Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na naomba niwatambue kama ifuatavyo; Mheshimiwa Subira Mgalu, Mheshimiwa Mtemvu, Mheshimiwa Halima Mdee na Mheshimiwa Kakunda. Naamini kabisa kungekuwa na muda wa kutosha Waheshimiwa Wabunge wengi walikuwa na haja ya kuchagia mpango huu mzuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba kama kuna siku ambayo nimewahi kusimama hapa kwenye Bunge lako tukufu, siku ambayo ni nyepesi kuweza kujibu hoja za Wabunge, hakuna siku ambayo imekuwa nyepesi kwangu kama leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge takribani wote waliosimama na ukiangalia ambao hawajasimama jisnia ambavyo walikuwa wanagonga meza, basi inadhihirisha kwamba wale wachache waliosimama wamewakilisha mawazo ya wengi ambao hawajachangia, kwamba wana pongezi za dhati sana kwa kazi nzuri na ubunifu wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengi ambayo yamezungumzwa na kama Serikali tutayachukua ili tuweze kuyaendeleza ikiwa ni jitihada njema ambazo zimeanzishwa na Serikali hii ya Awamu ya Sita. Lakini kubwa zaidi, nimefarijika kuona Wabunge wengi na nyuso za furaha kwa sababu leo hii Wabunge hawa wanatembea vifua mbele majimboni kwao kutokana na miradi ambayo inaendelea ya sekta mbalimbali ambayo imetokana na fedha hizi za UVIKO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wako ambao waliwahi kusema kwamba haya yanayoendelea sasa hivi hayajawahi kutokea tangu nchi yetu imepata uhuru na tokea Mapinduzi ya Zanzibar na tangu Muungano wetu uliounganisha nchi hizi mbili. Kwa hiyo ni jambo ambalo linatupa faraja kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mawazo mengine ambayo yametolewa, ikiwemo umuhimu wa kuendeleza utaratibu huu wa uwazi na ushirikishwaji wa Bunge wa iwango cha juu, basi kama Serikali tumelipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo mengi yalikuwa ni pongezi; wako waliozungumza kwamba katika utaratibu wa kawaida nchi yetu sasa ni nchi ambayo ipo katika uchumi wa kati, hivyo basi kupata mkopo usiokuwa na riba ukifikia status hiyo ni jambo gumu. Lakini kwa jitihada za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweza kufanikisha mkopo huu tukaweza kuupata kwa riba zero kutoka riba ya asilimia 1.05 ya kiwango cha asilimia 66.6 ya mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, nimeshangaa sana leo Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa aliyezungumza, nadhani ni mawazo ambayo niliona kidogo yanahitaji kutolewa ufafanuzi pengine ilikuwa ni ambayo alizungumza Mheshimiwa Halima Mdee, kwamba leo anahoji kuhusiana na utaratibu wa mkopo huu.

Mheshimiwa Spika, hivi mkopo kama huu unawezaje kuhoji? Mkopo wenye neema kama hizi. Kama nitakuwa nimemuelewa sawasawa, lakini naamini kabisa na yeye anaunga mkono, lakini labda kama aliteleza kidogo ulimu basi nadhani nataka niliweke sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkopo huu ni mkopo wa bei nafuu na maisha yote kama nchi tunajaribu kukopa mikopo ambayo itakuwa nafuu ili kupunguza mzigo wa kulipa madeni kwa ajili ya mikopo kila mwezi. Pale ambapo yanapatikana mapato ya Serikali, fedha ambayo itatengwa kwa ajili ya matumizi itakapomalizika na fedha ambayo itatengwa kwa ajili ya kulipa madeni itakuwa imemalizika maana yake fedha ambayo itabakia itakuwa ni chache. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapokuwa na mkopo ambao una muda mrefu wa kulipa kama huu maana yake unatoa nafuu ya kuweza kupata fedha za kuweza kutekeleza miradi mingi zaidi kwa sababu unapunguza matumizi. Lakini unapokuwa kwenye mkopo wenye riba zero kama huu maana yake una uwezo wa kulipa kidogo kwa sababu riba ni nafuu ama haipo kabisa. Kwa hiyo, niliona hili niliweke sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa ujumla Waheshimiwa Wabunge wamepongeza na zaidi ya pongezi sisi tunafarijika sana kwa jinsi ambavyo Bunge hili Tukufu limeweza kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais wetu za kuweza kuhakikisha kwamba mikopo kama hii tunaweza kuichangamkia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa zaidi ni jinsi ambavyo tumeweza kutumia mkopo huu kwa utaratibu ambao ni kinyume na nchi nyingi, kama Kamati ilivyosema kwamba nchi nyingi zaidi ya 40 ambazo zimeweza kupata mkopo huu hawakuweza kutumia kwa jinsi ambavyo sisi tumetumia kwa miradi ambayo ni ya kudumu na ya muda mrefu. Kwa hiyo niseme kwa ujumla kwamba yaliyochangiwa kwa ujumla ni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.