Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuuona mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nitumie fursa hii kuwatakiwa heri wale wote waliojaaliwa kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Wizara ya Fedha, Ofisi ya CAG, binafsi sioni kama tumeitendea haki Ofisi ya CAG kwa sababu pesa zote tunazozipeleka katika Halmashauri zetu bila kumuwezesha CAG hakuna tunachokifanya. Kwa sababu hatafanya kazi yake kwa uhakika, atafanya pale ambapo atakuwa amepafikia vinginevyo kama tunasema labda fedha hizi tunazozipeleka kule ziende zikaliwe na wale ambao wamezoea kula fedha za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisema hilo naomba nisemee mafao ya Wabunge. Mbunge ninakatwa kodi kila mwezi shilingi 1,063,000; inanishangaza sana kuona mafao yangu ya mwisho ninakwenda tena kukatwa kodi. Wakati ninapomaliza Ubunge mimi silipwi tena ile pensheni wanayolipwa watumishi wengine. Nimuombe Waziri wa Fedha atakapokuja hapa atuambie ni kwa nini na kwa nini iwe kwa Wabunge tu na kwa nini iwe ni mwaka huu? Kwa hilo Waziri wa Fedha naomba utupe mchanganuo mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninajikita zaidi leo katika hotuba ya Waziri wa Fedha ukurasa wake wa 30 mpaka ukurasa wa 31.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kusema Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tulisema kwenye majukwaa tutajenga vituo vya afya kila kata na tutajenga zahanati kila kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikichukua kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha hotuba yake ukurasa wa 31 naomba nimnukuu anasema; “Tutaimarisha mifumo, majengo na miundombinu mingine katika shule za awali, shule za misingi, za sekondari, upanuzi wa vyuo vikuu, ukarabati, ujenzi wa vyuo vya elimu ya juu, upanuzi wa vyuo vya ufundi, miradi ya kuboresha Hospitali za Rufaa, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Magonjwa Kuambukiza Kibong’oto na kuanzisha programu ya kuzalisha ajira na programu ya maendeleo ya ujuzi, mazingira na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sehemu yoyote ambayo ametuambia upande wa afya tunakwendaje kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya kujenga kituo cha afya kwa kila kata, hakuna kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya. Haitoshi kwenye Wizara ya TAMISEMI nilichangia nikasema hakuna sehemu yoyote ambapo TAMISEMI wameonesha kwamba ni wapi tunakwenda kutekeleza ujenzi wa vituo vya afya na zahanati katika vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamtaka Waziri aniambie, tunaposema tunakwenda kujenga vituo vya afya, tunategemea Halmashauri ikajenge vituo vya afya kwa mapato ya ndani? Halmashauri inayokusanya milioni 300 itakwenda kujenga vituo vya afya kwenye Kata zake? Hili haliwezekani! Sijui ni kwa nini Serikali yote kuanzia TAMISEMI mpaka Waziri wa fedha hawakuitizama Wizara ya Afya.
Mheshimwia Naibu Spika, tunaposema tunataka vituo vya afya kila kata. Tuna kata 3,963, vituo vilivyopo vya Serikali ni vituo 497 tu ambavyo vinatoa huduma ya afya na vituo hivi havijakamilika. Katika vituo 497 vinavyotoa huduma, ni vituo 106 tu vinavyotoa huduma ya upasuaji, sasa tunapokwenda kusema, tunataka kuondoa vifo vya mama na mtoto, tunaviondoaje wakati vituo vyetu vya afya havina majengo ya upasuaji? Tunaposema tunaboresha afya kwa wananchi wetu, tunaboreshaje wakati hata vitu vilivyopo havijakamilika?
Naomba Waziri wa fedha atuambie kama kwa mwaka huu hakuna
kitu chochote kinafanyika katka ujenzi huu, nina hakika Halmashauri hatuwezi kujenga vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano tu; Wilaya ninayotoka tuna kata 26, unakwendaje kujenga vituo vya afya vyote kwa kutegemea mapato ya ndani? Hili Wizara ya Fedha waliangalie halijakaa vizuri kabisa, hatutakwenda kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Ninaomba atakaposimama, ajibu wamejipanga vipi kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga vituo vya afya kwa kila kata ili kuhakikisha kwamba tunapunguza au tunaondoa kabisa vifo vya mama na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vifo vya mama na mtoto vinatokea kwa sababu gani? ukienda kwenye Kituo cha afya, huduma ya upasuaji haipo, huduma ya damu salama haipo. Vifo vya Watoto vinatokea ni kwa sababu ya upungufu wa damu. Ukienda kwenye kituo cha afya, damu salama haipo. Tunasemaje tunatapunguza vifo vya mama na mtoto wakati majengo ya upasuaji na huduma ya damu salama haipo kwenye vituo vyetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali, badala ya kusema tunakwenda kujenga vituo vipya vya afya, tuvichukue hivi 497 ambavyo vipo na vinatoa huduma, tuhakikishe vinatoa huduma zote zinazostahili katika vituo vya afya, kuliko kwenda kuanzisha majengo mapya ya ujenzi ambao pia tunaacha yale ambayo yanatoa huduma na hayajakamilika. Hayajakamilika kwa sababu gani? Unakuta hakuma wodi ya mama, hakuna wodi ya watoto, hakuna wodi ya akina baba, hakuna wodi ya akina mama wala hakuna jengo la upasuaji. Kwa hiyo, niishauri Serikali iende ikakamilishe kwanza vile vituo 497 wahakikishe kila kituo kinapata jengo la upasuaji, ndipo hapo tutakaposema kwamba huduma ya afya sasa tunakwenda kuiboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, niende kwenye shilingi milioni 50 za kila kijiji. Imetengwa kwenye bajeti, asilimia sita tu ya asilimia 50 kwenye kila kijiji. Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015, tulisimama tukasema kila kijiji kitapata shilingi milioni 50. Tuna maswali mengi kwa wananchi wetu, nikitizama kwenye bajeti hii ni shilingi bilioni 59 tu ambazo zimetengwa kwenye bajeti hii ambayo ni sawa na asilimia sita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inanitia hofu kama tutakwenda kwa asilimia sita mwaka huu, ndani ya miaka mitano, tutakuwa hatujafikia lengo ambalo tumelikusudia kwa wananchi wetu. Niungane na Kamati, niishauri Serikali badala ya kutoa asilimia sita, itoe asilimia 20 kwa mwaka huu wa fedha. Tukijipanga kwa kutoa asilimia 20 kwa mwaka huu wa fedha, maana yake utatoa shilingi bilioni 196, ndani ya miaka mitano tutakwenda kuvifikia vijiji vyote tulivyonavyo, bila kufanya hivyo tutafikisha miaka mitano na hatutakuwa tumevifikia vijiji vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda bado unaniruhusu, naomba niongelee suala la maji. Tatizo la maji ni kubwa sana. Nimuombe Waziri wa Fedha, kuna miradi mingi ya muda mrefu ambayo bado inadai fedha, wakandarasi wanadai fedha. Hebu nendeni mkakamilishe miradi hiyo, walipwe wakandarasi hao na miradi iweze kufanya kazi. Nitoe mfano mdogo tu, kuna mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Tinde ambao mpaka leo haujakamilika kwa shilingi milioni 100 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninaunga mkono hoja.