Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii lakini pia namshukuru Mungu sana kwa kupata afya nzuri ya kusema hapa sasa. Kwanza nianze kushukuru sana Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kwa nini nasema haya? Kimsingi namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Lukuvi na Naibu wake kwa kufanya kazi hii ambayo imekuwa kero sana kwa wananchi wetu hasa kwenye migogoro ya ardhi. Mheshimiwa Lukuvi amejitahidi sana kwa kweli kama wachangiaji waliotangulia walivyosema, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa jitihada zake binafsi zinazoonekana na Wizara yake kwa ujumla kuonesha moyo dhahiri kabisa wa kutatua matatizo ya ardhi; hasa amefika kule kwetu Mbulu, alisaidia Halmashauri ya Mji kwa kweli kurudishiwa ardhi yake na amesaidia kwenye Bonde la Yaeda Chini kutatua mgogoro ulioko pale ambao nimeuona pia ameuandika katika kitabu chake hiki cha migogoro kwenye ukurasa wa 18.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri kwamba kwa kuwa sasa Sheria ya Ardhi inataka watu wengi au majority kupiga kura ili kutoa adhi, lakini kuna maeneo mengine wapo watu ambao ni minority, naomba wale pia wazingatiwe. Kwa mfano, kwenye eneo letu kule kuna watu wanaoitwa Wahadzabe; wale mara nyingi wanakula kwa kufanya kitu kinachoitwa uwindaji. Kwa hiyo, wana tabia ya kuhama na kurudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba waangaliwe, kwani ardhi yao katika lile bonde ni ndogo sana. Nashukuru kwanza kwa kufanya hatua ile, lakini angalau wale watu wawe considered katika ardhi ambayo kimsingi iko kule ambayo ni eneo pekee katika maeneo ambayo wanayo katika Mbuga ile ya Yaeda Chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, amezungumza Mbunge mwenzangu wa Mjini, kama kuna maeneo yenye migogoro Tanzania hasa ya ardhi, nafikiri ni kule kwetu Mbulu. Namshukuru Waziri kwa kweli kwa kutusaidia na kutuambia kwamba yuko tayari sasa kuja kuanzisha Baraza la Ardhi ambalo litafanyika kule kwetu Mbulu. Nami nimwambie kabisa, jana Jumapili nilikuwa nyumbani, wamekubali, wameshapanga majengo ya kumpa kuanzisha Baraza la Ardhi na Halmashauri imeshamwandikia barua, nafikiri ataipata na nafikiri mwenzangu amezungumza, sina sababu ya kuendelea na hilo, lakini nakushukuru sana, Mungu ambariki kwa sababu kwa kweli akileta maendeleo yale ya kusikiliza kero za wananchi kwa haraka, migogoro yote itakuwa rahisi kutatulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kuishauri Wizara hasa katika upimaji wa ardhi. Ili kuondoa migogoro, ni vyema basi Wizara ikajielekeza kuipima ardhi hasa ardhi yote ya Tanzania, pawe na Land Bank ambayo itaondoa kitu kinachoitwa migogoro mingi. Ardhi ya Tanzania ikipimwa ni rahisi kuondoa migogoro; tutaelewa kabisa huu ni mwisho na mpaka wa mji na hapa panaelekea kuwa kwa wafugaji na hapa ni wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi yetu ikipimwa, kwa sababu sasa hivi kuna GPS, kwa hiyo, ni rahisi sasa kutumia GPS, kwa mfano ile ya Tume ya Uchaguzi, hivyo, ni rahisi sana kupima ardhi yote ya Tanzania. Ardhi ile ikipimwa ni rahisi pia kujua nani anaishia wapi, migogoro mingi itapungua kwa ajili hii. Kwa hiyo, naishauri Wizara yetu hii ya ardhi, pamoja na kazi nzuri inayofanya, ipime ardhi hizi na ardhi ikishapimwa basi, inaweza kutatua migogoro kwa wingi sana kila mtu akijua mipaka yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nizungumzie jambo la utaratibu wa kupata hatimiliki. Naiomba Wizara ifupishe kidogo utaratibu au iende kasi ya upatikanaji wa hatimiliki kwa wananchi wetu. Maana sasa hivi ukitaka kupata hatimiliki, kwa kweli unatumia utaratibu mrefu sana mpaka kuipata hati hii. Kupata wapimaji kwenye maeneo yetu ni kazi. Kwa mfano, katika Mkoa wa Manyara hasa Wilaya ya Mbulu, hatuna wapima ardhi, kwa hiyo, inachukua muda mwingi sana mpaka mtu apate hatimiliki ya kiwanja chake ili aweze kukiendeleza au kuombea mkopo au kufanyia maendeleo fulani. Nashauri haya, basi Wizara ijitahidi katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna jambo lingine ambalo napenda kulieleza. Kuna upimaji wa miji na upimaji wa miji midogo. Niombe sasa Wizara ijikite na ielekeze namna nzuri ya upimaji wa miji. Miji ikipimwa; kwa mfano, miji midogo ikipimwa na miji ikapimwa itakuwa rahisi sasa matumizi bora ya ardhi kufanyika. Sasa hivi maeneo mengi yanavunjwa kwa sababu hatuna plan management ya ardhi katika miji yetu midogo na mikubwa. Kwa hiyo, naiomba Wizara ijikite katika hali hii ya kupima miji yetu ili pawe na plan ya mji wowote unaoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kule kwetu kuna Miji ya Haidom ambao sasa tumeuombea kuwa mji na Mji wa Dongobesh ambao unazidi kuwa mji na Mji wa Mbulu ambao kimsingi ni wa siku nyingi, lakini una ramani nyingi ambazo nashukuru Mheshimiwa Waziri alipokuja alisema kabisa kwamba atatusaidia kutupatia mpima atakayesaidia kupima ule Mji wa Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa miji hii midogo ambayo sasa inakua, ufanyike upimaji mahususi wa mwanzo na miji mingine Tanzania ili migogoro isiwepo kwa sababu Maafisa wengi wa ardhi wanapata shida. Maeneo mengi hasa ya makorongo, maeneo ya kutoa maji yanaleta shida sana katika maeneo haya, kama ardhi isipopimwa hasa kwenye miji hii ambayo tunategemea kuwa miji mikubwa baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hela ambazo zinaitwa retention ambazo kimsingi Halmashauri zinakusanya kama maduhuli na zinakuja Wizarani, basi Wizara ihakikishe zile hela zinarudishwa kule ili Halmashauri zetu ziweze kujiendesha kwa kutumia hela za retention ambazo Serikali kuu inakusanya kupitia Hamashauri zetu. Maana Halmashauri zetu pia hicho ni chanzo cha pato na ni pato mojawapo ambalo likirudishwa kule kwa haraka basi, Halmashauri zinaweza kujiendeleza, zikaendelea kufanya mpango wa upimaji katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, napenda kujielekeza kwenye habari hii ya nyumba zenye bei nafuu. Tumeona mpango mzuri wa Mheshimiwa Waziri; kwanza nampongeza sana. Nina Bag hapa, yuko mchangiaji alisema hapa, sitaki kumtaja jina, anasema Wizara haikujipanga. Wizara imejipanga. Nimelisoma hili Bag! Yaliyomo humu ukiyasoma kama Mbunge ukayaona yalivyokuwa yanaelekeza, ni rahisi kuona kuwa Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wamejipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko Sheria za Ardhi huku, tukasome tuelewe tuwasaidie wananchi wetu ili waelewe. Sisi kama Wabunge tunaweza kuwa rahisi kuwaelekeza wananchi, kuwafundisha katika maeneo ili angalau waweze kuondoa migogoro. Hiyo itakuwa ni rahisi kuliko kulaumu kwamba Serikali haijajipanga. Serikali imejipanga, wametuletea mambo yako humu, migogoro imepangwa, Mheshimiwa Waziri ameandika nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Serikali tusaidie sasa kueleza wananchi wetu ile namna bora, maana hakuna Serikali mahali popote duniani inayoweza kufanya kazi kwa upande mmoja tu. Ni lazima upande mwingine wa sisi Wawakilishi tufanye kazi ya kuelimisha watu wetu ili migogoro hii nayo ipungue tufikie katika hali ambayo itasaidia Wizara na Serikali kwa ujumla, maana Serikali tu haiwezi kutatua migogoro kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro pia inatatuliwa na Wanasiasa ambao ni sisi wenyewe. Nasi Wanasiasa yaani Wabunge na wengine wanaotusikia wanaochaguliwa, tusaidie kuelekeza watu ili wasiwe wa kwanza kuvunja sheria. Maana tukianza kuvunja sheria, tutakuwa wa kwanza kuilaumu Serikali, kwa sababu mpaka Serikali ije inatumia muda mwingi na gharama nyingi, watu wengi wamefariki, wamepoteza maisha kwa migogoro hii ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba pia, Serikali kwa upande mwingine ijitahidi. Wakuu wa Wilaya; namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, anatatua migogoro kwa kuiona mwenyewe physically. Natoa rai yangu kwa Wakuu wa Wilaya wa maeneo mengine, Wenyeviti wa Vijiji, ni tatizo. Inafika mahali wako Matajiri wanaotaka ardhi kwa muda mwingi, lakini inafika mahali wakipewa kitu kidogo, yaani rushwa wanachanganyikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kufika mwenyewe na hadanganywi. Hadanganywi kwa sababu anaiona ile migogoro inavyokwenda, anaona jinsi ya uhaulishaji wa ardhi na wakati huo basi anafika mahali anaweza kustopisha zile ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri, lakini naomba pia, amalizie ile migogoro ambayo kimsingi iko Manyara na Mbulu. Naamini Mungu atamsaidia, atakuja tena. Najua Tanzania ni kubwa na lazima tuongee worldwide.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naipongeza Wizara, pia naunga mkono hoja hii. Nakuachia pia muda uendelee na Mungu akubariki sana. ahsante sana.