Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Savelina Slivanus Mwijage

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuweza kurudi ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakishukuru Chama change, Chama cha Wananchi CUF kuweza
kuniamini na kunirudisha hapa Bungeni. (Makofi)
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, namtaka Waziri wa Mawasiliano, kesho atuletee majibu hapa ni kwa nini wamezuia TV kuonesha Bunge. (Makofi)
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia hotuba ya Rais, watu wengi hapa wanabeza mchango wa Wabunge kuhusu Zanzibar. Tukumbuke kipindi cha nyuma Zanzibar ilivyokuwa na vurugu leo hii badala ya kuomba Mwenyezi Mungu kuepusha balaa la siku za nyuma tunaendelea kubeza na Wazanzibari wenyewe wanajua matatizo yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusiendelee kubeza mambo ya kisiasa, tusije humu kuwasafisha au kuwapongeza watu kwa mambo ya kutuletea matatizo kama yaliyotokea siku za nyuma. Watu walikufa na walipoteza mali zao nyingi. Kwa hiyo, nawaomba tushirikiane kupiga magoti kumrudia Mwenyezi Mungu tuweze kuiombea Zanzibar iweze kuwa na amani.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Marais wengi wanavyoingia kwenye kampeni wanawalaghai watu wa Kanda ya Ziwa, nitaanza na usafiri wa majini. Wakati wa uhuru mwaka 1961, wakazi wa Mkoa wa Kagera na Kanda ya Ziwa tulikuwa na chombo cha usafiri kinachoitwa MV Victoria,
MV Kabilondo, MV Usoga na MV Serengeti. Kila Rais kuanzia Rais Mkapa walisema wataleta meli mpya, meli za kusafirisha mizigo na ya kusafirisha Watanzania amekuja Jakaya hivyohivyo, amekuja Magufuli hivyohivyo. Tunaomba msiwe mnalaghai kwa kuahidi kitu ambacho
hamtaweza kukifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naelekea kwenye huduma ya afya. Mkoa wa Kagera una zaidi ya watu milioni 2.8. Hivi sasa Serikali ya Mkoa wa Kagera inamiliki hospitali tatu na vituo vya afya 25, zahanati 207, mashirika ya dini yanaongoza kwa kutoa huduma ya hospitali ili kuwasaidia wananchi. Serikali inajivunia hizo hospitali kwamba ni za Serikali. Hospitali ya Rubya, Isingilo - Nyakanga, Bugeni ni za dini. Tunaomba kuanzia sasa na wakati huu wa Magufuli, Hospitali ya Mkoa wa Kagera ipatiwe CT-Scan na Madaktari Bingwa kwa sababu haina Daktari
Bingwa wala vifaa. Leo hii anasema ataboresha hospitali, aboreshe kwanza vifaa ndiyo ajenge hiyo Hospitali ya Mkoa na Wilaya anayotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye kilimo. Mkoa wa Kagera tuna zao la kilimo cha migomba. Mgomba ndiyo zao kuu la biashara na zao la chakula. Ilitolewa taarifa kwamba zao hilo lina ugonjwa unaitwa mnyauko. Mpaka sasa hivi wananchi wa Mkoa wa Kagera wana njaa kubwa sana kutokana na ugonjwa huu wa migomba lakini Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia kuwapelekea wataalamu ili kutibu ugonjwa huo ili waendelee kulima migomba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1952, Serikali ya Kikoloni iliweka sheria ya kuwazuia kulima migomba bila kuweka mbolea ya chengachenga. Mwaka 2006 katika Kata ya Izigo, Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera ndiyo waliotangulia kupata ugonjwa huo wa mnyauko
ukitokea nchi ya jirani Uganda sasa hivi umeenea Mkoa mzima wa Kagera na watu wanalia na njaa. Kipindi kilichopita mkungu mmoja ilikuwa Sh.3,000, Sh.5,000 sasa hivi umefika Sh.16,000 mpaka Sh.30,000. Naiomba Serikali inayosema Kilimo Kwanza ianze kwanza kuwaboreshea wakulima wa Mkoa wa Kagera kwa kuwaletea wataalamu kuboresha zao hilo ili waweze kupata kipato cha kuuza ndizi Uganda na nchi nyingine jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naharakisha ili muda wangu usiishe, naenda kwenye elimu, wanasema elimu ni bure. Ukiangalia elimu ni bure lakini Mwalimu anayekwenda kufundisha elimu bure analala wapi? Darasani watoto wamejazana hawana mahali pa kukaa atapaje akili
ya kuweza kushinda darasa la saba au form four. Kwanza, boresha shule zilizopo, Walimu wapate sehemu ya kulala, tupate maabara za shule, wanafunzi wapate mahali pa kukaa na kusoma vizuri na Walimu wafundishe vizuri. Mwalimu hawezi kuacha mtoto ndani ya familia
anakosa chakula akapata akili ya kumfundisha shuleni na anafika darasani mtoto anasinzia kwa ajili ya kukosa chakula. Kwanza, tuboreshe kitu kilichopo ndiyo baadaye tuje kusema watoto wanasoma bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona fomu ya watoto wanaoingia form one, ukiangalia michango wanayoitoa ni mingi sana. Kama Serikali imekuwa tayari kuwasaidia wanafunzi ili wasome bure waanze kwenye chakula. Mtoto akiingia darasani ana njaa atashindwa kuendelea kusoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, watumishi walioajiriwa wanakaa katika Halmashauri miaka zaidi ya thelathini wanafanya kazi kwa mazoea. Juzi hapa mimi na Mheshimiwa Lwakatare tumekwenda kutoa misaada katika zahanati ambazo wanawake wanajifungua, kwa moyo safi tu lakini akatokea DMO akasema hospitali zote hazina shida ya beseni na unaangalia kila mwanamke anabeba beseni wakati huo unaona Wabunge wengine wa CCM wanatoa misaada inapokelewa. Hii ni kutokana na kufanya kazi kwa mazoea kwa miaka 30 yuko kwenye Halmashauri moja habadilishwi. Tunaiomba Serikali mfanyakazi yeyote akikaa miaka mitano inatosha ahamishiwe kwenda sehemu nyingine, siyo kufanya kazi kwa mazoea inaonekana pale ni nyumbani na anachokifanya anaamua mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye ajira, vijana wamejiajiri kwenye pikipiki lakini wananyanyasika, wanapigwa, wananyang‟anywa pikipiki na Maaskari halafu wanaziuza na hili tumeshuhudia. Kama kijana huyo hana elimu ya kuendesha pikipiki anaendesha kwa ajili ya
njaa na kutafuta ajira ya kulazimisha. Naiomba Serikali itoe elimu kwa vijana ambao wanaendesha bodaboda ili waweze kupata kipato chao kwa sababu ajira Serikalini hamna, inasema ajira, ajira, lakini ajira haipatikani. Kama hatuna viwanda, kama hatuna masoko makubwa, hakuna ajira yoyote vijana wataendelea kupigwa na Maaskari.
Mheshimiwa Naibu Spika…
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)