Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Lema Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, kwa kutoa ndani ya roho yake na ndani ya nafsi yake maudhui aliyekuwa ameyatayarisha kwa ajili ya kuwakilisha kambi. Nizungumze suala moja, mimi binafsi sitaki kuunga hoja na napinga kwa nguvu zangu zote mafungu ambayo yameelekezwa kwa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa sababu ya Jeshi la Polisi kutumiwa vibaya wakati wa kipindi cha uchaguzi. Wakati wa uchaguzi Jeshi la Polisi kasoro tu hawavai nguo za green wanavaa kombati za polisi lakini asilimia 100 wanakuwa wametayarishwa kusaidia Chama cha Mapinduzi kushinda uchaguzi, huo ndio ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hiyo kwa mifano hai. Mwaka 2005 nikiwa nagombea pale Bukoba Mjini, Jeshi la Polisi lilitumika kunizuia kukusanya matokeo chini ya mtutu wa bunduki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 Jeshi la Polisi limetumika kusimamia uharamia na kubaka demokrasia ya watu kupiga kura kadri wanavyotaka. Nachukua mfano hai wa kwangu, nimewapa taarifa polisi kwamba Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi amebaka uchaguzi kwa kunyofoa karatasi ndani ya vitabu vya kupigia kura na anazisambaza kwa ajili ya kuhakikisha yule mpinzani wangu anashinda na pia wagombea wa CCM wanashinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini polisi wakakataa kufuatilia suala, lakini vijana makamanda walikuwa wamejipanga tukazifuma hizo kura zilivyokuwa zimepangwa. Nashukuru vituo vya ITV vilifanya kazi nzuri lakini hata mimi na makamanda tuliweza kuzizingira kura zaidi ya 2000 zikiwa zimetayarishwa kwa ajili ya kuwekwa kwenye masanduku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu kubwa ya kura hizo niliziwasilisha mpaka kwa msimamizi wa uchaguzi. Nilitoa taarifa kwa makamanda wa Jeshi la Polisi wote wakazikimbia, lakini msimamizi wa uchaguzi nilihakikisha kwamba nampelekea sehemu ya kura hizo na nikaandika waraka kwenda mpaka Tume. Mpaka leo ninapozungumza Tume haijawahi kuchukua hatua yoyote na hiyo imeonesha jinsi gani wenzetu wa upande wa pili wanashinda uchaguzi, wananyofoa kura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wasimamizi wa uchaguzi wanakuwa ndiyo marefa, lakini kumbe ni wachezaji pia. Polisi inajifanya kusimamia lakini na wenyewe wanaongeza namba, wanacheza namba mpaka wachezaji 16 upande mmoja. Kwa kuthibitisha hilo, sehemu ya kura ambazo sikuzikabidhi ni hizi hapa, wasiwe wanatambatamba kwamba, wanashinda uchaguzi wakati kura bandia zipo tuliziteka, hizi hapa zimepigwa tick, mgombea CCM wa Urais na Makamu wake mkizihitaji nitapeleka mezani njoo mchukue. (Makofi/Vigelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hapa nyingine namuuliza Mkurugenzi, hizi zimetokaje katika mfumo wake? Anakimbia, anakimbia hana maelezo. Kwa hiyo, makamanda ninachowaambia kwa jeshi tulilonalo ,kwa chama tawala tulichonacho wameshazoea vya kunyonga, vya kuchinja hawaviwezi, tutapiga kelele hapa, tutaimbiana ngonjera hawa watu sikio la kufa halisikii dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwaeleza ukweli lililopo makamanda ni kujipanga upya kukabiliana na ngoma inayokuja mwaka 2020. Watakuja vingine hawa kwa wizi wa style nyingine, wanasema wana-style 86. Kwa hiyo, ninachowaomba makamanda hapa ni kutwanga maji kwenye kinu, hawa watu wameshazoea vya kunyonga, vya kuchinja hawaviwezi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona wakati wa uchaguzi, tulikuwa na vituo vyetu vya kuweza ku-tally matokeo katika maeneo mbalimbali, chama kilikuwa kimeandaa vijana wa IT wa kuweza kusema matokeo CCM wakiwa Milimani City na sisi vijana wetu wakiwa katika maeneo mengine, vituo tulivyokuwa tumeviandaa, lakini Jeshi la Polisi limetumika kuwavamia vijana wetu katika maeneo walipokuwa wana-tally kura za uchaguzi, lakini CCM wakaachwa bwelele wakafanya jinsi wanavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu nafikiri huko mbele tunapoelekea hili Jeshi la Polisi ukweli wenyewe tunapopitisha mafungu hapa tunakwenda kuongeza nguvu kuwaelekeza na kupata mafunzo namna ya kubaka demokrasia ya kweli. Hiyo siko tayari kuacha pesa ziende kufanya haramu, Jeshi la Polisi tulilonalo ndugu yangu Kitwanga namfahamu vizuri sana, tena bahati nzuri nilimwona na Shekhe Yahya Simba hawa walikuwa inside brothers kwenye club moja tukiwa Chuo Kikuu, walikuwa vijana safi, wametulia, wenye maadili, naomba maadili hayo basi hebu ajaribu kurekebisha na kunyoosha Jeshi la Polisi, tuwe na jeshi ambalo linajiita polisi jamii lisiwe polisi...?
Polisi CCM. Tunaomba, tunaomba suala hili kama jeshi haliwezi kujirekebisha ni vyema tuanze kujenga hoja, tuanze kukusanya sahihi za Watanzania na tuombe ulimwengu, tuombe Taasisi za Kimataifa zije kusimamia uchaguzi mwaka 2020 badala ya jeshi la namna hii ambalo limebeba sura na taswira ya kubaka demokrasia ni hilo siwezi kukubaliana nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho ambalo nataka kuzungumza ni suala la kubambikiana kesi. Makamanda, sisi wengine tunatembea kama wafungwa watarajiwa, kwa sababu ya Jeshi la Polisi kubambikiza kesi, lakini hata hivyo nawashukuru wengine tumejengewa historia ya kusindikizwa na ving’ora kama Rais jambo ambalo hatukulitarajia. Tumejenga dhana, lakini nataka kuomba Jeshi la Polisi lijerekebishe vinginevyo msiufikishe umma, msiwafikishe Watanzania wakaanza kuwa na fikra za kuona wanajipangaje katika majeshi yasiyokuwa rasmi kwa ajili ya kulinda haki yao ya kura wanazozipiga. Hilo litafanyika watalifanya kwa kulazimishwa na hali ya mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze vijana wa Bukoba wakati namaliza, pamoja na mbinu zote hizo zilizokuwa zimepangwa kuleta Mbunge wa kuchonga lakini vijana walikaba mpaka penalty, vijana wa Bukoba walikaba mpaka penalty na wala hizo dhuluma, hazikuweza kupenya. Makamanda na Watanzania wote nawapa rai, hawa jamaa ni wepesi, ni wepesi kuliko nyama ya utumbo, kama unajipanga hawa jamaa ni wepesi kwelikweli, lakini nawaomba na nyie polisi basi, polisi Mheshimiwa Rais aliwahi kusema kwamba, ukielezwa na wewe changanya...?
Na za kwako, hebu msitumike, msitumike kwa sababu hawa jamaa huko tunakokwenda naamini ICC inakwenda kufanya kazi The Hague, angalia na wewe usiwe miongoni mwa list ambayo itapelekwa The Hague.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.