Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nianze kwanza kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na watumishi wote wa Bunge, kama mtakavyokumbuka kwa mujibu wa Katiba ya Bunge Sports Club ambapo wamiliki wake na wanachama ni Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watumishi wote, tarehe 1 Juni, 2016 kwa pamoja mlinichagua kuwa Mwenyekiti wa Bunge Sports Club. Natumia fursa hii kuwashukuru sana. Ahsanteni sana. Ninaahidi kutowaangusha katika masuala ya burudani na michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara ya Fedha na Mipango kwa hotuba yao nzuri, imetupa mwelekeo, lakini shukrani za pekee ni kwa Mheshimiwa Rais, amekuja na bajeti ambayo 40% inakwenda kwenye maendeleo ya Taifa. Tunashukuru sana kwa sababu, ni kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida, kwa taratibu za kawaida za mijadala kama hii, ukiona watu hawaliongelei jambo, maana yake wanakubaliana nalo. Kwa hiyo, hata mimi mwenyewe sitatumia muda mwingi sana kwa mambo ambayo hayana mjadala mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee mambo machache. Ukurasa wa saba wa Kitabu cha Hotuba cha Mheshimiwa Waziri anatukumbusha malengo makuu ya hotuba hii ya bajeti kwamba, la kwanza ni kutatua kero za wananchi, lakini la pili ni kujenga uchumi wa kipato cha kati kiuhalisia kwa kusimamia kwa umakini na utulivu kuhusu uchumi wetu huu uliopo sasa. Kwa kweli uchumi wetu uko vizuri. Pamoja na kwamba ni nchi maskini, lakini wote tunakumbuka kwamba kwa taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia mwaka jana, 2015 mwanzoni Tanzania sasa siyo miongoni mwa nchi masikini sana duniani, tumeshajinasua kutoka kwenye lile kundi. Kwa hiyo, kwa namna yake kwa aina fulani tuna utulivu wa kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye hoja niliyokuwa naisema, yale mambo ambayo hayazungumzwi sana, hayana utata hapa, tunakubaliana nayo; lakini yako mambo yanahitaji Serikali na Wabunge tuyatafakari kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nihoji kuhusu hili lengo la pili la kuusimamia utulivu wa uchumi wetu kwa umakini na kwa ubora ili kuongeza tija na hasa katika suala la ajira. La kwanza, hivi tunapokuwa tunaanzisha kodi ya VAT kwenye huduma za utalii wakati tunafahamu kabisa majirani zetu, washindani wetu wameshaondoa hiyo kodi, huu ni usimamizi makini wa uchumi ambao tunakusudia kuufikia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kama alivyosikia Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla mlivyosikia, Waheshimiwa Wabunge tukiwa wawakilishi wa wananchi, kuna hajo na kuna jambo la kutafakari hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anafanya rejea kwenye hotuba yake wakati anawasilisha, alisema baadhi ya nchi ambazo zimekuwa na utaratibu huo ni pamoja na Kenya, lakini kesho yake kuna gazeti moja liliandika Mheshimiwa Waziri wa Fedha apigwa chenga. Kwa sababu nchi ile siku hiyo hiyo, bajeti zetu kwa kuwa zilisomwa pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati tuna-introduce hiyo kodi, wenzetu wanaiondoa na ni jambo la kusikitisha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri asikate tamaa, hatujachelewa, tuko pamoja hapa tunajadili. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali kwa ujumla, wasikilize mawazo na ushauri wa Wabunge kwa sababu ni wawakilishi wa wananchi na ni kwa nia njema, hatushindani, hakuna nani zaidi hapa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba suala hili tulitafakari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, natafakari tu. Ukisoma ukurasa wa 64 tunaongeza ada za usajili wa pikipiki kutoka shilingi 45,000 ilivyo sasa mpaka shilingi 95,000. Nataka niikumbushe Serikali na inafahamu zaidi kuliko sisi. Taarifa iliyotolewa mwezi wa tano mwaka huu na Benki ya Dunia inasema; na mtu mwingine anaweza kusema tusitegemee sana taarifa za Benki ya Dunia, lakini hawa ni washirika wetu, kila siku tunawasifu hapa. Wamesema zaidi ya 50% ya Watanzania ni maskini na katika hao miongoni mwao milioni 12 ni maskini zaidi. Chini ya mstari wa umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia waendesha bodaboda na wamiliki badoboda, pikipiki hizi, ndio kundi la milioni 12. Leo tunapandisha ada ya kusajili vyombo hivi kutoka shilingi 45,000 mpaka shilingi 95,000, tutafakari tu kwa pamoja. Hii kweli tunajenga! Tunasimamia uchumi wetu kwa utulivu na kwa umakini ambao tunauzungumza hapa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tutembee kwenye maneno yetu. We must walk the talk, kwamba hivi ni kweli, hawa ni wapiga kura wetu. Nataka niseme la ziada katika hilo. Ukiongeza hii ada ya kutoka shilingi 45,000 kwenda shilingi 95,000 wanaoathirika miongoni mwetu ni sisi Wabunge hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yaliyopo kwa Waheshimiwa Wabunge kuwasaidia na ujue kwamba fedha hizi ni za mfukoni, kwa sababu Mfuko wa Jimbo hauruhusu mambo haya. Kwa hiyo, nasema Serikali tushiriki kwa pamoja, tusaidiane, tulitafakari tu. Huu ndiyo umakini na utulivu tunaozungumzia? Nadhani hapana. Hata hivyo, halijaharibika jambo, ndiyo maana tunajadili wiki nzima kuhusu jambo hili. Kwa hiyo, naishauri sana Serikali itafakari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina tafakari nyingine tena ukurasa huo wa 64, kuhusu ada ya usajili kwa namba za magari binafsi. Kwa waliokuwa wanapenda kuandika majina yao kama mtani wangu Mheshimiwa Profesa Maji Marefu, imepandishwa kutoka shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 10 kwa kila baada ya miaka mitatu; natafakari tu. Inavyoonekana ni kama Serikali haitaki kuwaona hawa. Nadhani inasema hawa watu ni kama wanajidai. Ni kama wanaleta mbwembwe, ni kama wanaleta “ubishoo.” Kwa sababu hii kodi ni ya hiyari tu, kwa sababu halazimiki mtu kusajili kwa jina lake. Anaweza kusajili kwa namba za kawaida, lakini kwenye eneo hili pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Waziri anakusudia kupata shilingi bilioni 26. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza, kama tuna umakini na utulivu kuimarisha uchumi wetu tulivu kama ulivyo, inakuwaje tunawaongezea hawa? Kwa sababu hawa wanasajili kwa hiyari yao tu. Anyway, kwa nini tunawaongezea sasa? Ni kwa sababu hatutatki tuone watu wamesajili kwa kutumia majina yao? Hii haiwezi kuwa sawa. Tunaishauri Serikali itafakari, tuone kama kuongeza huku tunaweza kufikia lengo tulilokusudia la kuongeza mapato, kwa sababu wataona kama unawapiga penalty na matokeo yake hawataendelea kusajili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilikuwa nalitafakari, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukurasa wa 44 ukaoanisha na Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anawasilisha ukurasa wa 35, katika mambo ambayo tunakusudia tuimarishe kiuchumi ni sekta ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuuliza, natafakari tu, naiomba Serikali itupe ufafanuzi, kwa nini hatuzungumzii uwekezaji mkubwa wa madini? Kwa sababu hotuba hii ya fedha inazungumzia uchimbaji mdogo. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inazungumzia uchimbaji mdogo, kwa nini hatuzungumzii wachimbaji wakubwa na hapa sizungumzii wachimbaji kutoka nje, tunaweza kuzungumzia wachimbaji wa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo madini yetu tuliyoyachimba hapa hayajafikia 20% kwa hiyo, tuna rasilimali ya madini zaidi ya 80%. Kwa nini hatuweki mkakati wa kuendeleza sekta hii itusaidie katika uchumi wetu? Kwa hiyo, natafakari tu, naomba Serikali itusaidie. Kwa nini hatutaki kuzungumzia uchimbaji mkubwa? Au sasa ndiyo mwisho? Naamini kwamba sio mwisho, lakini tunashauriana na ninaamini kwamba tutafika tunakokusidia.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naamini ya kwanza hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia yanayozungumzwa sana. Kodi kwenye gratuity, kiinua mgongo kwa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hilo eneo linasema, Mheshimiwa Waziri anasema, kodi hii imeanzishwa kwa sababu ya kuweka usawa katika walengwa, walipa kodi. Fine, jambo zuri, tunakubaliana, hatubishani nalo. Nasi hatuhitaji special treatment, lakini kwa sababu msingi ni huo huo kwamba tusibaguane, kwa nini imeletwa kwa Wabunge tu wakati sisi ni kada ya watu wengi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaishauri Serikali itafakari, watufafanulie tu, kwa nini wasilete watu wote wenye hadhi ya kisiasa hawa; wapo wengi wametajwa; Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine wa kisiasa. Kwa sababu msingi wa kuweka hii kodi ni kutokuwa na ubaguzi katika wanaolipa kodi. Sasa kwa sababu tumelengwa sisi na msingi wa utungaji sheria, tunakumbushwa waliosoma sheria, mojawapo ya misingi mikubwa inayozingatiwa ni kutokuwa na kodi baguzi. Sasa tunapolengwa sisi Wabunge tu na wengine wakaachwa; hii ndio inayotuchonganisha na wananchi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali itafakari. Kwa sababu mwishoni tutakuwa na muswada, turekebishe tu kwamba kama ni makundi yote yanayopata hadhi hii yote yawekwe hapa, itakuwa fine; lakini isiwe ni Waheshimiwa Wabunge peke yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine bajeti hii si tunakwenda kukusanya na kutumia? Sasa nilikuwa naangalia, hili suala la gratuity yetu limejitokeza kwenye fungu gani hapa kwenye hiki kitabu? Kwamba leo tunaweka hapa; au ni maandalizi ya kisaikolojia ili tusonge mbele? Natafakari tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma pale, kuna eneo limesema ukusanyaji wa kodi za majengo. Hapa naiunga mkono Serikali, nina sababu zangu. Hapa naomba niiunge mkono Serikali kwa sababu pamoja na wenzangu ambao wamezungumza kwa maoni tofauti, baadhi yao na tumegawanyika hapa, lakini msingi wa Serikali iliokuja nao hapa inasema inakwenda kuimarisha ukusanyaji. Naamini Serikali inasikia kwamba yako maeneo TRA hawajajiandaa vizuri, mojawapo ni Wilaya ya Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu mwezi wa tatu, TRA ni pamoja na Halmashauri, zilikaa pamoja; uwezo wao kwa kweli wa kuyafikia maeneo yote kuhusu eneo hili ni mdogo, lakini kwa sababu Serikali kuna eneo inasema imedhamiria kwenda kuimarisha uwezo wa TRA na kwa sababu lengo ni ukusanyaji, lakini mapato yatazirudia Halmashauri, Majiji na Manispaa kama ambavyo imekusudiwa, tuwape Serikali muda kama alivyosema Mheshimiwa Zungu na Waheshimiwa wengine walivyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuipe muda Serikali ikashughulikie hili jambo, lakini kilicholengwa kwenda kwenye Halmashauri kisiende kinyume na hapo. Tuipe nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nasema katika kufanya mambo makubwa ya msingi lazima kuna kuthubutu. Na mimi nina ushuhuda kwa sababu, wakati mwingine nimeshakuwa muhanga nikiwa Waziri wa Nishati na Madini. Wakati nimekwenda China mwaka 2009 nikiongoza msafara wa Serikali kuzungumzia bomba la gesi la kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam wako watu walitubeza sana wakasema Tanzania haiwezi kujenga bomba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati niliitwa kwenye nchi moja kubwa sana duniani, nikaambiwa kwa nini mnafanya hivyo badala ya kuiachia sekta binafsi? Kwa nini msije tukawapa fedha sisi hapa? Tuliwaambia kuna nchi hapa ziliathiriwa na msukosuko wa uchumi wa dunia zilikwenda kukopa fedha kwenye nchi ya China, na sisi tuna historia ya nchi ya China ya urafiki wa miaka mingi, ndiyo maana tumekatiza kwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika hili nilikuwa naomba tukubali tuipe Serikali muda, kazi yake…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.