Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami kwanza nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Temeke kwa kuniamini na kunipa fursa ya kuwatumikia. Nawaahidi tu wasiwe na wasiwasi, nitawatumikia kukidhi mahitaji yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeipitia hii hotuba ya Mheshimiwa Rais na yako mambo ameyataja, lakini vizuri tungependa tuyaongezee nyama ili Serikali inapokwenda katika utekelezaji wake, basi iweze kuyatekeleza haya kwa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la afya. Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa huduma ya afya hasa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam. Serikali iliwahi kuzipandisha hadhi hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala kuwa katika hadhi ya Hospitali za Mkoa, lakini baada ya kuzifanyia hivyo, haijawahi kuzipa support kwa maana ya kuzihudumia kama Hospitali za Mkoa na badala yake majukumu hayo yameachiwa Halmashauri, na kwa uwezo wa Halmashauri zetu imekuwa ni vigumu kuhakikisha inaboresha huduma katika hospitali hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana sasa hivi hospitali hizi za Temeke, Amana na Mwananyamala zimebaki kuwa kama sehemu ya mifano mibaya, yaani ukitaka kutoa mifano mibaya au kuonesha watu kwamba huduma mbaya hospitalini zinapatikana wapi, basi ni vizuri ukawapeleka katika hospitali hizi, maana watashuhudia wagonjwa wanalala chini, dawa hakuna, au wengine wakilala watatu watatu kwenye vitanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali hii ya Awamu ya Tano ikahakikisha kwamba matatizo ya vitanda, wauguzi na dawa hospitalini yanakwisha kabisa. Tupatiwe vitanda vya kutosha katika Hospitali ya Temeke, tupate madawa, wananchi watibiwe pale; na wakifika waone kwamba wamefika sehemu salama na magonjwa yao yatakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni elimu. Serikali imeanza kwa kuondoa michango na ada, lakini hili ni suala dogo sana katika matatizo ya elimu yanayoikabili nchi hii. Bado hizi shule, hasa Shule za Msingi. Kwa Dar es Salaam tu ukitembelea Shule za Msingi utagundua
kwamba shule zina matatizo makubwa, achilia mbali tatizo la madawati, lakini majengo yenyewe, mapaa yametoboka, sakafu zimekwisha. Kuna madarasa ukipita unaweza kufikiri kwamba hapa ni kituo cha kuwekea ng‟ombe kabla hawajakwenda kuchinjwa, lakini kumbe ni
madarasa hayo, watoto wanakwenda kusoma pale. Unajiuliza, mtoto huyu anawezaje kuipenda shule akiwa anakaa chini, hana madawati, sakafu imeharibika na juu kunavuja?
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tunakoelekea katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali iamue jambo moja, itoe mikopo ya elimu kuanzia Shule za Msingi ili mzazi aweze kuchagua shule ya kumpeleka mtoto wake kulingana na viwango vya ufaulu na siyo kwa sababu tu hana ada.
Hii itatusaidia kuondoa ile gap ya nani anasoma katika shule nzuri na nani asome katika shule mbaya. Maana yake anayesoma katika shule nzuri ndiye atafanikiwa; na hao ni watoto wa matajiri; hao ambao wanasoma kwenye shule hi zo mbovu, hawawezi kufanikiwa, tunaua vipaji
vyao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa napenda Serikali ilichukulie hili kama jambo muhimu sana. Tuondoe madaraja ya elimu kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake alizungumzia suala la Mahakama Maalum kwa ajili ya Mafisadi, lakini amesahau pia kuzungumzia Mahakama Maalum ya wale wanaowatesa na kuwaua ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu tumekuwa na hili tatizo. Albino wanauawa, wanakatwa viungo vyao, na hizi kesi zao zinachelewa sana Mahakamani. Mwisho wa siku hata wale wachache ambao wamehukumiwa, hasa waliohukumiwa vifungo vya kunyongwa hadi
kufa, inasemekana hakuna aliyewahi kunyongwa. Hiyo ni kwa sababu kabla ya utekelezaji wa hiyo adhabu, Mheshimiwa Rais anahitaji kusaini kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya kikatiba.
Sasa tumtake Rais huyu wa Awamu ya Tano atuoneshe mfano kwamba na yeye anachukizwa na mauaji ya albino. Atie nguvu kuhakikisha kesi zile zinasikilizwa na zinafika mwisho haraka. Waliohukumiwa kunyongwa, wanyongwe mpaka kufa ili jamii ione kwamba kweli Serikali imeamua kukomesha tatizo la mauaji ya albino. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la uingizaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya. Kwa sisi tunaokaa Dar es Salaam hasa pale Jimboni kwangu Temeke ambako ni moja kati ya maeneo ambayo yameathirika na matumizi haya ya dawa za kulevya, hatuamini kama kweli Serikali imewahi kuchukua jitihada za dhati au ina mipango ya dhati ya kukomesha uingizwaji na usambazwaji wa dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa uingizaji wa dawa za kulevya katika nchi hii haujawahi kuyumbishwa hata kidogo. Mfumo wa kuingiza mafuta ya petroli ukiyumba, siku mbili tu utaona watu wanahangaika kutafuta mafuta. Mfumo wa chakula ukiyumba, utaona watu
wanahangaika kutafuta chakula, lakini niwahakikishieni, hatujawahi kuona hawa watumiaji wa dawa za kulevya wakihangaika kutafuta dawa hizo. Maana yake mfumo wa kuingiza na kusambaza haujawahi kuyumbishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaitaka Serikali hii ya Awamu ya Tano kuweka jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba inadhibiti uingizaji wa dawa za kulevya, lakini pia usambazaji huko mitaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku tunapishana na polisi na magari yao hayo maarufu kama defender, wamekamata wauza gongo na wauza bangi, lakini hatuoni wakikamata hawa wanaouza dawa za kulevya. Huwezi kuniambia kwamba wanaouza haya dawa za kulevya
wanajificha sana, kwa sababu wale watumiaji wenyewe muda wote unawakuta kama wameshalewa, lakini akizunguka nyumba ya pili, ya tatu ameshapata, anatumia tena. Ni kwa nini Serikali haiwaoni? Kwa nini isidhibiti huku kwa wauzaji wadogo wadogo ambao ndio
wanaotuharibia vijana wetu na ndugu zetu? Kwa hiyo, tunaomba Serikali ya Awamu ya Tano iweke macho sana katika kukomesha
uingizaji wa dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni hili la amani na usalama. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake pale ukurasa wa kumi amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Wananchi (CUF) na CCM zinafanya jitihada ya kuondoa tatizo
la kisiasa lililopo Zanzibar. Hapa ukiangalia kauli hii ni kama vile Mheshimiwa Rais anajitoa katika kushughulikia tatizo la Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, unawezaje kuiachia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ishughulikie tatizo la Zanzibar wakati tatizo lenyewe linahusu kuiweka Serikali madarakani? Serikali imemaliza muda wake, Serikali nyingine haitaki kutangazwa. Tumtake Mheshimiwa Rais ambaye kimsingi wananchi tuna imani naye kubwa sana, ameanza kuonesha kwamba analolisema analitekeleza. Hebu aamue sasa kusema kwamba aliyeshinda katika uchaguzi wa Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2015 atangazwe kuwa Rais. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Uchaguzi haujaisha! (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kuona suala la Zanzibar kama ni la Zanzibar, lakini hili suala siyo la Zanzibar, ni suala la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii heshima ya amani na usalama ambayo Watanzania tunayo leo ni kwa sababu
nchi nzima iko salama. Sehemu moja ikianza kutumbukia katika machafuko, hakuna atakayekuwa salama hata huku kwetu. Kwa hiyo, tulichukulie hili jambo kama suala la Kitaifa na siyo suala la kisiasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu anafahamu kilichotokea katika uchaguzi wa Zanzibar. Mshindi kapatikana na kama kuna matatizo kwenye baadhi ya Majimbo, uchaguzi urudiwe kwenye Majimbo hayo ambayo yana matatizo, siyo uchaguzi wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuiombe Serikali hii, tumwombe Mheshimiwa Rais ahakikishe…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtolea, ahsante. Naomba umalize.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, tumwombe Mheshimiwa Rais ahakikishe mshindi kwa uchaguzi wa Zanzibar anatangwazwa. Ahsante. (Makofi)