Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Na mimi pia nimshukuru Profesa Muhongo kwasababu kwenye Bunge la mwanzo mwezi wa pili aliunda kamati ya kwenda kuchunguza suala la Nyamongo na ndugu yangu Agness pale anasema aliniteua, mimi sikuteuliwa na Profesa ni vyema nikaweka wazi haya mambo yakajulikana.
Kwa hiyo, nampongeza Profesa kwa ile kazi na wananchi wa Nyamongo wanasubiria majibu yao kwa matatizo yale makubwa ambayo yamekuwa pale kwa miaka yote. Leo nilitaka tu niseme kidogo kuhusiana na historia ya mgodi ule wa Nyamongo na utofauti wake na migodi mingine ili Profesa uelewe unapokwenda kutoa majibu ya wale wananchi, utoe majibu ukijua hilo kichwani kwako.
Kwanza ule mgodi ni tofauti na migodi mingine ambayo wazungu wanakwenda wanapata eneo porini huko, wanaanzisha uchimbaji, wanafanya exploration na wanaanza kuchimba. Ule mgodi ni mgodi wa wananchi tangu mwaka 1911, watu wa pale walianza kuchimba madini pale kabla hata ya ukoloni na kabla ya Uhuru. Watu wa eneo lile hawana hata eneo la kulima, kwa hiyo waalikuwa maisha yao yote yanategemea uchimbaji wa madini ya Nyamongo, ndivyo maisha yao yalivyokuwa kwa miaka yote. Mwaka 1994, Serikali haya maamuzi ya kuamuliwa Dar es Salaam; Serikali ikachukua leseni ikawapa wazungu. Ina maana ikabadilisha economic activity ya watu, kama mimi nafanya biashara ya duka, leo unakuja unafunga duka langu, hunioneshi kazi nyingine mbadala ya kufanya. Kwa hiyo, Serikali ikachukua leseni ikawapa wazungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungu wakaja wakatwaa eneo na ule mgodi uko katikati ya makazi ya watu. Wakatwaa eneo, migogoro ikaanza tangia mwaka 1994. Mauaji kila mwaka, tena siyo kila mwaka, karibia kila siku na juzi tarehe 7 mwezi huu umesikia ndiyo mauaji ya mwisho yametokea. Wananchi wale tumebadilisha uchumi wao, hatutaki kuwaandalia njia mbadala, hatujawapa hata mita moja. Nimesoma hapa Profesa uje ufafanue, umesema kwenye ukurasa wa 50 kwamba mmewatengea eneo, liko wapi? Hilo eneo mmewapa wachimbaji wapi? Kwa sababu mimi na wewe tulikuwa pale na demand yao ni hii na mimi najua hujatoa taarifa, hujapeleka taarifa ile kwa wananchi lakini umesema ukurasa wa 50 kuna eneo limetengwa kwa wachimbaji wale, akina nani? Hilo eneo halipo na hii ndiyo imekuwa mgogoro siku zote Profesa, pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka kuingia pale wachukue kwa sababu hawawezi kufa kwa njaa, wakati mali yao wanachukua wazungu wanaondoka nayo, haiwezekani, ni lazima kutafuta suluhu. Tangia mwaka 1994 Watanzania wenzetu zaidi ya 400 wameuawa pale mgodini. Watu wamebaki na vilema vya maisha, wengi tu ambao hawana idadi. Na hili suala ni suala ambalo kama hatutatatua kwa kuwapa wananchi eneo la kuchimba, hakuna suluhu pale. Wale wazungu wametumia shilingi bilioni 21 kujenga ukuta, yaani badala ya kutengeneza mahusiano na wananchi kwa kupeleka hizo pesa kwenye maendeleo wamejenga ukuta zaidi ya kilometa 10 na kitu, shilingi bilioni 21 ukuta mrefu na bado haiwi suluhu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mkuu wa Wilaya anasema kwamba mtu aliyepigwa risasi alikuwa ameenda rompad kuiba madini. Eti anasema rompad kuna madini. Mimi nimefanya kazi pale mgodini Nyamongo, rompad hawaweki madini, wanaweka mawe na mawe yanakuwa pale zaidi ya tani 2,000, 3,000. Mtu anaenda na kamkoba kuchukua jiwe pale ambalo halifiki hata kilo moja unampiga risasi una-justify kifo chake eti alikuwa ameenda rompad kuchukua madini, hata hajui amekurupuka tu. Mkuu wa Mkoa anakuja bila heshima anasema waliopigwa risasi ni wahuni kwamba wananchi wa Tarime wanauawa halafu mnawaita wahuni? na nilitamani Waziri Mkuu awe hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutakubali kauli za aina hiyo kwa wananchi wa Tarime ambao mali yao imechukuliwa, inasafirishwa kila siku na Profesa hapa leo mimi nimekuwa mpole sana kwa sababu nategemea utatoa majibu ambayo ni positive, lakini kauli kama zile za Magesa Mulongo kwa watu wa Tarime na watu wa Mkoa wa Mara; Profesa wewe unajua sisi sio wanafiki – nyeupe ni nyeupe. Nilikuwa naona wengine wanakupongeza huko ambao tu walitumika mwaka jana kuku-crucify. Bora sisi ambao tumesema na msimamo wetu umebaki pale pale. Sisi si wanafiki. Wengine ooh Profesa tunashukuru Mungu amekuleta tena, hawa hawa! (Makofi/Vicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Profesa, ninakuomba tatua mgogoro wa watu wa Nyamongo. Nilipokuwa form two nasoma historia wanasema sababu zilizosababisha kukua kwa miji kama Johannesburg, ni kuwepo kwa madini pale. Lakini wewe umeenda Nyamongo pale hata mita moja ya lami tangu mwaka 1994 hakuna. Halafu mnataka Wakurya waendelee kupigia makofi mambo yale, madini yanaondoka. Tunabaki na mashimo, milima, unakuta vijana zaidi ya 2,000 wako kule juu ya mawe. Siku mgodi ukifungwa sijui watakwenda wapi? Mkoa wa Mara hautakalika. Serikali haioni, sisi tunaolia kila siku saidieni hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa wenyekiti, Waziri Mkuu angekuwa hapa asikie, Waziri wa Mambo ya Ndani na Mawaziri wengine msikie. Mgodi unalipa mpaka askari, mimi naamini askari analipwa kulinda mwekezaji na analipwa na Serikali. Lakini mgodi sasa hivi unalipa askari kila siku shilingi 50,000, askari wanaokwenda kulinda ule mgodi na ndiyo maana wamekuwa loyal kwa mgodi. Mtu wa mgodi akiwaamrisha kupiga Mtanzania risasi wanapiga tu, hawajali. Askari wamekuwa wanyama pale. Juzi wanakwenda kwenye Kituo cha Afya, wanapiga risasi Kituo cha Afya? Kuna watu wanafanyiwa upasuaji pale, kuna watu wana pressure pale, wanapiga mpaka mama ambaye anachukua dawa pale, na Tanzania mambo haya mnaona ni sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema na hii ni kauli yangu na ni kweli tupu, lazima yale mauaji yakome pale. Yasipoisha askari wenu wale wataniua mimi, nawaambia ukweli. Wataniua mimi kabla sijamaliza Ubunge wangu. Siwezi kukubali tena waendelee kuua wananchi pale. Nitawapelekea wananchi laki moja pale, watatupiga risasi hawatatumaliza, watajiua wenyewe baadaye. Tangu mwaka 1994 Wakurya wanauawa kama wanyama hata Profesa Maghembe hapa ukigusa swala pale porini hawezi kukubali. Huyu hapa na TANAPA yake gusa swala mle ndani uone kama atakubali, sembuse mtu? Watu wanauawa kama wanyama halafu sisi tukae hapa tunapiga makofi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba Profesa tunaomba suala la wachimbaji wadogo lile lipatiwe ufumbuzi. Watu wapate eneo kwa sababu mzungu amekuja akawakuta wanachimba Nyabirama, amewakuta wanachimba pale Nyarugusu, amechukua lile eneo hamjatengea wananchi maeneo. Bila kufanya hivyo mgogoro ule hautaisha, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu, tutaunda kamati na kamati. Achilia mbali DC amekwenda pale amehamisha mto, tulikuwa na wewe unaona pale, umemuhoji bila aibu DC anafanya maamuzi ya kuhamisha mto sasa ule mto mvua ikinyesha una flood kwenye mazao ya watu kwa sababu ya maslahi ya wazungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, DC anakuja pale siku mbili anajifanya mkali, wazungu wanamchukua wanamweka mfukoni tayari anaanza kuimba nyimbo za wazungu kama yule wa pale. Sasa hivi ukigusa mgodi anasema ua, ndiyo suluhu anayoona. Kwa hiyo ninakuomba Profesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili yale magari ya mgodi yanayosomba mafuta, tuko karibu kuyawekea magogo kuyazuia yasitembee kwenye barabara zetu, kwa sababu yale magari wazungu wale hawarekebishi barabara, Halmashauri tunahangaika na barabara kwa vifedha vyetu vidogo wao wanatembeza mzigo mkubwa. Kama wanataka warekebishe ile barabara yao ya chini ya mgodi, ile ya kule chini watembeze magari yao. Wakipita huku juu ntawahamasisha wananchi wataweka magogo watayapiga mawe. Hatuwezi kukubali watembeze pale, hawaleti hela pale wanataka watembeze, wanatembezaje magari kwenye barabara yetu pale? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, Profesa kuna uamuzi unaweza ukafanya ambao hautakusababisha upigiwe makofi sana…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Heche, muda wako umemalizika.