Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu asubuhi hii ya leo, nikushukuru wewe pia kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Naibu wake Dkt. Angelina Mabula kwa kazi nzuri wanayofanya, niwape pole kwa changamoto nyingi wanazokumbana nazo ndani ya Wizara hii, kwani zipo nyingi zikiwemo zile za migogoro ya ardhi ambazo zimekuwa ni za muda mrefu na zenye kuhitaji hekima na busara katika kuzitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa gender sensitivity nipende kumshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kumteua mwanamama Dkt. Angelina Mabula kuwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Baada ya salamu hizi naomba nijielekeze katika kuchangia hotuba iliyoko mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina hekta milioni 88.6 za nchi kavu na kati ya hizo ni hekta milioni 60 ambazo ni mbuga na zina uwezo wa ku-accommodate ufugaji. Pamoja na kuwa na eneo kubwa la kututosheleza bado kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na migogoro hii imekuwa ikisababisha ulemavu vifo, upotevu wa mali lakini hata wananchi kuhama makazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua jitihada ya Wizara hii katika kutatua migogoro hii lakini naiomba Serikali ikae itafakari, itafute mbinu mbadala na rafiki kutatua matatizo haya. Hata pale inapowezekana ishirikishe wazee wa kimila katika kuwashawishi wakulima na wafugaji kutumia maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli zao. Niishauri Serikali kutengeneza mifumo ya kuzuia kuliko kutengeneza mifumo ya kupambana baada ya matatizo haya kufumuka. Kubwa zaidi niishauri Serikali kuhakikisha inafanya utafiti ili iweze kujua vyanzo halisi vya migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaisihi Serikali kuona haja ya kutambua ufugaji wa asili katika Sera ya Taifa ya Ufugaji ya mwaka 2006, kwani ufugaji huu umekuwa ukichangia asilimia 7.4 ya Pato la Taifa. Kikubwa ni kutengeneza mfumo madhubuti kuhakikisha kwamba ufugaji huu haugeuki kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Sheria ya Ardhi kumekuwa na changamoto kubwa ya wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha wa sheria hiyo, kumekuwa na tafiti nyingi ambazo zimebainisha kwamba wananchi wanaoishi katika ngazi za msingi hususani vijijini wakiwemo wanawake, wakiwemo wafugaji, wachimbaji wadogo na wakulima wamekuwa wakikosa haki katika kumiliki ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi zipo mila ambazo zinamkandamiza mwanamke katika kumiliki ardhi, mila hizi zimekuwa zikimwaminisha mwanamke kwamba yeye ni wa kuolewa na kusubiri kurithi ardhi kutoka kwa mume wake. Hii tumeona changamoto yake kwamba, yapo baadhi ya makabila yanasadikika kwamba wanawake wao wanawaua waume zao ili waweze kurithi mali. Hii imekuwa ikiwanyima wanawake haki ya kupata, kutumia na kudhibiti ardhi moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iweke mpango mkakati wa kutoa elimu ya Sheria hii ya Ardhi katika ngazi ya vijiji ili wananchi waweze kujua haki zao katika kumiliki ardhi. Kama Sheria ya Ardhi Na. 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 za mwaka 1999 zinavyoainisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wawekezaji na ardhi; kumekuwa na tatizo la wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi na baadhi yao wamekuwa wakitumia sehemu ndogo tu ardhi hiyo, wapo ambao hawajaendeleza kabisa maeneo hayo na kusababisha mapori katikati ya vijiji na mara nyingi mapori haya yamekuwa yakitumika na wahalifu kama maeneo ya kujifichia. Vijana wa Kitanzania wana uhitaji mkubwa wa ardhi ili kuweza kufanya shughuli za kiuchumi, tukumbuke kwamba vijana hawa wa Kitanzania wamelelewa katika mila na desturi za Kiafrika ambapo mali zote ikiwemo ardhi ni za baba, hata pale wanapojitahidi kwenda shule na kuhitimu vyuo vikuu bado wanakuwa hawana fursa kubwa ya kupata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Wizara hii isitengeneze utaratibu wa kuwagawia maeneo ya ardhi vijana ili nao waweze ku-contribute katika uchumi wa nchi yetu. Kwa kufanya hivi tutakuwa tumepunguza tatizo ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara la wananchi kuvamia maeneo kama haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa kumiliki ardhi, kumekuwa na mlolongo mrefu katika umilikishaji wa ardhi, aidha kwa kupata cheti cha hakimiliki ya kimila ama kwa kupata hati. Hii imesababisha wawekezaji kukosa uvumilivu na kukimbilia katika nchi ambazo zina unafuu katika kumilikisha ardhi. Mlolongo huu mrefu umesababisha Watanzania kuwa wavivu wa kumiliki ardhi kihalali na kwa namna moja au nyingine tumekuwa tukiikosesha Serikali yetu mapato yanayotokana na ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 37(a) inasisitiza kuimarisha utoaji wa huduma za ardhi. Napenda kuiomba Serikali hii iweze kutekeleza Ilani hiyo ili kuweza kumsaidia Mtanzania kuweza kumiliki ardhi ndani ya muda mfupi. Hili linawezekana kama tu tukiziwezesha Halmashauri zetu za Wilaya kuajiri vijana wa kutosha na Wizara ijikite zaidi katika kampeni nyingi zikiwemo zile za upimaji wa ardhi kuanzia ngazi za Vijiji mpaka za Miji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijahitimisha napenda kuikumbusha Serikali kwamba ilikuja Wilayani kwetu Magu Jimbo la Mheshimiwa Kiswaga ikaomba eneo kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wananchi. Napenda kuwataarifu kwamba eneo hilo tayari lipo tunawasubiri tu ninyi mje muwekeze ili wananchi wetu waweze kunufaika kwa kupata nyumba bora kwa bei nafuu. Hata Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu tayari wameshawatengea eneo, tena eneo lipo halihitaji hata fidia ni kazi kwenu kuja kujenga nyumba hizo ili wananchi waweze kupata nyumba bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha, napenda kuungana na wenzangu wote kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.