Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi njema na kazi nzuri anayoifanya kwa kuwatumikia wananchi ambapo mpaka sasa ninaamini kabisa kwamba Rais ndiyo mzalendo namba moja wa nchi yetu hii kwa kazi kubwa sana ambayo ameweza kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache sana ya kuchangia na Wabunge wenzangu wengi wamechangia, lakini nataka kuchangia suala la CAG kupewa fedha ndogo. Sioni dhamira ya dhati au dhamira njema ya Serikali yetu katika suala la kuhakikisha tunawamaliza kabisa mafisadi nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha tulizowapa CAG ni fedha ambayo itatosheleza tu kulipa mishahara na kuendesha ofisi pale, hatutoweza kwenda mbali zaidi kufuatilia fedha zetu ambazo leo hii Serikali yetu ya CCM imesema elimu bure mpaka shule ya msingi, mpaka shule ya sekondari na fedha tumepeleka, nani wa kuzifuatlia fedha zile? Sasa ninaona kuna shida, Waziri atuambie ana dhamira gani au ana chuki gani au Bunge mtuambie CAG ni adui wa Serikali? Na kama ni adui tujue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake mimi nijuavyo, CAG ndiyo anaetusaidia sisi kuona, CAG ndiye anayeweza kutuambia wapi kumeibiwa fedha Bunge likaenda kufuatilia. Kwa hiyo, ninavyojua CAG ndiye jicho la Serikali yetu na Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Leo Serikali yetu, Waziri wa Fedha unampa fedha ndogo sana ambazo ninaamini yeyote yule ambaye anataka kujua ufisadi upo wapi lazima tumtumie CAG, fedha hana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema leo kwamba akiwa amepungukiwa fedha aje agonge tena mlango, usipomfungulia mlango, aende wapi? Kwa hiyo, ninataka Waziri ukija utuambie CAG ni mtumishi wa Serikali? CAG ni adui wetu? CAG ni nani, ni shetani au ni mtu gani? Tujue. Maana yake tunakua tunamtenga, tukimchukia bila sababu yoyote ya msingi na leo hii unamwambia aje akuombe fedha tena, atakuwa akija kukuomba mara kwa mara mwisho wa siku atakuwa anakupigia magoti hatoweza kukuchunguza, hatoweza kukukagua na dhamira ya Serikali yetu na Rais wetu ni kuhakikisha mafisadi wote tunawateketeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunampa fedha kiasi kidogo, tunawezesha watu wengine, mfano tunaenda kumpa TAKUKURU shilingi bilioni 72. Ili TAKUKURU afanyekazi vizuri anamtegemea CAG avumbue maovu kule, leo tunampa fedha kiasi kidogo asiweze kufanya kazi. Hili naomba sana tulisimamie, Wabunge kama kweli Wabunge kazi yetu ni hiyo basi naomba tulisimamie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Waziri wa fedha, ninakumbuka kwenye party caucus ukija kujitambulisha kama Mbunge na Waziri, kuna kauli ulisema leo hii nataka kuiamini. Ulisema Wabunge tusitegemee kukupenda. Hili leo umekuja kusema Wabunge tukatwe kiinua mgongo chetu kodi, Mbunge peke yake tena unasema narudia ili wananchi watuchukie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani niseme hili Wabunge msikilize, katika hili wananchi hawataweza kutuchukia, wataendelea kutupenda kwa sababu nusu ya fedha hizi asilimia 60 zinakwenda kwao. Inawezekana Mheshimiwa labda hujui uchungu wa Jimbo. Sisi ndiyo tunaojua uchungu wa majimbo yetu. Kwa nini iwe ni kwa Mbunge peke yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema ukarudia tena, narudia tena, narudia tena ili wananchi wasikilize, Wabunge tukupigie makofi na mimi nasema Wapinzani walikuja hapa wakasema na wenyewe wanaunga mkono hoja, nilitaka kucheka sana.
Mimi nataka niseme mimi leo nasema hivi, kama atatokea Mbunge yeyote wa CHADEMA akaja akaandika hapa barua kwako, kwamba mimi naomba nikatwe kiinua mgongo na posho hizi kwa barua na mimi nitakuwa wa kwanza kukatwa. Mnikate! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hii Mheshimiwa Waziri uliitoa wapi, umekuja kuwapa ajenda isiyokuwepo hapa, hili sijui limetoka wapi? Maana yake hawa jamaa tulikuwa tumeshawaua, wanakuja wanasema na wenyewe wanaunga mkono hoja. Nataka niseme, waje hapa Wabunge wa CHADEMA hususani Mheshimiwa Silinde aandike barua kwa maandishi yake kwamba na mimi niwe wa kwanza kukatwa posho na mimi niwe wa kwanza kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo changu na mimi nitakuwa wa pili kutoka yeye.

MHE. KHALFAN H. AESHI: Hamna, hatoweza kuja hapa. Sasa hii tusiwe tunawapa hapa kila siku sababu ya kusema. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri ukija hapa kodi zetu kwenye kiinua mgongo ifutwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kuongelea kuhusiana na suala la kilimo. Tumetoa kodi kwenye mazao mbalimbali, tunatoa kodi tukitegemea kwamba tutazalisha, lakini ninavyojua wafanyabiashara hawa mawakala wadogo wadogo walioamua kukopa mabenki na kwenda kuwakopesha wakulima pembejeo, mpaka leo fedha hizi hawajalipwa, mwaka wa pili unakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha hebu liangalie hili, wapeni fedha hawa Kilimo wawalipe hawa wakulima, wakawalipe hawa mawakala ili mwaka huu waweze kuagiza mbolea kutoka nje, waje huko wawakopeshe tena wakulima. Lakini mpaka leo fedha hizo hakuna. Sasa tutategemea nini? Mnasema kilimo uti wa mgongo, kilimo ndiyo tunakitegemea, nashindwa kuelewa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kabla muda haujakwisha ni suala la afya. Wizara ya Afya wamepewa fedha ndogo. Kutokana na kukosekana kwa fedha tumejikuta tuna majengo ambayo yalijengwa na Taasisi ya Benjamin William Mkapa, ndani ya Mkoa wa Rukwa mpaka leo hayajafunguliwa kwa kukosa fedha. Matokeo yake mwaka wa tatu sasa unakwenda, majengo yanaharibika na unajua majengo yasipotumika yanaenda yanashuka thamani siku hadi siku. Wapeni fedha wakafungue zahanati zile na majengo yale ili yaweze kufanya kazi. (Makofi)
Nheshimiwa Naibu Spika, mwisho najua bado dakika nyingi kengele ya kwanza hiyo! Kuhusu suala la kodi kwenye transit goods tumeingiza VAT, lakini ninavyojua anayetakiwa kulipa VAT ni yule mtumiaji wa mwisho! leo mzigo unatoka hapa unakwenda Zambia, wanalipia VAT. Mzigo unatoka hapa unakwenda Congo tunalipia VAT. Mwisho wa siku hawa wasafirishaji watatuhama watakwenda kwenye bandari nyingine. Hivi kwa nini hili hatulisikii? Kwa nini tunapowashauri Serikali hamtaki kusikia? Nataka niulize hii Kamati ya Bajeti ina kazi gani? Kama maoni yao yote hakuna hata moja iliyochukuliwa, futa Kamati ya Bajeti, eeh!(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana tumeweka Kamati ya Bajeti kuishauri Serikali lakini hakuna hata moja kwa kumsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, anasema mambo yote hayajaungwa mkono hata moja na Waziri. Toa chini wanatumia fedha nyingi, sasa hivi wako kwenye vikao wanakaa kule, hakuna lolote linaweza kuchukuliwa.
Mimi nasema kwa uchungu sana, nina nia njema na nchi yetu, lengo la Wabunge ni kuiongoza nchi yetu, tuwashauri Mawaziri, tuishauri Serikali ili tuweze kwenda kule tunakotaka kwenda na kule ambapo Rais wetu anataka kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ana dhamira njema sana lakini inawezekana tunampotosha, kuna baadhi ya mambo hatumwambii ukweli. Sasa hao wasafirishaji wakihama wakihamia Beira, wakahamia Mombasa, bandari yetu inakufa. Tulikuwa na nia ya kuongeza bandari ya pili kutokana na mizigo kuwa mingi leo hii ukienda bandarini mizigo inapungua. Itapungua leo, itapungua kesho, itapungua siku hadi siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kuna suala la kodi kwenye crude oil ambayo leo yamewekwa mwaka jana na mwaka juzi uliopita tuliondoa kodi hiyo kwasababu tuliona kama ni raw material anayekuja hapa ili viwanda viweze kutengeneza mafuta ya kula.

TAARIFA.....

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sina kampuni, kampuni ya baba ile, siyo ya kwangu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongelea kuhusu crude oil, mafuta yetu ya kupikia. Tumeongeza kodi kwenye viwanda vyetu vinavyotengeneza mafuta na sasa hivi tumeweka kodi ya raw material inayotoka nje ili iweze kuzalishwa wananchi wetu hawa waweze kupata mafuta kwa bei nafuu, sasa tumembana kote kote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumembana kwa wakulima hawa wanaozalisha alizeti, anapoenda kuuza kiwandani yale mafuta yanapotoka pale yanakuwa na kodi, lakini vilevile tumewabana sasa hawa waagizaji mafuta ya crude oil inayotoka nje na yenyewe imewekwa kodi. Lengo letu ni kuinua viwanda, dhamira ya dhati ya Rais ni kujenga viwanda na hawa wawekezaji wanasema walitaka kuomba waongezewe angalau mwaka mmoja mbele ili viwanda vya hapa nchini viwe vimekamilika waweze kuzalisha hapa crude oil. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi lakini nimuombe Waziri pale ambapo tunakuwa tunawashauri basi haya tunayowashauri wayachukue kwa sababu sisi tunawawakilisha wananchi na haya tunayoyaongelea hapa ni mawazo ya wananchi ili muweze kuyafanyia kazi na tuendelee pale ambapo Rais anapotaka tufike. Ahsante.