Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DKT. GODWIN A. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru kwa kupata nafasi. Kwanza nakubaliana na wenzangu wanaosema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni nami niseme tu katika migogoro ambayo nimewahi kumletea Mheshimiwa Waziri kuhusu ardhi ndani ya Wilaya yetu ya Siha, nimeeleza hata ya kufanya na kuyafuatilia na amefika katika Wilaya ya Siha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeona wanavyoshirikiana na Wizara ya Kilimo kutatua migogoro iliyoko eneo la Ushirika. Vile vile niseme kwamba leo tujielekeze zaidi wapi atakapokwenda kukwama wakati anafanya shughuli zake ili ajipange mapema zaidi na nimwombe anayemwakilisha Waziri Mkuu, ili aweze kunisikiliza kwa makini na kumfikishia ujumbe huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Wilaya ya Siha, tuna migogoro ya mipaka kati ya Arumeru na Longido, lakini sikuwepo siku mbili ,tatu hizi wananchi kati ya Arumeru na Siha wamebomoleana nyumba upande wa Arumeru wamebomoa nyumba moja lakini Siha kwa sababu Mkuu wa Wilaya kafika pale tena kafika amelewa, lakini alipofika pale ame-provoke wananchi kati ya pande zote mbili zimebomolewa nyumba nne za Arumeru, lakini ikabomolewa na ofisi ya mtendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda pale kazi ilikuwa ni rahisi, ilikuwa tu kukutanisha wananchi pande zote mbili na kuwaelewesha na kukaa chini mkondo wa sheria ufuate sehemu yake, lakini Mkuu wa Wilaya ya Siha alitaka nguvu zitumike kuliko akili. Niseme tu nimshukuru OCD Meru na Siha, lakini na Mkuu wa Wilaya ya Meru angalau anasimama kwenye nafasi yake kama tunavyotaka aende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapoongea hivi najua migogoro ambayo nimewaandikia, lakini migogoro ambayo ameandika Mkuu wa Wilaya ya Siha baada ya maagizo ya Mheshimiwa Waziri, mgogoro ambao nimekuwa nikiusisitiza kila siku, leo tunapoongea hivi matrekta mawili yamebomolewa na wananchi, nimepata meseji sasa hivi lakini gari la polisi limevunjwa kioo, huyo ndiyo Mkuu wa Wilaya tuliyenaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanasemaje? Wananchi wanasema na baadhi ya watumishi, wananchi walipoona yule mwekezaji kwenye Kata ya Songu, alipokuwa anaenda kwenye Kata ya Songu kulima hilo eneo ,wananchi walimzuia. Walipomzuia wakamtaka Mkuu wa Wilaya na uongozi wamzuie kwa sababu bado wana mgogoro, wao wanasema eneo ni lao na wenyewe wawekezaji wanasema eneo ni lao, wakataka tu kwamba azuiliwe na yeye asilime ili waendelee na mchakato wa kawaida, lakini Mkuu wa Wilaya akaagiza polisi waje wakamate watu. Polisi wakatumia nguvu nyingi wakakamata na viongozi, ndiyo yaliyofikia, hayo sasa ndiyo matatizo tuliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana nashukuru Mheshimiwa Waziri alikwenda kwenye Wilaya ya Siha, lakini nimwambie kuondoa Mkuu wa Mkoa ambaye alikwenda naye baba, wengine wote ni watuhumiwa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na hata juzi tulimuuliza amekodisha heka nyingi ambazo haziruhusiwi, tena beacon zimepimwa amewapa watu viwanja, halafu wakaenda tena kukodishwa halafu zikalimwa wakang‟oa zile beacon, anatuambia tutafute shilingi milioni mia moja kwa ajili ya kurudishia beacon, hiyo ndiyo Serikali ya Wilaya tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe na nimwombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Waziri wa Kilimo, twende ili wathibitishe ninayosema kwa maneno yao hawathubutu kumwambia ukweli. Akienda cha kwanza kiongozi akifika pale anaambiwa yule Mbunge ni mkorofi, ana fujo, lakini kiukweli mimi sina fujo wala huwa mimi siyo mkorofim isipokuwa nataka watu waende kwenye focus ambayo ndiyo tunaitaka nchi hii ifike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubaliana kwamba, tunataka kuipeleka Tanzania iwe ni nchi ya pato la kati, hamna namna yoyote tutakuwa nchi ya pato la kati na narudia tena, ni lazima kama tunajenga viwanda, basi watakaotengeneza malighafi kwa ajili ya hivyo viwanda wawe ni Watanzania wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tukatengeneza kiwanda, sawa tunakubali na mwekezaji wa kiwanda awe na sehemu ya kutafuta malighafi, lakini ili kuwapeleka nao Watanzania waweze kumiliki uchumi wa nchi yao, ni lazima nao waweze kuzalisha malighafi ambayo itatumika kwenye hivyo viwanda, ndicho tunachokisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Wilaya ya Siha, nilisema tena hapa tunaweka 130,000, hivi tungesema tunatoa eka 10,000 tunahakikisha nao watu wa Siha wanamiliki au Watanzania wanamiliki, sio lazima watu wa Siha wakamiliki zile 120,000, tukawekeza tutapunguza migogoro. Leo umeona Mheshimiwa lile shamba la maparachichi ni zuri, lakini ndani ya Wilaya ya Siha ni mojawapo ya wilaya hazina pato, inasemekana baraza lao livunjwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ukienda kwa wawekezaji wanakwambia kwanza tumechoka viongozi wako wa Wilaya sisi ndiyo tunatengeneza magari, sisi ndiyo tunawapa hela na vitu vingine, tunakuomba uende ukasema tuwe tunadaiwa kile tunachostahili, tena tupeleke kwenye maendeleo yaonekane na wananchi. Kama mimi nasema uwongo, naombeni twende tuthibitishe haya ninayosema na niko tayari kuwajibika kama nasema uwongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, tukiwamilikisha namna hiyo tutapunguza migogoro, kama mkulima mwekezaji amewekeza kwenye zao fulani, nao wakulima wakawekeza kwenye zao hilo hilo kwa kupewa ardhi, kwa sababu wanatumia soko moja na wakatumia eneo moja kuuza, urafiki utakuwepo na migogoro haitakuwepo na upendo kati ya wawekezaji na wananchi utakuwa mkubwa sana. Hicho ndicho tunachokisema, hatusemi hatutaki wawekezaji, sisi tunasema tunataka wawekezaji lakini tunataka tunapofikiria uwekezaji tufikirie sustainability ya uwekezaji wenyewe kwamba uwekezaji wenyewe utadumu vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu huyu huyu Mkuu wa Wilaya nilishawahi kumwambia, wala mimi siyo Mbunge wakati huo nilikuwa mfanyakazi wa kawaida tu. Nikamwambia migogoro wa Endarakwai ambao ameandika hapa eka 5,000 wakati ni eka 11,000, nikamwambia fanya hivi, fanya hivi, akakataa akasema yeye ni dola na hatuwezi kumfundisha. Tuliona kilichotokea, nyumba zimechomwa na mabilioni yamepatikana na ni aibu kwetu kama nchi na ni aibu kwetu kama wilaya, wawekezaji kuvamiwa halafu inarushwa nje, je, na tunataka tuwekeze, tukitaka tuwekeze wakati tunatangaza sehemu zetu za uwekezaji, watu waki-google wakiona wawekezaji wamevamiwa tunakosa uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka watu wenye hekima ambao wanajua kupeleka uwekezaji pamoja na wananchi bila kuwa na migogoro ili watu waipende nchi yetu. Nilikuwa naangalia leo hata Ujerumani wanatangaza wanaomba wawekezaji watoke nje, hata sisi tunawahitaji, lakini tunawahitaji kwa namna ambayo itamfanya Mtanzania afaidike, mwekezaji afaidike lakini na mtu ambaye anakaa katika eneo husika afaidike, ndiyo uwekezaji tunaousema. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri anaona hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie watu hao wasimkwamishe kwa sababu hapewi ukweli. Leo shamba ambalo limechomwa matrekta hajawahi kwenye ofisi yake kuambiwa, lakini siku zote tunasema kwa sababu wana maslahi. Mashamba ya ushirika alikuja Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya wananchi walimzomea kwa masuala ya ardhi, lakini kwa nini ndani ya mashamba ya ushirika ni wao wanalima wananchi hawapati mashamba? Kama nasema uwongo twendeni halafu niko tayari wala msiseme nimesema kwenye Bunge siwajibiki, niwajibike kama nasema uwongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe hili limfikie Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, sisi tunapenda hiyo nafasi ya Ukuu wa Wilaya, lakini huyo ambaye anakaa mpaka saa nane bar, dereva anakaa kwenye gari na gari la Serikali la kodi ya wananchi, sisi tumechoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaki mtu anayesababisha Serikali idharauliwe, tunataka Serikali ya Tanzania iheshimike, watu waheshimu Serikali ya Tanzania. Unapokwenda kwa wawekezaji Mkuu wa Wilaya mzima unaongoza Serikali halafu unapewa vitu vidogo vidogo unaidhalilisha Serikali yetu na hatutakuwa tayari. Nilimwambia Mkuu wa Mkoa, huyu Mkuu wa Wilaya anatusumbua na tukamweleza, nikamwambia nitakuja kuomba hapa ahamishwe ikishindikana wananchi wa Siha hatupo tayari Serikali ya Tanzania kuaibishwa, tutamtoa wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kwa sababu anatudhalilisha, anafanya vitu ambavyo ukienda kwa mzungu akikuona mweusi anakudharau, hatuko tayari. Kwa hiyo, niseme bila kuathiri juhudi nzuri zinazo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naomba kuwasilisha.