Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kulipongeza Shirika la Hifadhi la TANAPA na Ngorongoro kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhifadhi rasilimali hapa Tanzania. Imekuwa ni kawaida pale ambapo Serikali inashindwa kuhifadhi maeneo mbalimbali kimbilio lake ni shirika lake ambalo linawapelekea na kwa kiasi kikubwa kwa kweli wameonekana wanajitahidi sana kulinda rasilimali zetu na vituo vyetu hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo tetesi kwamba Serikali inataka kuhodhi mashirika haya, kuyarudisha mikononi mwake kwa hili napinga kwa asilimia zote. Kama ni kweli kwamba ziko taarifa Serikali inataka kuhodhi mashirika haya irudishe kwenye mikono yake, wawe wanaendesha wao ni uhakika kabisa kwamba tunakwenda kuua uhifadhi hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mashirika mengi hapa nchini yalikufa kwa sababu Serikali imeshindwa kuyasimamia. Yale machache ambayo iliamua kuyapa full authority yajiendeshe yenyewe ndiyo bado yapo. Leo TANAPA na Ngorongoro wanajiendesha wenyewe kwa asilimia 100 na bado wanapeleka ruzuku Serikalini na ni mashirika pekee ambayo Serikali haiweki ruzuku hata senti moja. Leo kama wanataka kuyarudisha ndani ya mikono yao tunakwenda kuua uhifadhi hapa nchini. Naomba kama mpango huo upo ufe kabisa haufai kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana pekee TANAPA imetoa shilingi bilioni 10 kama ruzuku Serikalini na bado inajiendesha. Tumekuwa tunalia kilio hapa kwamba Serikali ijenge angalau miundombinu ya kwenda kwenye vivutio, barabara kutoka Iringa kwenda Ruaha kwa miaka 10 Serikali imeshindwa kujenga, leo tunanyang‟anya mashirika haya mamlaka ya kujisimamia tunakwenda kuua uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa nimeona tunayo mapori ya akiba zaidi ya 28, tunayo mapori tengefu zaidi ya 42, tunazo hizi hifadhi za TANAPA 16. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri haya mapori ya akiba 28 na mapori tengefu 42, mengi yapo taabani na mengine hayapo, yapo kwenye vitabu kwenye ground hayapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapori haya yana hali mbaya, tumekuwa tunalia hapa, mapori haya mengine yamevamiwa miaka 35 iliyopita huko nyuma na wamejenga ndani ya hifadhi vijiji, hospitali na barabara. Tumekuwa tunalia hapa mapori haya yalivamiwa miaka mingi iliyopita Serikali haikuchukua hatua, wamesajili vijiji kisheria, wanapeleka huduma, leo Mheshimiwa Waziri anatuambia tuna mapori ya akiba 28, yako kwenye hali mbaya, mengine hayapo katika ground, yapo kwenye karatasi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora peke yake tuna vijiji zaidi ya 50 ndani ya hifadhi vina vyeti vya usajili na kila kitu kipo mfano shule na hospitali. Ninayo taarifa hapa kamili ya Kiserikali, Mkoa wa Tabora wenyewe vijiji zaidi ya 50, Wilaya ya Kaliua peke yake tuna vijiji 21 vimesajiliwa kisheria ndani ya hifadhi. Wananchi hawa wamekaa kwa hofu miaka mingi, Serikali tunaiambia hapa miaka 10, lakini hakuna hatua inayochukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea hatua ya leo Mheshimiwa Waziri angekuja na mpango kamili namna gani watu hawa wanashughulikiwa ili waache kuishi kwa hofu, waache kunyanyaswa, wanauliwa mifugo yao, wanaharibiwa mashamba yao, ni shida, ni matatizo makubwa. Watu wa hifadhi wanachokifanya kwa watu ambao wamesajiliwa kisheria siyo halali ndani ya nchi ambayo tunaishi kwa kufuata Katiba na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu naomba nitaje tu kwa ufupi vijiji ambavyo vimeathirika na suala hili. Tuna Vijiji vya Ukumbi Kakonko, Lumbe, Usinga, Ukumbi Siganga, Kombe, Kashishi, Uyowa, Seleli, Nyasa, Mwendakulima, Sasu, Kiwakonko, Nsimbo, Mpanda Mlowoka, Mwahalaja, Chemkeni, Kanoge, Ulanga, Mwendakulima, vijiji 21 miaka yote watu wanaishi kwa hofu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hapa atueleze nini hatma ya watu hawa na nini hatma ya shule ambazo zimejengwa kule? Hatuwezi kuacha wananchi waendelee kuishi kwa hofu miaka yote, wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo, lakini Serikali ipo tu imetulia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala la TFS. Tulianzisha Wakala wa Misitu (TFS) kwa maana ya kuokoa rasilimali ya misitu inayopotea na ndiyo lengo letu kama Watanzania, Wizara na Wabunge. Watu wa TFS wamekuwa ndiyo chanzo kikubwa cha kuangamiza misitu kuliko tulivyokuwa mwanzoni. Leo watu wa TFS hawana mpango wowote makini wa kuja kuokoa misitu, wao wanakaa wanasubiri wachukue mbao, wagonge muhuri mbao isafirishwe. Serikali imeweka utaratibu, imefunga kabisa kutoa magogo kwenye miti ya asili pamoja na mbao kutoka kwenye misitu ya asili. Kwa nini Serikali inaweka malengo kwenye TFS? Kwa nini Maafisa Misitu wanapewa malengo ya makusanyo? Leo misitu yetu inateketea kwa kasi kubwa ya ajabu kuliko ilivyokuwa TFS haipo. Labda hawakupewa malengo, labda Serikali haikuwa na mipango, labda hawajaambiwa wanatakiwa wafanye nini. Hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chain saws zilizopo ndani ya maeneo ya misitu ya asili nyingi ni za watu wa TFS. Wao ndiyo wananunua chain saws wanawapa watu wao wanaenda kuweka kule kwenye misitu, kwa hiyo, hakuna tunachokifanya. Naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa kuhitimisha atuambie nini hasa kazi na wajibu wa TFS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TFS walikuja Kaliua, wamekuja kufyeka mahindi ya wananchi kwenye Jimbo langu, tena leo naomba njaa ikija, muwe wa kwanza kuja kuwalisha chakula wananchi wa Kaliua. Mahindi yalishafikia karibu kuzaa, wanakuja wanaweka beacon ndani ya nyumba za watu. Nimeongea nao kwenye simu hamfanyi kazi kwa weledi? Hamna mpango shirikishi, Wilaya haijui, Mbunge hajui, Mkurugenzi hajui, wanakuja wenyewe wanakwenda kufyeka mahindi ya watu, hawana weledi wa kufanya kazi. Naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa atujibu nini kazi ya TFS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ikija hapa itujibu, kuna Tume ya Kimahakama iliundwa na Mheshimiwa Rais wa awamu iliyopita, kutokana na ripoti ya Operesheni Tokomeza kwenda kuangalia madhara makubwa waliyopata wananchi nchi nzima, leo ni mwaka wa tatu iko wapi ripoti ile? Iko wapi? Wananchi wanateseka, watu waliuawa, watoto wananyanyasika, mifugo iliteketea, operesheni tokomeza ilikuwa ya kutokomeza watu. Tunaitaka ripoti ya Mheshimiwa Rais hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge lako liagize tupate ripoti ya Tume ya Kimahakama ya Mheshimiwa Rais ili tuweze kuangalia namna gani ya kuwasaidia wale watu waliopata madhara makubwa sana na wengine walipoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni tozo kwenye hoteli za kitalii ambazo ziko ndani ya hifadhi. Kwa miaka mingi tumekuwa tunazungumzia suala hili la tozo. Tozo zinazotozwa sasa hivi na TANAPA ni za miaka 10 iliyopita wakati vitanda vikiwa vinatozwa dola 50 - 100, leo kitanda kimoja dola 300 - 500, tozo ni zile zile huu ni wizi, haiwezekani! Kwa nini concession fee iwe ya miaka 10 iliyopita? Leo maisha yamepanda, gharama zimepanda, vitu vyote vimepanda Serikali imenyamaza kimya kuna nini hapa? Naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie, Mahakama imeshatoa rulings wale wafanyabiashara walishindwa kwa nini hatuletewi tozo nyingine zinazoendana na hali ya sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.