Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie Wizara hii. Kabla sijafanya hivyo nimshukuru sana Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kusimama tena hapa na kuchangia Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyoanza walionitangulia naomba nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake ya Maliasili na Utalii kwanza kwa kutuletea hotuba hii nzuri, detailed na imegusa kila sekta kwenye Wizara yake. Naomba vilevile niwapongeze sana Wajumbe wa Kamati inayosimamia Wizara hii nao kwa hotuba yao nzuri ambayo imetoa maoni na ushauri ambayo kwa kweli yanatusaidia sisi tunaochangia kuweza kujua maeneo gani yatafanyiwa kazi na Kamati iliona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu tumemwona Mheshimiwa Waziri anavyohangaika na kupambana na ujangili nchini. Waziri na Wizara imeonyesha nguvu yake yote kwenye jambo hili. Nataka niwatie moyo kupitia mchango wangu huu kwamba kazi wanayoifanya ni kwa faida ya nchi, waendelee mbele na wasivunjike moyo. Tumeona wale majangili wote waliotungua ndege wamekwishakamatwa. Juzi niliona video moja kwenye mitandao ya kijamii maaskari wetu wamekamata majangili haya yaliyokuwa yanafanya kazi ya kuua wanyama wetu. Naomba niwatie moyo na kuwaombea kwa Mungu waendelee bila shaka wanyama hawa ni kwa faida ya nchi yetu na vizazi vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bukombe asilimia 40 ya ardhi ya Bukombe ambayo ni kilometa za mraba 8,055.59 ni hifadhi. Wananchi wanaoishi Bukombe wana maingiliano ya karibu na hifadhi ya Kigosi Moyowosi lakini mahusiano ya Kigosi Moyowosi hayajawahi kuwapatia faida na hapa nataka niseme kwa uchungu kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walio wengi wa Wilaya ya Bukombe wana majonzi makubwa na hifadhi hii. Nimesimama hapa kumwomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama na kuhitimisha aje na majibu ambayo yatawapa tumaini watu wa Bukombe juu ya mahusiano mabaya ya Wahifadhi na wananchi wa Wilaya ya Bukombe. Nenda Ngara, nenda Biharamulo, njoo Bukombe, pita Mbogwe, nenda Kahama, nenda Ushetu kwa jirani yangu Kwandikwa kila Mbunge aliyemo humu ambaye anawakilisha maeneo haya hana habari njema ya kuelezea juu ya mahusiano ya Maliasili pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako manyanyaso makubwa ambayo yamefanyika ukiambiwa hapa unaweza ukatokwa na machozi. Leo nataka niyazungumze haya na niseme hadharani ikiwa sitapata majibu, watu wa Bukombe watanishangaa kuunga mkono bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, Kitongoji cha Idoselo kilichoko kwenye Kijiji cha Nampalahala, watu wa Maliasili wameingia hapo, wamechoma moto nyumba za wananchi 40, kijiji ambacho kina GN ya Serikali kwa maana hiyo kimetambuliwa na Serikali! Katika kijiji hicho tumefanya uandikishaji wa BVR, kampeni tumepiga kule, walishachagua Mwenyekiti wa Kijiji, kilishasajiliwa, kina GN ya Serikali, watu wametoka nyumbani wamekula chai wameshiba vizuri, wana magari na mafuta ya Serikali, wana kiberiti na bunduki, wanaenda kuchoma nyumba za wanachi ambao hawana uwezo wa kujitetea, wamepiga na wameharibu mazao ya watu, watu hao wapo wanaendelea kutamba na kusema kwamba mtatufanya nini. Jambo hili lisipopata majibu leo namwambia Mheshimiwa Waziri hapa hapa nakufa na yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani wananchi wale ambao wamelima mashamba yao, mazao yao yamekua yamefikia mahali fulani wanatumaini kwamba baada ya miezi fulani tunakwenda kuvuna tulishe familia zetu, tusomeshe watoto wetu, ananyanyuka mtu mmoja tu au wawili kwa sababu wana nembo ya Serikali kwa maana ya Maliasili wanakwenda kuchoma nyumba zao na baadaye wanatamba kwenye vyombo vya habari tumechoma vibanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie ikiwa wao wana maghorofa, hivyo vibanda vya wananchi wao ni maghorofa yao. Ikiwa wao wanakula vizuri hayo waliyosema ni vi-plot wao ndiyo mashamba yao ambayo yanalisha familia zao. Lazima nipate majibu kwenye Bunge hili, lazima wananchi wa Bukombe wafutwe machozi kwa jambo la ukaidi, kwa jambo hili kubwa lililofanyika Wilaya ya Bukombe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bukombe pamoja na mambo haya, kuna manyanyaso makubwa yamefanyika. Wako wananchi wamevunjwa miguu, wako wananchi wamevunjwa mikono, wako wananchi wamefanywa kuwa walemavu wa kudumu, walikuwa wanalima kwa ajili ya familia zao, leo watu hawa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu wamekuwa walemavu, aliyefanya ni nani? Baadhi ya Askari wasio waaminifu wa Maliasili wamewaumiza watu hawa. Nataka majibu wananchi hawa mnawafanyia nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii imepiga risasi ng‟ombe za wananchi, nataka majibu ni kwa nini. Ng‟ombe waliopigwa risasi ni wa Ndugu Masanja Njalikila, ng‟ombe sitini (60); Ndugu Hamisi Ngimbagu, ng‟ombe wanane (8); Ndugu Manzagata Mang‟omb,e ng‟ombe mmoja (1); Ndugu Fikiri Masesa, ng‟ombe wawili (2); Ndugu Sikujua Majaliwa, ng‟ombe kumi na nane (18); Ndugu Blashi Ng‟wanadotto, ng‟ombe arobaini na tatu (43); Ndugu Juma Masong‟we, ng‟ombe kumi na mbili (12); Ndugu Mussa Seni, ng‟ombe wawili (2); Ndugu Serikali Andrea, ng‟ombe wawili (2); Ndugu Juma Langa, ng‟ombe kumi na nane (18) na Ndugu John Mashamba, ng‟ombe wawili (2); jumla ng‟ombe 215. Ndugu Jofrey Omboko punda wake wane (4) wamepigwa risasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa leo nataka majibu hatma ya watu hawa inapatikanaje. Kama inabidi nisimame kwenye Bunge hili nilie machozi kwa ajili ya wana Bukombe nitafanya hivyo, lakini watu wangu wapate majibu. Haiwezekani niwepo Mbunge hapa nimekaa kwenye kiti hiki cha kuzunguka, wananchi wangu wana mateso na nijione Mbunge mwenye furaha, hilo sitafanya. Naomba nipatiwe majibu, vinginevyo sitaunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine limetokea na hili ni la kisheria na naunga mkono usimamiaji na utii wa sheria. Iko tabia ya watu kupewa adhabu ya kutaifishwa mifugo yao. Leo ninavyosimama hapa jumla ya ng‟ombe 603 za wananchi wa Bukombe wametaifishwa, wamechukuliwa kuanzia siku ile ni mali ya Serikali. Nataka niseme kwenye kundi la wale waliopelekwa Mahakamani wenye ng‟ombe walikuwa watano (5), watatu (3) walikubali kutoa fedha, wakapelekwa Mahakamani wakadanganywa kwamba wakiwa huko wataachiwa Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme fedha zao wamekula na ng‟ombe zao zimetaifishwa lakini wako wawili (2) waliokataa kutoa fedha kujumuishwa tu kwenye mashtaka yale wakati wanadai ng‟ombe wao Maliasili wamekataa kuwaweka. Wamekwenda kuhukumiwa wale ng‟ombe kama ng‟ombe wasiokuwa na mwenyewe. Watu hawa wamekwenda Polisi, wameripoti Maliasili wakawaambia tunaomba mtufanyie jambo moja mtuingize kwenye mashtaka na sisi tushtakiwe wamekataa kuwapeleka wanasema hawa ng‟ombe hawana mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unyanyasaji huu una-turnish image ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Unyanyasaji huu hauwezi kumfanya Mbunge wa Bukombe afurahie Wizara ya Maliasili na utalii. By the way kwenye Sheria zao za Maliasili na Utalii sisi tunaopakana na hifadhi tunapaswa kupata asilimia 25% ya mapato yale. Toka nimekuwa Bukombe pale sijawahi kuona hata shilingi moja inapelekwa Bukombe. Naomba na hiyo hela Mheshimiwa Waziri na yenyewe aniambie naipataje kwenye Halmashauri yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na naomba niseme ahsante sana.