Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwasilisha mpango na bajeti ya mwaka 2016/2017. Sekta hii ni muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu, ardhi ni msingi wa shughuli zote za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu migogoro ya ardhi. Narejea Jimbo langu la Muleba Kaskazini, tunayo migogoro mikuu miwili katika Kata za Mayombwe na Muhutire kati ya wananchi na kambi ya Jeshi la Wananchi Kaboya. Jeshi la Wananchi kwa maslahi ya Taifa waliamua kuongeza ukubwa wa eneo lao. Mgogoro huu umepitia ngazi zote za uongozi wa nchi ukiondoa mahakama. Uamuzi wa Wizara ya Ardhi na ile ya Ulinzi kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Kikwete na Rais wa Awamu ya Tano ni kuwa Serikali iwalipe fidia wananchi wa maeneo yote yatakayotwaliwa, lakini mpaka sasa fidia haijalipwa na wananchi wamezuiwa kuendeleza maeneo yao kwa miaka sasa. Katika mwaka 2016/2017, Wizara ya Ardhi ibebe jukumu la uongozi na kumaliza mgogoro huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa pili ni katika Kata ya Rutoro. Eneo hili kampuni ya NARCO iligawa vitalu vya ufugaji kwa wawekezaji kwa kuwapatia wawekezaji hao maeneo ambayo tayari vilikuwepo vijiji tena vinavyotambuliwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limeanza tangu miaka ya 2005, Kamati nyingi zimeundwa kutatua tatizo hili, zilileta mapendekezo bila utekelezaji. Moja ya Kamati iliyotoa mapendekezo yaliyolenga kuleta suluhu ni Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara sita iliyoteuliwa na Mheshimiwa John Pombe Magufuli, wakati huo alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Kamati za Bunge mara mbili zimefanyia kazi suala hili na kutoa mapendekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Kikwete wa Awamu ya Nne aliamua kutwaa hati ya NARCO inayohusu eneo la Kata ya Rutoro, iliagizwa eneo hilo ligawiwe upya kwa kubainisha eneo la vijiji na lile la wafugaji. Uongozi wa Mkoa umejaribu kutoa mapendekezo namna ya kutatua mgogoro huo kwa kuazima mapendekezo ya Kamati mbalimbali nilizozitaja hapo juu. Nakubaliana na mapendekezo hayo kwa asilimia 49, sikubaliani na mpango huo pale unapotaka kurudia makosa ya kutoa maeneo kwa watu ambao si raia wa nchi hii na pale wanaposhindwa kutambua kuwa wananchi wa Rutoro ni wakulima na wafugaji. Mgogoro huu hapa ulipofikia ni rahisi sana kuutatua, tuwe objective bila kupendelea upande wowote, tulenge maslahi ya Taifa, tumalize mgogoro huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.