Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kutoa mchango kwenye hoja hii iliyoko mbele ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri inaonesha kwamba Wizara yake au sekta ya utalii inaingiza asilimia 25 ya fedha zote za kigeni katika Taifa hili, kwa hivyo ni sekta nyeji. GDP - Pato la Taifa katika utalii, na hii ni zaidi ya miaka mitatu iliyopita tunataka atupe takwimu za sasa, ni asilimia 17.5, ya leo ikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Tanzania ni ya pili kwa vivutio vya utalii duniani baada ya Brazil. Tumekaa na sekta ya utalii wakati Mheshimiwa Chenge akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, tukafanya michanganuo mingi na tukatoa ushauri kwa Serikali namna bora ya kuweza kuweka mazingira mazuri na rafiki na yenye kuvutia ili tuweze tukaingia kwenye ushindani hasa wa soko la utalii duniani. Ukizungumzia Serengeti, ina kilometa za mraba zaidi ya 14,000 tukishindana na Masai Mara ambayo ina kilometa za mraba 1,400, ukizungumzia Mlima Kilimanjaro, ukizungumzia Ukanda wa Bahari ya Hindi kilometa 1,424, unataja vingi tu lakini Tanzania inashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133 kwenye mazingira rafiki na mapato katika sekta ya utalii, huu ni uendawazimu, yaani kwenye mtu mwenye akili nzuri unaona kabisa hatuko serious. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka na wewe Mwenyekiti tulikuwa pamoja kwenye Kamati ya Chenge One kuhusu sekta ya utalii wakati tunatafuta vyanzo vipya vya mapato. Leo hii kulikoni sekta hii, nimesoma hotuba ya Waziri, TANAPA mchango wake kwenye maendeleo ya jamii ni one billion, wakati ukiangalia kwa mfano Mlima Kilimanjaro peke yake mapato yake ni zaidi ya bilioni 60 kwa mwaka ambayo ni asilimia 34 ya mapato yote ya sekta ya utalii. Lakini ukiangalia mazingira yanayozunguka Mlima Kilimanjaro, likiwepo Jimbo la Vunjo, hali ya vijiji ambavyo viko karibu na mlima huo hali yake ni hoi bin taabani. (Makofi)
Leo hii Mbunge unaambiwa uchangie kujenga shule, changia madawati, changia huduma sijui za nini hii haiwezekani wakati vivutio tunavyo, fedha zipo. Hii ni Serikali naamini ni endelevu ya chama hicho hicho. Serikali iliyopita Waziri mwenye dhamana alikubali kwenye Bunge hili kwamba angalau asilimia 25 ya mapato yanayotokana na hifadhi hizi yaweze kuhudumia maeneo ambayo yako karibu na hifadhi hizi, ambapo ukiwa karibu na waridi unanukia waridi. Sasa leo hii ukiangalia maeneo haya yako hoi bin taabani lakini mapato haya je, leo hii Wizara yake inaendeleza ile sera ambayo ndiyo nilikuwa nataka iwe endelevu katika kuhakikisha tunapata mapato au laa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri inajichanganya, ukisoma ukurasa wa 87 unasema mwaka 2014 walipata bilioni nne kutokana na kodi ya vitanda kwa watalii ambayo ni dola moja na nusu kwa kila kitanda kwa usiku. Ukisoma ukurasa wa 127 mwaka 2014 watalii waliolala watalii hotelini ni 1054 na wastani wa kukaa hotelini siku kumi, ukizidisha unapata zaidi ya shilingi bilioni 31 na sio bilioni nne ambazo zimeandikwa hapa na ni takwimu zinazotoka hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu Wizara hii ili iweze ikawa ni endelevu lazima kuwe na mazingira rafiki kwa wawekezaji hasa wazawa kwenye sekta ya utalii. Ukiangalia kodi ambazo Serikali inatoza kwenye sekta ya utalii na hasa tour operators ni zaidi ya 40. Tumeimba, tumeimba, tumeimba! Ajira zinazotolewa vijana kwa mfano kule Marangu kule ambao wanaelekea Mlima Kilimanjaro hawa ma-tour guiders hali ya maisha waliyonayo ambayo ni hoi bin taabani hakuna sera ya kuweza kuwalinda vijana hao. Kama sekta ya utalii umesema indirectly inatoa ajira zaidi ya milioni moja, je wale ambao wanazalisha katika sekta hii hali yao inakuwa ya namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ada hizi, tozo hizi, leseni hizi ambazo wewe unamkamua ng‟ombe tu huna namna bora ya kuweza kumlisha huyo ng‟ombe ili aweze kutoa maziwa zaidi; angalia utalii wa Kusini ulinganishe na utalii wa Kaskazini na kama huu utalii wa Kaskazini unazalisha zaidi unasaidiaje utalii wa Kusini ili kweli kama sisi ni wa pili kwa vivutio vya utalii tuweze tukafaidika na rasilimali hii badala ya danadana ambazo tunapiga kila siku hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia viwanja vya ndege kwa mfano cha Musoma kiko kwenye hali gani? Angalia kiwanja cha ndege cha Iringa kiko kwenye hali gani? Angalia viwanja vya ndege vya kusini kwa mfano Masasi pale ile air strip iko kwenye hali ya namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu Serikali iangalie upya tozo na ada na leseni katika sekta hii ili kujenga mazingira rafiki na endelevu, na hizi fedha zinazotokana na tozo zirudi sasa kwenye sekta yenyewe na hasa kujenga miundombinu ambayo itakuwa ni rafiki na tuweze tukazalisha zaidi. La sivyo huwezi ukakamua tu wakati hutengenezi hali ya ulinzi na usalama kwenye mbuga zetu na kwenye mazingira ya utalii; hali ya miundombinu ya vyoo na hali ya maji, hali ya barabara na hali yote ya mazingira ambayo ni rafiki katika sekta ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa wanyapori. Vitalu zaidi ya 50 vimerudishwa. Mwaka 2008/2009 Serikali ilikuwa inapata zaidi ya dola milioni 20 kwa mwaka kutokana na uwindaji. Leo hii mazingira yamekuwa tofauti kwenye soko la ushindani, mwaka jana Serikali imepata dola milioni nne tu kutoka dola milioni 20 miaka minane iliyopita. Sasa hapa tunaenda mbele tunarudi nyuma? Na hapa kwenye ukurasa wa 36 tunawapongeza TANAPA, ndio wanafanya kazi vizuri, Mlima Kilimanjaro uhifadhi umekuwa wa kwanza kivutio katika Bara la Afrika lakini je, mazingira yale yanatuweka kwenye mazingira gani ambayo leo tunaweza tukasema kweli Tanzania au wanaozunguka mazingira hayo ni rafiki na ni endelevu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe kupitia kwako kwenda kwa Serikali kwamba waangalie tena, narudi tena, kodi hizi, tozo hizi na ukiangalia wawekezaji wazawa kwenye sekta ya wanyama pori ambao ndo tungewasaidia zaidi ya asilimia 90 wameondoka wamefilisika, jiulize kwa nini? Kwanini hamkai nao? Kwanini hamzungumzi? Kwa nini hatujengi mazingira rafiki? Huwezi ukakaa mahali ukajifungia, watu wachache wanafanya maamuzi kwa wale wawekezaji ambao ndio wangesaidia taifa letu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Tanzania yetu hii tuna haki nayo sote kwa pamoja. Mawazo mazuri ni mawazo mazuri tu hata kama yangekuwa yametoka kwa shetani. Ukisoma taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuna mawazo lukuki ambayo yataisaidia sana Serikali. Ukisoma taarifa ya kamati hasa ukurasa wa 12 na 13 ni mawazo mazuri kweli kweli lakini mbona tunarudia kauli zile zile miaka nenda rudi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nishauri kwamba yafaa Mheshimiwa Waziri afanye semina na Wabunge wote, Wabunge wampe mbinu mpya, mawazo mazuri, fikra mpya za kisasa za kuhakikisha Wizara hii miaka mitano ijayo tunatoka hapa tulipo kwenye asilimia 17 ya DGP twende hata asilimia 30 mpaka asilimia 50 tuendane na kigezo cha sisi kuwa wa pili kwa vivutio vya utalii duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mwenyezi Mungu akubariki.