Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Mary Deo Muro

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja zilizoko mezani juu ya Mpango wa Miaka Mitano. Kwanza namshukuru Mungu kuniwezesha kufika katika Bunge lako Tukufu. Pia nashukuru chama changu kuniona nafaa kuiwakilisha jamii. (Makofi)
Awali ya yote, napenda kuungana na wale wote ambao wamechangia hoja inayohusu Tanzania ya viwanda kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kabisa kwamba Tanzania ya viwanda lazima iendane na afya ya wananchi, elimu, utawala bora, miundombinu, maji na ardhi. Nafahamu kabisa kwamba nia na madhumuni ya mpango huu ni kuleta ustawi wa jamii kwa wananchi wa Tanzania ndiyo maana Upinzani na Chama Tawala tunachangia kwa hoja nzito ili tuweze kuleta ustawi wa jamii kwa Watanzania wote. Lengo letu siyo malumbano, lengo letu ni kuhakikisha kwamba Watanzania ambao wanatumia pesa zao kwa ajili ya kutuweka hapa wanapata haki stahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye mada halisi. Ningependa kuongelea afya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa kwamba hakuna ufanisi katika Tanzana ya viwanda bila wananchi kuwa na afya bora. Tukiangalia maeneo mengi ya Tanzania tunakuta kwamba huduma za afya ziko hafifu. Kwanza nakumbuka asubuhi ya leo kulikuwa na msemaji mmoja ambae alitoa haja yake kuhusu hali halisi ya afya ya Watanzania na mazingira wanayoishi. Waziri husika alijibu kwamba Serikali siyo sababu ya wananchi kupata matatizo ya afya, isipokuwa wananchi wenyewe ndiyo sababu ya kupata matatizo ya afya au magonjwa ya kipindupindu na magonjwa ya mlipuko. Mimi napenda niulize Serikali iliyoko madarakani kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa kwamba kuna sekta zinazoshughulikia afya na kama kuna tatizo la kipindupindu ina maana kwamba sekta inayohusika haijawajibika. Nataka nijielekeze kwa mfano, natoka Mkoa wa Pwani Wilaya ya Kibaha, ilitokea mlipuko wa kipindupindu na sababu kubwa ni kwamba, Wizara ya Maji kwa Pwani haina mamlaka isipokuwa tunatumia DAWASCO ambayo kwa Pwani hakuna miundombinu ya kutoa maji machafu. Ina maana utiririshaji wa maji machafu ni lazima kwa sababu DAWASCO haijawajibika na watu wa Pwani wanahitaji mamlaka yao ili waweze kuiwajibisha pale inapokuwa haiwezi kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, narudi kwa Waziri aliposema kwamba siyo wao wanaosababisha, yeye kama Waziri anafahamu kabisa ni nani ambaye hakuwajibika mpaka mlipuko wa magonjwa utokee. Kwa hiyo, hawezi kusema kwamba yeye siyo sababu. Napenda kumwambia kwamba yeye na Watendaji wenzake hawakuwajibika. Walitakiwa wawajibike ili ugonjwa wa kipindupindu usitokee kwa sababu wapo ambao wako kwa ajili ya kazi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kwenda kwenye sekta ya elimu, tunaangalia Tanzania ya viwanda ambayo inatakiwa iende na elimu. Ni kweli tumedahili watu wengi kwa ajili ya sekta mbalimbali, lakini tuangalie sheria zinazo-govern uanzishwaji wa viwanda. Tunafahamu kabisa uanzishwaji wa viwanda siyo ufufuaji wa viwanda pengine ni uanzishaji wa viwanda kwa mashirika yanayotoka nje, wawekezaji kutoka nje. Hautaondoa umaskini Watanzania kama waanzishaji wa viwanda wanakuja wa watu wao kutoka nje, kama sheria za nchi haziwezi kusimamia kuhakikisha kwamba rasilimali watu iliyopo hapa ambayo ni watoto wetu ambao wamesomeshwa kwa pesa za Watanzania wanaajiriwa katika viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeiomba au niishauri Serikali kwamba, itakapoanzisha mpango huo ihakikishe kwamba inatunga sheria ambazo wawekezaji watakuwa nazo wakiangalia kwamba Tanzania ina watu ambao wanaweza kufanya kazi ambazo wanaleta watu wao kuja kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano, kuna bomba sasa hivi linatoka Ruvu chini kupeleka maji Dar es Salaam. Nimeshuhudia kwa macho yangu, mpaka yule wa kufukua udongo, yule mtu wa kufanya kazi za welding ni Mhindi wakati tuna Watanzania tunawasomesha VETA hizo mnazosema zimeanzishwa wamekaa mitaani hawana kazi. Sasa unajiuliza je, huu umaskini tunaouimba hapa utaondolewaje kwa kiasi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiachana na hapo naomba niende kwenye kilimo, nimesoma, nimeangalia jinsi Waziri wa kilimo alivyojipanga, lakini naomba niongee machache juu ya hilo. Nimeona kilimo kina ufugaji, kina kilimo yenyewe, lakini nikiangalia kuna ufugaji, naomba ni-declare interest mimi ni mfugaji wa kuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mara nyingi sana kuku wakitoka Kenya wanajazwa pale Dar es Salaam kiasi kwamba wafugaji wa Tanzania tunashindwa, wajasiriamali wa Tanzania tunashindwa kuweza kufanya biashara. Sasa ningeomba Wizara katika Mpango huu wa Tanzania ya viwanda basi wahakikishe kwamba Wizara husika inasimamia kidete hali hii ili Watanzania wajasiriamali waweze kufaidika na kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeomba upangaji wa bei, mkulima amelima kwa shida zote, Serikali inakuwa mpangaji wa bei. Serikali inapanga bei wakati mkulima amelima kwa gharama zake. Anapokosa mapato mkulima anashindwa kuendeleza kilimo. Kwa hiyo, umaskini hatuwezi kuondoa kama Serikali haiwezi kusimamia kilimo ipasavyo, kutafuta masoko ambayo yana tija na kuhakikisha kwamba mkulima anapata faida ili kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu. Nimeangalia miundombinu nikaona kwamba kwa usafiri kwa mfano wa Dar es Salaam, msongamano wa Dar es Salaam nilivyouangalia, sisi sote tunafahamu kwamba time ni factor ya production, kama hatuwezi ku-save time tuna-consume time kwenye kutembea kwenye barabara masaa manne kutoka Kibaha mpaka ufike Dar es Salaam, masaa manne kutoka Mbagala mpaka city center ukafanye kazi, ina maana muda mwingi unapotea hapo katikati bila kutumika. Hii ina maana kwamba Tanzania ya viwanda watu watakuwa wanatembea kwenye magari masaa manne hawajafika kiwandani ina maana utekelezaji wake utakuwa mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende kwenye miundombinu ya maji. Nimesoma na nimesikiliza lakini nimeshangaa kusikia kwamba asilimia 68 ya Watanzania wanapata maji. Jamani mimi natoka kijijini kwetu Makambako chini kule hawajawahi kuona maji ya bomba hata siku moja. Nimekuja huku Kisarawe Mkoa wa Pwani wanachota maji ya visima, hiyo asilimia 68 ambayo wamei-calculate wakapata hapa sijaweza kuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama kweli tuna nia ya dhati ya kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na afya bora, hebu Serikali ijipange kuhakikisha maji ya uhakika yanapatikana kwa ajili ya kuwapa afya bora Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye ardhi. Ni kweli kabisa ardhi ndiyo mpango mzima wa Tanzania ya viwanda ya Mheshimiwa Magufuli, lakini naomba nitoe ushauri...
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha mchangiaji.