Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Gibson Blasius Meiseyeki

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja ya Wizara ya Ardhi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Waziri Mheshimiwa William Lukuvi kwa kuchaguliwa tena kuongoza Wizara hii, hakika anaweza. Nampongeza pia na kumshukuru kwa ziara aliyoifanya Jimboni kwetu kwani ilitupa mwanga wa utatuzi wa migogoro mingi ya ardhi iliyotuzunguka. Bado tunamhitaji Mheshimiwa Waziri Arumeru ili tuweze kumaliza kabisa changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya sababu ambazo zinasababisha migogoro ni Serikali kuwapa wawekezaji maeneo makubwa mno kuliko uwezo wao na kuyaendeleza. Hii hupelekea wawekezaji kufanya biashara kukodisha ama kugawia wananchi mashamba hayo ambayo baadaye hushindwa kuwaondoa pindi wanavyotaka kufanya shughuli nyingine katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo kama haya hasa katika shamba ya Fill Estate na Tanzania Plantation yote katika Jimbo la Arumeru Magharibi, Kata ya Bwawani. Wananchi wameumizana sana na vyombo vya dola na zaidi ya watu 11 wapo rumande kwa miezi miwili sasa kwa kubambikiziwa kesi ya wizi wa kutumia silaha eti kwa sababu tu wanagombania shamba na askari polisi ambao wawekezaji wakawakodisha katika shamba ambalo wananchi tayari walikuwepo kwa lengo la kuwatoa kwa nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Arumeru karibu sasa yote inakuwa mji, hivyo mashamba mengi ya wawekezaji yamemezwa na idadi kubwa ya wananchi wanaoongezeka kila kukicha na hivyo mashamba haya yanalimwa mjini na bado hayajaendelezwa vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali huchukua muda mrefu sana kubatilisha haki za umiliki za wawekezaji zilizopita muda wake na kupelekea wananchi kuvamia mashamba hayo na kuanza kujigawia. Serikali sasa ichukue hatua madhubuti kutengua hati za ardhi ambazo muda wake umeisha. Hii ni pamoja na kuwatafutia maeneo mengine wawekezaji ambao mashamba yao yameingia ndani ya miji kuepusha migongano zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu linaelekea pabaya hasa jinsi suala la migogoro ya ardhi inavyoshughulikiwa, Taifa linaelekea Zimbabwe. Kwa Mkoa wetu wa Arumeru hali siyo shwari kwa wawekezaji na hivyo wapo kwenye hofu kubwa sasa, wananchi kila wanapoona shamba kubwa basi hulazimisha wanasiasa kufanya liwezekanalo ili wanyang‟anywe na wapewe wao, jambo ambalo siyo zuri kwa ustawi wa Taifa letu ambalo bado linahitaji wawekezaji kwa ustawi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kwa Serikali, hasa kwa Mkoa wa Arusha kuboreshewa miundombinu inayounganisha mikoa mingine hasa Manyara, Wilaya ya Simanjiro ili kuwaunganisha wananchi hawa na maeneo hayo ambayo bado ardhi ni virgin. Mashamba yaliyo mjini na muda wake umekaribia kwisha, Serikali iyatwae na kufanya mipango mipya ya ardhi/mashamba hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wanasiasa siyo rahisi kutoa elimu ambazo siyo rafiki kwa wananchi kuhusu umiliki wa mipango ardhi, Serikali kwa kutumia vyombo vyake, elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi kuhusu sera za ardhi na umiliki mashamba ili wananchi waache tabia ya kuvamia mashamba ambayo nyaraka zake ziko thabiti/genuine ili kuhakikisha kwamba wawekezaji ambao Serikali inahangaika kuwaalika wanakuwa salama na wanafanya kazi zao kwa amani na utulivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninamwalika tena Mheshimiwa Waziri Jimboni Arumeru Magharibi ili tumalizie migogoro iliyopo once and for all. Ahsante sana, naomba kuwasilisha.