioni moja na milioni mia moja tisini na tisa.
Mheshimiwa Spika, hizi fedha zingeweza kujenga vituo vya afya vingine, hizi fedha zingeboresha katika sekta ya afya hasa kule vijijini ambako tunatoka sisi. Mfano Halmashauri moja tu, kwenye taarifa yake imesema imetumia milioni 55 kwenda kununua dawa na vifaa tiba, lakini katika ripoti ya CAG alivyofanya ukaguzi, wametumia milioni 31, milioni 20 ni wizi mtupu. Sasa tunaomba kuwe na ukaguzi wa mara kwa mara na uangalizi kuhakikisha hizi fedha zinatumika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tunajua kuna upungufu katika Mfuko wa Afya wa wafanyakazi 32,000 katika Halmashauri zetu na hawa wafanyakazi ni pamoja na wataalam, kule Mheshimiwa Kigwangalla ambako hakuna hata mlango wa kwenda kumfungia mfanyakazi wala mfanyakazi wa kumfungia, kule ndiko tunatakiwa tupeleke wataalam, tuepushe vifo vya akinamama wajawazito, tuepushe matatizo ambayo yanawakumba wananchi wetu wa vijijini. Huu Mfuko ni mzuri, nia njema lakini lazima tufuatilie mara kwa mara, fedha zinazotengwa zitumike kwa malengo husika, ili tuweze kutatua changamoto za afya katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na nipongeze hotuba ya Kambi ya Upinzani na pia nikupongeze kwa kusoma vizuri hotuba yako, lakini changamoto kubwa dada yangu uliyonayo, hicho ulichokisoma upate fedha na ziende katika utekelezaji. Ahsante sana.