Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia Wizara hii ya Ardhi katika Jimbo langu la Kibiti. Kwanza napenda kuipongeza Wizara hii kwa ujumla pamoja na Waziri mwenye dhamana baba yangu Mheshimiwa William Lukuvi kwa anavyochapa kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi ni Wizara mtambuka kwani ardhi ni muhimu sana katika shughuli za kila siku za mwanadamu. Hatuwezi kujenga viwanda bila ya kutenga ardhi ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kibiti lina ardhi ya kutosha lakini naiomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kutoa msisitizo kwa watendaji wetu wa Halmashauri kuwajibika katika shughuli zao za kujenga Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Baraza la Ardhi na Mahakama ya Ardhi; Baraza la Ardhi katika maeneo yetu tunapoishi ni muhimu sana, kama Baraza la Ardhi la Kata. Napenda kuishauri Serikali yangu sikivu itoe semina elekezi ya Baraza hili la Ardhi ili liipe uwezo wa ufahamu katika shughuli zake za kutatua migogoro ya ardhi katika kata zetu. Mahakama ya Ardhi nayo iwe inatoa lakini kwa muda mfupi; hii itachangia kupunguza dhana potovu ya rushwa kwa wananchi wenye migogoro katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa hati za kimila katika Jimbo langu la Kibiti bado ni tatizo, naomba Wizara yenye dhamana ambayo inaongozwa na Waziri wetu mchapakazi na mwenye weledi mkubwa, Mheshimiwa Willium Lukuvi ahakikishe Jimbo langu la Kibiti sasa wananchi wanapata hati za kimila kama kauli yake Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi katika Jimbo la Kibiti ipo migogoro kadhaa ambayo inahitajika kupatiwa utatuzi kama kata ya Mlanzi na Mahenge. Maeneo mengine ni ya Kibiti na Bumba Msoro; mgogoro wa mpaka kati ya kijiji cha Msafiri, Nyambili, Uponda na maeneo mengine. Katika Jimbo langu pia ipo migogoro ya wakulima na wafugaji. Hii inatokana na kutopanga matumizi bora ya ardhi kama kutenga maeneo ya kilimo, ufugaji, benki ya ardhi pamoja na maeneo ya kujenga viwanda. Migogoro hiyo ipo kata ya Matunda na maeneo mengine. Hapa jimboni kwangu kuna watu wasiojulikana wamechukua maeneo ya Nyatanga, Nyale, Ngambuni, Kisima, Nananyumbani, wananyanyasa wananchi wangu wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumuuliza swali Waziri mwenye dhamana, kwa nini hadi leo Songa hawajapata kijiji ikiwa vigezo vyote vya kupata kijiji cha Songa umekamilika lakini hadi leo Serikali bado haijakitangaza kijiji hicho cha Songa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto katika Idara ya Ardhi Jimboni kwangu Kibiti ni kutokuwa na vitendea kazi vya kisasa ili kuhakikisha wanapima kwa haraka, usafiri wa uhakika, Afisa Ardhi Mteule, fedha ndogo inayotokana na kodi ni vizuri ingebaki asilimia 50 badala ya asilimia 30 ya sasa. Kuongeza watumishi, kwa sasa wapo wachache, kuwalipa posho za kujikimu kwa wakati, kuwalipa posho za masaa ya ziada na hili inatokana na upungufu wa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji tunawapenda na tunawahitaji katika Jimbo letu la Kibiti; lakini angalizo langu ni kwamba hawa wawekezaji wasipewe ardhi kwa kulipia fidia badala yake wafanye kama ifuatavyo:-
(i) Wanakijiji watoe ardhi na wawekezaji watoe mtaji ili pande zote mbili wawe wamiliki wa kiwanda hicho husika, hii itasaidia kutatua migogoro na dhana potovu ya mwekezaji kuwa kama mnyonyaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na taasisi za fedha, napenda kusema Waziri mwenye dhamana atoe tamko maalum juu ya kuzitaka taasisi za fedha zote hapa nchini kutambua hati miliki za kimila nazo ni dhamana ya wananchi kupata mikopo katika taasisi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja mia kwa mia, Hapa Kazi Tu.