Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Na mimi naomba nichukue nafasi hii kuchangia machache katika hii hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango katika hotuba zake mbili ya Hali ya Uchumi pamoja na Bajeti nzima ya Nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na nianze kabisa kwa kuunga mkono hoja yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mambo aliyoyazungumzia vizuri katika kitabu cha hali ya uchumi ni suala la kilimo, lakini kilimo kinaonekana kimekuwa kinakua kwa kiwango kidogo sana. Kilimo inaonekana kimekua kwa asilimia 2.3 ukilinganisha na sekta nyingine. Hii inatia wasiwasi wakati tumekuwa tukiimba kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo, kilimo ndiyo kila kitu, ndiyo kinatakiwa kuchangia kwa kiwango kikubwa Pato la Taifa, kilimo ndiyo kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, kilimo ndicho ambacho kinaweza kikachangia katika kuimarisha thamani ya fedha yetu kwa kutuletea fedha za kigeni. Sasa hivi fedha zetu zimekuwa zikishuka thamani sana kwa muda mrefu ukilinganisha na dola, ni kwa sababu uzalishaji umekuwa siyo mzuri na mauzo yetu nje ya nchi yamekuwa siyo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo hiki kikiimarika kinaweze kusaidia vizuri sana ukiangalia katika hotuba zote tulizozitoa, ukiangalia katika maelezo yote aliyotoa tumeimba sana kilimo ni uti wa mgongo, lakini hakuna mikakati ya dhati inayoonekana kabisa kwamba kweli tunaenda kuiimarisha kilimo. Nataka kusema bila kuimarisha kilimo hii tunayosema uchumi umeimarika, umekuwa itakuwa ni hadithi, kwa sababu watu walio wengi asilimia kubwa wanategemea kilimo, bila kuwasaidia wao hizo sekta nyingine haziwagusi moja kwa moja. Kwa hiyo, ni lazima tuweke mikakati ya makusudi ya kuhakikisha kwamba kilimo kweli kinawekewa mikakati itakayosaidia kuimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kabisa ruzuku ambayo itatolewa kwenye pambejeo ni ndogo sana, sasa kama kweli tunataka kuimarisha kilimo tuongeze zuruku. Mimi nina uhakika kabisa Mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini na hasa kwenye Jimbo langu la Vwawa wakulima wakipatiwa pembejeo za kutosha tutalima vizuri sana na tutazalisha kwa ziada nchi itapata ziada nyingi sana.
Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iangalie upya sera ya kilimo ili kuhakikisha kwamba pembejeo zinafika kwa wakati na zinapatikana. Kilimo cha kahawa kiweze kufufuliwa, mahindi, pareto, tumbaku na mazao mengine yatachangia sana katika kuimarisha uchumi wa nchi hii. Hii kwa kweli haijanifurahisha kuona kwamba kilimo sasa hivi kimechangia kwa asilimia 2.3 tu wakati ndiYo kilikuwa kinaongoza kuliko sekta nyingine zote, hilo ni la msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo ningependa nichangie ni kuhusu Mfuko wa Maji Vijijini. Naipongeza Serikali imesema kwamba kutakuwepo na Mfuko wa Maji Vijijini na utaendelea kuwepo, lakini huu mfuko fedha ambazo zinapatikana zinaonekana bado ni ndogo. Sisi tungependa kabisa vijiji vyote vipate maji ili tuondokane na hili lazima tuje na mkakati wa makusudi kwa kipindi kifupi, iwezekane kabisa kipindi cha miaka miwili, mitatu tumalize kabisa hili tatizo la maji vijijini. Ili kumaliza hilo ni lazima tuweke tozo kwenye mafuta, kama tukiweka kwa mfano ikiwa shilingi mia tutapata fedha za kutosha kabisa zitakazoweza kusambaza maji katika vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaita Mfuko wa Maji, lakini hivi fedha nyingi zimekuwa zinatumika kwenye maendeleo ya maji mijini, kama ni za vijijini ziende kweli vijijini hiyo ndiyo itakayoweze kutusaidia na kuleta kweli kuinua hadhi. Mimi ninaamini kabisa kama maji tukiyasambaza vijijini wale wananachi wa vijijini maisha yao yatakuwa mazuri na watapata maji safi na salama na pia wataweze kulima hata kumwagilia bustani pale walipo katika maeneo yao itasaidia sana. Nafikiri hilo ni suala la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni kuhusu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa kweli niseme kabisa mimi nimesikitika na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya ofisi hii, hii inatokana bajeti yetu imeongezeka! Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali anatakiwa kukagua Wizara zote, anatakiwa kukagua Idara zinazojitegemea zote, Wakala zote, Balozi zote, Mashirika ya Umma na haishii hapo tu anatakiwa kwenda kukagua miradi yote ambayo tumeipitisha. Ukiangalia kwenye bajeti yetu miradi ni mingi sana tunayoenda kuitekeleza, asilimia 40 ya bajeti inaenda kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipompa fedha za kutosha Mkaguzi nani atakayekwenda kufuatilia hiyo miradi na kuhakikisha kwamba hizo fedha kweli zimetekeleza yale ambayo tunayapitisha hapa Bungeni? Kwa hiyo, nashauri lazima iangaliwe upya ikiwezekana Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unapitia upya mid year review ya bajeti lazima tuhakikishe Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anapatiwa fedha za kutosha ili aweze kutekeleza majukumu yake ambayo yapo Kikatiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hatakiwi uhuru wake kuingiliwa, kwa sasa hivi kinachojionesha ni kwamba atakuwa anaanza kuomba omba fedha na akianza kubembeleza kuomba fedha maana yake atakuwa na compromise independence yake, sasa hili ni suala ambalo lazima tuliangalie sana na huyu ndiye mwakilishi na ndiyo jicho la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kwamba inaisimamia ipasavyo Serikali. Kwa hiyo, naomba lazima hili suala liangaliwe vizuri ili angalau tuweze kwenda mbele, hili ni la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naelewa azma ya Waziri anayoisema, labda tuangalie Waziri je, mlipokagua mlikuta hela zake zinatumika vibaya? Kama mmekuta kwamba matumizi yake yalionekana mabaya basi ni sawa sawa. Lakini kama haijaonesha hivyo ni vema akapewa fedha za kutosha ili akafanye kazi ile ambayo tumeikusudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa nichangie ni kuhusu kiinua mgongo cha Wabunge. Wenzangu wamechangia vizuri na mimi nisingependa nilisema sana. Nilitaka kusema sikuona sababu ya azma ya Serikali ya kulileta kwenye Bunge hili la kwanza kwa nini limeletwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, naelewa Kanuni za uhasibu za kimataifa zinavyosema, zinataka kiinua mgongo kitakacholipwa baada ya miaka mitano kinatakiwa kisambazwe katika miaka yote ambayo mfanyakazi ametumikia, yaani kama Mbunge ametumika kwa muda wa miaka mitano basi iwe prolated katika kipindi cha miaka mitano. Kwa hiyo, ina maana lazima ianze kuwa provided kwenye vitabu vya uhasibu kuanzia mwaka wa kwanza, hiyo azma naielewa, lakini haitakatwa kodi na haitatolewa, haiwezi kutolewa sasa hivi kwa sababu itakuja kutolewa mwaka wa mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna sababu gani ya kuzungumzia masuala ya kodi kwa leo wakati hii kodi haitakatwa chochote mwaka huu? Kwa hiyo, hili suala kuna haja ya kuliangalia vizuri. Mimi nadhani hili linatuletea matatizo. Wenzangu wamelizungumzia vizuri nisingependa niliseme. Najua lazima liwe provided kwenye books of accounts, lakini lifanyiwe kazi vizuri ili li-cover wote wanaotakiwa kulipa kodi walipe, siyo tu iende kwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la mwisho ambalo ningependa nilichangie ni kuhusu shirika letu la ndege. Nimefurahishwa sana na Serikali kwamba tunataka sasa kulifufua shirika letu, lakini hili shirika lina madeni mengi sana na makubwa. Hizi fedha ambazo zimetengwa nisingependa ziende tena kwenye hili shirika, ningependa lianzishwe shirika lingine au hilo livunjwe lianzishwe lingine ndiyo lipewe hizo fedha na ndege tatu, hapo tutaweze kuona mchango halisi. Hizi fedha zikitolewa kama zilivyo mwisho zitaenda kulipa madeni mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante.