Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushuru kwa kunipa nafasi hii, namshukuru Ndugu yangu Mheshimiwa Lukuvi; Mheshimiwa Mabula ambaye ni jirani yetu Kanda ya Ziwa. Tumshukuru Rais kwa kuwapa nafasi hiyo, mnafaa kupewa nafasi hiyo na Mungu awasaidie muweze kutongoza vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti,nimeangalia taarifa hizi za Kamati ya Ardhi na Kambi Rasmi ya Upinzani wamesema vizuri sana. Wametofautiana kitu kimoja tu, hawa waCCM wameunga mkono, wale wa upinzani wameunga mkono kwa kushauri kwamba Serikali ikae pamoja itatue migogoro, jambo zuri sana.
Namshukuru rafiki yangu wa Bukoba Town na leo ni mnada, kwa hiyo, tutajua namna ya kufanya huko. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye mambo muhimu na naomba niulize maswali ambayo natakiwa wakati unakuja hapa ku-wind up uweze kuyatolea ufafanuzi. Ni nani anapima mipaka kati ya vijiji na hifadhi za wanyamapori? Kama ni Wizara ya Ardhi inapima, inakuwaje mpaka huo buffer zone moja iwe na kilometa kadhaa na buffer zone nyingine au kutoka mpaka wa wanyamapori kwenda kwa binadamu ni nusu kilometa; lakini kutoka mpaka wa wananchi kwenda porini ni zero. Nani anapima mipaka hiyo na kwa upendeleo gani wa aina hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanapima wataalamu wa wanyamapori, kweli wanaweza kutenda haki? Mipaka ya Jimbo langu la Rubana, kwa Mto Rubana, ukiingia mtoni, ukivuka tu, umekamatwa. Ukivuka mto tu, umekematwa; lakini wao kutoka mpakani, mita 500 ambayo ni nusu kilometa. Kwa hiyo, ina maana mita 500 hizo kama kuna mazao yakiliwa na wanyamapori, hakuna kulipwa. Hakuna malipo! Hawa jamaa wamejiwekea sheria, unalipa kutoka kilometa moja mpaka kilometa tano ndiyo unalipwa na unalipwa kwa heka moja shilingi 100,000. Kwa hiyo, kama tembo amekula mazao heka 20, unalipwa heka tano, heka 15 ni sadaka ya Serikali. Nani alifanya maneno ya namna hii? Tunataka kujua nani anapima hii mipaka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nani anatatua migogoro kati ya hifadhi ya wanyamapori na wananchi? Maana yake wamelalamika mika nenda-rudi, hakuna mtu anaenda. Tuna eneo moja linaitwa Kawanga; mpaka uchaguzi wa mwaka 1995 ulimtoa Waziri Mkuu, hiyo Kawanga. Aliuliza swali, nani atatatua mgogoro wa Kawanga? Akasema hii ni sheria, tutakwenda kufanya. Wakasema hapana, sisi tumeshachoka. Mpaka leo mgogoro upo, Mawaziri wameenda watano, sita, wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Mawaziri wengine mlioko humu ndani, hebu tuambieni, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Waziri wa Ardhi, wametamka humu Bungeni kwamba watakaa vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii watatue migogoro ya wakulima, wafugaji na Hifadhi za Taifa, mtakaa mtatue. Uchaguzi tumetoka juzi! Mheshimiwa Rais wetu mtiifu amesema wafugaji sitawangusha. Tumetoka juzi tu, lakini operation zinaendelea kukamata watu. Hii maana yake nini hasa? Migogoro haijatatuliwa, watu wanakamatwa, watu wanatolewa; nani sasa amesema wewe uko sahihi kutoa watu? Tupo tu tunaangalia. Mheshimiwa Lukuvi, nafasi yako naitaka, ikifika miaka miwili na nusu miaka ijayo kama migogoro haijaisha angalau hata robo, wewe toka tu mimi niingie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mgogoro wa Jimbo la Bunda, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri, ameandika vizuri sana hapa. Mgogoro wa Bunda kati ya Wilaya tatu; kuna Serengeti, Bunda na Musoma Vijijini. Mgogoro wa mwaka 1941 mpaka leo haujaisha. Watu wanapigana, wanauana mgogoro upo tu. Mheshimiwa Mabula, wewe ulikuwepo Mkuu wa Wilaya ya Butiama, unaujua mgogoro. Mara uko TAMISEMI, mara uko Ardhi, mara uko wapi, toka miaka hiyo mpaka leo. Mimi sitaunga mkono hoja hii kama kweli mgogoro huu hautaniambia unaisha lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la Kyandege na wameliandika vizuri hapa. Sasa haya ni mambo ya ajabu. Wakati fulani hawa wenzetu wakisema maneno hapa, ingawaje sisi hatuna mpango wa kutoka madarakani, lakini wana maneno yao mazuri. Hivi inakuwaje? Kwa mfano, inakuwaje GN ya kijiji imetoka; na imetoka Makao Makuu ya Ardhi, imekwenda kijijini; imeandika mpaka kati ya kijiji ni kaskazini na kusini, lakini anayekwenda kukata mipaka kutoka Halmashauri au sijui kutoka wapi, anaenda anakata Magharibi Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamelalamika toka 2007 mpaka leo; eneo hilo tu moja, Muliyanchoka kweli hii? Hapana, hii hapana! Kwa hiyo, naomba kujua hili tatizo litaisha lini? Kwa kweli kusema kweli yapo mambo ya msingi ya kufanya, lakini vinginevyo nakushukuru sana unajitahidi kufanya. Tatizo tulilokuwa nalo, Waziri ulielewe na Mawaziri wote mlielewe, mnafanya kazi sana ya kutumikia watu lakini watumishi wenu wakati fulani wanasema ninyi wanasiasa tu. Watumishi wenu wanawaangusha sana ninyi. Kila ukisema maneno wanakwambia huyu ni mwanasiasa tu. Sasa muangalie, hao wanaosema wanasiasa waondoeni kwanza mbaki ninyi ambao mnafanya kazi. Nashukuru sana.
MWENYEKITI: Ahsante.