Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwanza kwa ushindi mkubwa alioupata lakini kwa kazi kubwa anazofanya hadi hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hayo, moja ya eneo kubwa ambalo limekuwa likileta shida sana katika mambo ambayo sisi wana-CCM tumekuwa tukiahidi ni utengaji wa fedha kwa ajili ya sekta ya miundombinu. Kwa mara ya kwanza Mheshimiwa Rais amekuwa kwenye ofisi hiyo na tumeshuhudia shilingi trilioni zaidi ya nne zimetengwa kwa ajili ya miundombinu. Naomba nimpongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, naomba nionyeshe masikitiko yangu kwenye baadhi ya maeneo. Baadhi ya Wabunge wamezungumzia, ninaamini kwamba fedha hizi zingeweza kufanya kazi nzuri sana katika utekelezaji wa Ilani yetu ya CCM, lakini ninavyoona kuna hatari kubwa ya kutapanya fedha hizi kwenye maeneo mengi na mengine ambayo wala hayaendani kwa kiasi kikubwa na Vision 2020 - 2025 na mengine wala hayawiani na ahadi ambazo tulizitoa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la reli. Reli ya kati iko katika Ilani ya CCM, ukisoma Ilani yetu tuliahidi ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge. Si kwamba tutaanza, si kwamba tutafanya feasibility study au tutafanya kitu kingine chochote. Mimi kama Mwenyekiti wa Wabunge wanaotoka kwenye ukanda unaopitiwa na reli ya kati, tumekuwa na mazungumzo kwa nyakati kadhaa na Mheshimiwa Waziri tukizungumzia suala hili na hata tunapokuja kwenye bajeti yake tulikuwa hatujakutana kuzungumza na kuweka mkakati na Wabunge wenzangu kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekuwa akituhakikishia mipango aliyoweka kwenye bajeti yake itahakikisha reli inajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kusema kwamba Waziri ametu-betray kwa sababu upembuzi yakinifu na mambo mengine ya awali kabla ya ujenzi kuanza yalikuwa yameshakamilika na tulichokuwa tunategemea kwa hatua ya sasa ni kutafuta fedha na kuanza kujenga. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote ambao tunatumia reli ya kati, ambao wananchi wetu wanaumia kimaisha kutokana na ughali wa bidhaa zote tuliangalie suala hili. Kwa mfano, mabati, nondo, cement zote zinatoka Ukanda wa Pwani, viwanda vyote vya cement viko Ukanda wa Pwani lakini ujenzi unafanyika mpaka Kigoma. Mfuko wa cement Kigoma ni zaidi ya shilingi 20,000/=, mfuko wa cement Dar es Salaam ni shilingi 12,000/=, shilingi 8,000 anayolipa mwananchi wa Kigoma ni adhabu anayopewa kwa sababu tu Mheshimiwa Waziri hajachukuwa hatua za kujenga reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hatua hazichakuliwa kwa sababu ukisoma ukurasa, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote tuchukuwe vitabu vya hotuba ya Waziri, muangalie ukurasa wa 72, ile Iibara ya 127. Ukisoma ile ibara inasema, mpango uliokuwepo mwanzo ulikuwa ni wa kujenga reli kwanza kwa kujenga sisi wenyewe lakini pia kwa kutumia mpango wa PPP, Serikali imiliki reli, sekta binafisi iendeshe. Waziri anasema mpango huo umekwama na sasa wamefuta mwezi Februari baada ya kukutana na Mawaziri wenzake wa Rwanda na Burundi sijui wanachangia shilingi ngapi katika ujenzi wa reli ya kwenda Mwanza, mbaya zaidi wamefuta na sasa wanasema utajengwa kwa utaratibu mwingine unaitwa Sanifu, Jenga, Endesha, Kabidhi. Utaratibu huu utaanzia kwenye design ambayo inaonyesha kwamba itakamilika baada ya miezi 24. Ukihesabu miezi 24 kuanzia sasa obvious itakwenda zaidi ya mwaka 2019 na ilani yetu ya CCM ilisema tutajenga reli kabla ya mwaka 2020, tutakuwa tumeiba kura za wananchi kwa kuahidi reli ambayo haitakuwepo. (Mkaofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza naomba niseme maelezo ya Waziri hayajaniridhisha kwenye suala hili. Kwa maana hiyo nilikuwa naomba endapo Waziri katika majumuisho yake hatasema ni nini kitafanyika kuanza kujenga reli wala siyo maneno yaliyoko kwenye ukurasa wa 72 nilioonyesha, mimi binafisi na Wabunge wenzangu nitawashawishi sana wote tunaotumia reli ya kati tusikubaliane na jambo hili hadi tutakapohakikisha reli inajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siko tayari mimi kuhukumiwa kwa kuiba kura, nimesimama Isaka niwaambia reli inajengwa sikuwaambia kwamba tunaanza kujenga kwa utaratibu tofauti, sikuwaambia kwamba tunaanza upembuzi yakinifu, tulisema tunaanza kujenga reli. Naomba reli ijengwe, bila kufanya hivyo Wabunge wote tunachimbiwa shimo, Mheshimiwa Mwakasaka hutarudi na rafiki zangu wote hamtarudi kwa sababu reli haitajengwa na hata Mheshimiwa Genzabuke hautarudi. Mpango wa ujenzi wa reli hauridhishi na hauendani na ahadi tulizotoa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia suala hilo, naomba nizungumzie suala lingine la barabara na hapa nizungumzie barabara yangu ambayo kimsingi inakidhi vigezo vyote. Mbunge mmoja amesema kwamba tunataka barabara zinazounganisha mikoa na mikoa ndipo twende kwenye barabara zinazounganisha wilaya na wilaya na baadaye kata na kata. Wote ni Watanzania na wote tunalipa kodi, tumekuwa tukizungumza toka mimi nimekuwa Mbunge mwaka 2005 kuunganisha mkoa wa Shinyanga na Geita. Tunasema kuunganisha, kwanza ni kuunganisha mkoa na mkoa lakini baya zaidi maeneo haya yana uchumi mkubwa unaoendesha uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kahama kuna migodi miwili, Mgodi wa Bulyanhulu na Mgodi wa Buzwagi, Geita kuna Mgodi wa Geita. Si mara moja wala mara mbili mimi nimezungumza na wenye migodi ile na bahati mbaya kanuni haziruhusu lakini ningeomba kama utaruhusu tutengue kanuni tumkaribishe Injinia Dabalize aliyekuwa Mhandisi wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, tulishazungumza na watu wa Mgodi wa Bulyanhulu, tulishazungumza na watu wa Mgodi wa Geita wanasema wako tayari kushiriki katika ujenzi wa barabara ya Kahama - Geita kwa kiwango cha lami, upembuzi yakinifu umeshakamilika. Kwenye hotuba ya Waziri barabara hiyo wala haijatajwa, wala hajaonyesha nia yoyote ya kuzungumza na hawa wawekezaji ambao wako tayari kushiriki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kahama, Msalala, Geita siyo kwamba tu wanahitaji barabara hiyo kwa sababu ya umuhimu wake wa kibiashara lakini wanahitaji pia kwa sababu ya masuala mazima ya afya.
Waheshimiwa Wabunge wenzangu hii barabara kwa wale ambao hamjaipitia, inapitisha malori yenye kusomba mafuta kupeleka mgodi wa Bulyanhulu, inapitisha malori yanayosomba mchanga wa dhahabu kutoka mgodi wa Bulyanhulu kwenda nje ya nchi na kwa wastani kwa siku zinapita semi trailer zaidi ya 200. TANROADS Shinyanga na Geita wamejaribu kuwa wanakarabati barabara hii lakini haiishi zaidi ya miezi miwili imeshaharibika. Sasa niulize, hivi nini kinakwamisha kuanza ujenzi wa barabara hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sana Mheshimiwa Rais ambaye alikuwa Waziri wa Ujenzi miaka ya nyuma, alisema na akahakikisha kwamba barabara hii itaanza kujengwa immediately baada ya kuwa ameshaingia madarakani kama Rais.
Ninaamini jambo hili Mheshimiwa Rais halifahamu na naomba Mheshimiwa Rais huko uliko ufahamu kwamba Mheshimiwa Profesa Mbarawa hajaanza kuweka mpango wa kujenga barabara ya Kahama - Geita kama ulivyoahidi ulivyokuwa unahutubia wananchi wa Kahama. Ninaamini amefanya hivyo kinyume cha dhamira yako, kinyume cha matakwa ya Watanzania wanaoishi Kahama na Geita. Naomba Mheshimiwa Waziri tafuta fedha ujenge hii barabara, upembuzi yakinifu umekamilika, wawekezaji wa hiyo migodi wako tayari kuchangia ili mradi Serikali ikubaliane nao namna ya kurekebisha masuala ya kodi, kufanya tax rebate kwa miaka ya mbele kutokana na uchangiaji watakaokuwa wamefanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimepigiwa kengele nimalizie kwa kuomba sana kwamba Kanda ya Ziwa tunategemea uwanja wa ndege wa Mwanza uwe wa Kimataifa kwani utafungua ukanda wetu ule ili tuweze kupata watalii. Nimeona kuna fedha zimetengwa lakini ningeomba tu Waziri atuambie hivi ni lini uwanja wa ndege wa Mwanza utakamilika kujengwa kwa kiwango cha kimataifa na utakuwa International Airport ili wageni waingilie uwanja wa ndege wa Mwanza, waingie Serengeti watokee KIA au waingilie KIA waje watokee Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona bado kuna dakika chache, nimalizie kwa kusema jambo lingine kwamba ili kupunguza msongamano wa malori Dar es Salaam kumekuwepo na pendekezo la kuweka dry port nje ya Dar es Salaam hasa eneo la Kibaha. Naomba Wizara hii ilichukulie jambo hili kwa uzito unaostahili, tujenge bandari kavu eneo la Kibaha ili malori yasiwe yanaingia Dar es Salaam hasa kwa kuangalia misongamano na ajali zinazotokea ambazo kwa kwa kweli hazina maana yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Niombe kwa dakika chache zilizobaki feasibility study ya barabara ya kutoka Kahama - Mwanza kupitia Bulige na Solwa ianze. Feasibility study ya barabara ya kutoka Kahama - Msalala - Nyang‟hwale - Busisi ianze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Mheshimiwa Rais na Makamu wa Rais walipokuja Nyang‟hwale pale kwenye mkutano Karumwa waliahidi barabara ya kutoka Busisi - Sengerema - Nyang‟hwale – Karumwa - Msalala - Kahama nayo itajengwa kwa kiwango cha lami. Ni barabara inayounganisha mikoa mitatu na ina sifa zote za kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.