Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mungu kwa kutupa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa Rais wetu wa Awamu ya Tano na mikakati yake ya kuiendeleza Tanzania. Kwa vyovyote vile ametumia weledi stahiki wa Marais waliomtangulia ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa nchi ya neema.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme mambo machache. Mimi ni mmoja wa waumini wa kodi, nashukuru wenzangu waliotangulia wamesema pia kuhusu kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kodi za kawaida za VAT kwenye maduka yetu na huduma zingine za mahoteli, mpaka sasa nchi yetu, kwa maana ya TRA hawajaitendea haki Tanzania kwa maana ya ukusanyaji wa kodi kwa wanaotakiwa kulipa kodi. Ingia maduka ya jumla yaliyoko Dodoma, ingia maduka ya jumla yaliyoko Dar es Salaam, migahawa mikubwa iliyoko Dodoma na of course Tanzania ona ni wapi ambapo wanalipa kodi? Hawatoi risiti, TRA wapo;na kwa sababu kutokulipa kodi ni criminal offence, naomba niishauri Serikali kwenye hili hakuna awareness creation. Huwezi ukahamasisha watu kulipa kodi, ni lazima ufanye coercion, ni lazima utumie nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, badala ya Jeshi letu la Polisi kukaa barabarani na kusimamisha magari yanayokwenda kasi, waingie mtaani kukamata watu wasiolipa kodi na hasa kwenye maduka. Ni lazima wote tukubaliane kwamba tutengeneze nchi ambayo inaabudu kulipa kodi na kwa kuanza hiari haipo, haiwezekani. Huwezi ukasema unatoa tangazo redioni ili mtu alipe kodi, haipo, ni lazima uende kwa shuruti, mtu aone adhabu ya mtu anayopata baada ya kukwepa kodi ndipo wengine wanaanza kulipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fulani nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai pale. Wachaga wakawa wananiambia kitu gani kiliwafanya wao walime kahawa. Wakasema haiwezekani ukahamasisha watu walime zao ambalo wao hawalijui. Wakasema wakoloni walichofanya ni kushurutisha watu ili walime kahawa, lakini baada ya kukomaa ile kahawa wameuza, wale Wazungu wakawaambia sasa haya mapato ni ya kwenu ndiyo waka-induce spirit ya kupenda kulima kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema ni kwamba, kwenye kodi hakuna lelemama, ni lazima kama nchi tukubaliane, kwamba Jeshi letu la polisi tunalo, tunajua maduka hata hapa Dodoma hawalipi kodi, Dar es Salaam tunajua miji yote hawalipi kodi lazima tulipe kodi. Kodi ndiyo itakayoifanya nchi yetu isonge mbele. Kwa hili TRA lazima waongoze, lakini Police Force nayo ifundishwe jinsi ya kufuatilia kodi zetu badala ya kwenda kwenye vitu ambavyo kimsingi havizalishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Bajeti ya Waziri wa Fedha, ameonesha kuanzisha kodi kwenye transfer of shares, yaani unapouza hisa zako, basi wewe utozwe kodi. Nasikitika Mheshimiwa Philip Mpango rafiki yangu na Waziri wetu its unacceptable from all economic point of view; haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukatoza kodi kwenye transfer ya hisa; NMB kwa mfano ilipouza hisa mara ya kwanza iliuza kwa sh. 150, zikapanda mpaka 5000, zimeshuka mpaka 1,500 uliyemtoza capital gain kwenye transfer ya hisa ilipofika 5000; anapo encounter capital loss Serikali itamfidia? Anataka kuuza hisa zake alizonunua kwa 4,000 na bei ya soko ni shilingi 1,000 utafidia hiyo difference ya 3,000? Huwezi kufanya hivyo. Kwa hiyo, siyo ya kiuchumi wala siyo ya kinadharia wala siyo ya kivitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya, Rwanda, South Africa hawafanyi, kwa maana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hakuna anayeifanya hiyo ninyi mnaitoa wapi? Kenya waliiweka kwenye sheria wakaiondoa hata kabla hawajaitekeleza na tukumbuke ni vizuri Waziri afahamu, moja ya sababu ya kuanzisha Soko la Dar es Salaam ni kuhamasisha uwekezaji. Unaposema mtu akiuza unamtoza kodi unafukuza wawekezaji kwenye nchi yetu, chonde chonde naishauri Serikali iachane kabisa na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi ya miamala ya simu. Kaka yangu Mheshimiwa Zungu ameliongelea sana, naomba nisisitize. Bahati nzuri mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; chonde chonde Watanzania kodi hii ni lazima itozwe. Ni kweli miamala hii ni kati ya trilioni 40 mpaka 50 kwa mwaka, Serikali inakosa fedha nyingi kwenye hili. Naomba sana katika hili tuiunge mkono Serikali iendelee kutoza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niunge mkono haraka haraka Kamati ya Bajeti ya kupendekeza ongezeko la Sh. 50 kwenye mafuta ili tuwe na maji. Hivi ni nani ambaye atakataa kwenye hili? Ndiyo maana sioni kigugumizi cha Serikali kinatoka wapi; Wabunge tunapoongea, tunaongea kwa niaba ya wananchi wa Tanzania; this is the feeling of Tanzanians, tunajua kabisa ukiongeza sh.50, kama ukituma salamu kwamba ni kwa ajili ya maji hakuna atakayekataa kigugumizi kinatoka wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisemee kidogo milioni 50 kwa dhima ya Rais wetu. Marais wote duniani wana-dictate vision, lakini kufasili vision ni wajibu wa watendaji kama Waziri na sisi Wabunge kwa nafasi zetu. Rais, Magufuli alichosema kila kijiji atatoa milioni 50, mwenye kufasili utekelezaji huo sio Rais wetu, siyo kazi yake, ni Mawaziri, ni sisi Wabunge. Hakuna uchumi duniani wa kugawa hela.
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu, kwa mfano, Wilaya ya Makete ina vijiji 103, ukikipa kila kijiji milioni 50 maana yake ni Sh. 5,150,000,000/=; Bilioni tano zinatosha kuanzisha Community Development Bank ya Makete na kwenye Tarafa zake sita ukaweka ofisi kwa sababu mtaji wa Community Development Bank ni bilioni tatu. Kwa hiyo, bilioni tano zangu Wilaya ya Makete, ukiwapelekea wakope kwa riba nafuu, hao wote mnaotaka vijiji vikope sasa zitakwenda kwenye Community Development Bank, mtaji ni wa Serikali, wa bilioni tano na Community Development Bank bilioni tano, kwa hiyo Wilaya nzima itanufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama si hivyo, ukiwauliza Wabunge wanajua, kwangu mimi ukipeleka bilioni tano ambazo zinatakiwa kwa milioni 50 kila kijiji, umemaliza kabisa tatizo la maji Makete. Badala ya kugawa milioni 50 waulize wananchi wa Makete watakwambia tunataka lami, tunataka maji. Bilioni tano zinatosha kufuta tatizo la maji, kutengeneza benki Wilayani Makete na Wilaya nyingine za Tanzania ili tuweze kupata maendeleo. Sina hakika kama ni kengele ya kwanza ama ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme naunga mkono hoja na Mungu ambariki Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wake ili twende kwenye haya tuliyopendekeza. Amina.