Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri wanazozifanya na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kukupongeza wewe kwani katika filamu inayoendelea ndani ya ukumbi huu, wewe ndio nyota wa mchezo. Nikuhakikishie siku zote sterling huwa hauwawi, akiuawa ujue picha imekwisha. Kwa hiyo, naendelea kukupa moyo, endelea kufanya kazi mpaka tarehe 1 Julai na wewe ndiyo kipepeo wa jengo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza bajeti hii kwa sababu imeweka vipaumbele katika afya, elimu, maji na miundombinu na wenzangu wamechangia vizuri na mimi naomba niongeze nyama katika yale waliochangia wenzangu.
Kwanza niishauri Serikali yangu sikivu kwamba bajeti hii ilivyopangwa naomba fedha hizo zipelekwe kwa muda muafaka. Kumekuwa na tabia ya kupanga vitu tunashangilia halafu hela haziendi kwenye maeneo husika na zikienda zinaenda zikiwa zimechelewa na wakati mwingine zinafika kidogo. Sasa ili kutekeleza yale ambayo tumeyapanga hapa, ni vizuri fedha hizo zikapelekwa kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuikumbuke ile miradi kiporo. Iko miradi ambayo sasa hivi imekuwa magofu na kila anayesimama anataja kwenye Jimbo lake, kwenye Wilaya yake. Naona ni vizuri sasa viporo hivyo tuvikamilishe ili hadithi ile ya kuhadithia tena, iwe imekamilika na isiadithiwe tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miradi ambayo imeanzishwa kwa nguvu au michango ya wananchi. Tumehamasisha wananchi wamajitolea na wamejenga hadi walipofikia lakini Serikali bado haijapeleka hizo fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo. Naomba Serikali ipeleke hizo fedha ili kuwatia nguvu wananchi ambao wamejitolea kwa namna mbalimbali kuikubali miradi ile na kuichangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la ukusanyaji wa mapato kupitia kodi za majengo. Katika hili, naomba tathmini ifanyike upya kwa baadhi ya maeneo. Mfano kuna nyumba yangu moja iko Chanika ndani ya plot moja lakini nimeletewa karatasi tatu. Nyumba yenyewe ina karatasi yake, banda la kuweka gari lina karatasi yake na choo cha nje kina karatasi yake. Sasa najiuliza hapa nikalipe nini, kuna nyumba isiyokuwa na choo nje au nikalipe choo tu nyumba niache, au nilipe banda la gari nyumba niache au nikalipe banda la kuku nyumba niache? Siyo hiyo peke yake, nimeona katika nyumba yangu ya Mvuti jiko la nje nalo nimepewa karatasi yake, sasa najiuliza hiyo tathmini ilifanywaje, kwa kuangalia sura ya mtu au kwa majina?
Naomba katika maeneo kama hayo tathmini ifanyike upya, wananchi wako tayari kulipa kodi ya majengo na sisi viongozi tuko tayari kulipa kodi ya majengo lakini iende kihalali. Yapo maeneo ambayo kuna nyumba ya vyumba viwili havijapigwa plasta lakini anaambiwa alipe shilingi 36,000 wakati mwingine ana vyumba vinne vina tiles, bati la South Africa anaambiwa alipe shilingi 21,000, hivi tathmini hiyo inapigwaje? Ni vizuri tujipange upya ili kutekeleza suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hilo hilo la ukusanyaji wa kodi ya majengo na mimi naungana na wenzangu kuomba Halmashauri ziachiwe kukusanya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba yapo mambo ambayo tumekubaliana kwamba mambo haya yatafanywa na Halmashauri, tutakapochukua kodi ya majengo, tutakuwa tunaziua zile Halmashauri na yale ambayo tumewapangia wafanye watashindwa kuyafanya. Kama tumekubaliana kuwapa mamlaka basi tuwape na madaraka ili waweze kufaya kazi vizuri. Halmashauri zimejipanga na zimeishafanya utafiti wa kutosha na wako tayari kwa ajili ya kukusanya fedha hizo za majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kwenye suala la vivuko. Yapo majimbo mengi ambayo yamelalamikia vivuko na yakitaja viongozi mbalimbali wa zamani kwamba waliahidi kuvikamilisha lakini havijakamilika. Yapo maeneo ya Mafia, Bukoba, Ukerewe katika Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika lakini pia bila kusahau Visiwa vya Unguja na Pemba. Wenzetu hawa suala la boat au meli ndiyo chombo kikubwa cha usafiri kwao. Kwa hiyo, yapo mambo ya kusubiri, lakini mengine inabidi tuyafanyie kazi mapema ili wenzetu twende nao pamoja. Kila nikifikiria mimi msiba wa MV Bukoba na MV Spice, bado najiuliza kwa nini mpaka leo hii meli nyingine hazijanunuliwa, naomba hilo tulifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la michezo. Imefika sehemu hizi timu zinakuja kuonekana kama ni za mtu binafsi wakati zinawakilisha nchi. Inafika sehemu timu ya ngumi, netball, riadha, mpira wa miguu, kuogelea, unaambiwa imeshindwa kwenda kambini au imeshindwa kusafiri kwenda kuiwakilisha nchi kwa sababu hakuna pesa, sasa sijui tunajipangaje? Ndiyo maana wale wanaojitolea wachache kusafirisha timu wanajifanya wao maarufu sana na wanajifanya wao ndiyo wanazijua sana hizi timu kuliko Serikali, naomba Serikali zile safari za nje iwe inazigharamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba pia nichangie kuhusiana na ahadi za viongozi. Kuna ahadi za viongozi ambazo wamezitoa katika kampeni, zinavyojirudia mara tatu, mara nne, mara tano kwa awamu tofauti, ile tu siyo aibu kwa Serikali lakini pia ni aibu kwa chama chetu ambacho kimeongoza kwa kipindi chote. Naomba katika awamu hii zile ahadi zote zilizoahidiwa na viongozi waliopita zifanyiwe kazi ili tuendelee kuwapa imani wananchi na pia kuwahakikishia kuwa Chama cha Mapinduzi hakidanganyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ili nisipoteze muda, napenda kuzungumzia suala la kukata kodi ya kiinua mgongo kwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo waliotetea majimbo, mimi ni Mbunge wa Viti Maalum nawakilisha Mkoa mzima, misiba huko mkoani tunaijua, mipira ya huko mikoani tunaijua, michango ya huko mikoani tunaijua, tuna matatizo chungu mzima. Kama kukatwa kodi tulishakatwa kwenye mishahara na ipo michango mbalimbali ambayo Wabunge tunatakiwa tuitoe na huwa tunaitoa. Mpaka tunapofika dakika ya mwisho tunajipanga kwa ajili ya uchaguzi mwingine, naweza nisiwe mimi lakini akaja mtu mwingine, mnapokuja kumkwangua Mbunge moja kwa moja atasaidiaje yule mgombea wa chama chake ili aweze kuingia? Hakuna uchaguzi usiokuwa na gharama, chaguzi zote zina gharama, ndiyo maana hata Serikali huwa inajipanga.
Sasa mimi niombe, suala la kukata kiinua mgogo kodi ya Wabunge litafakariwe upya na tuangalie jinsi gani ya kulifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili niweze kutoa nafasi kwa wengine tena, naendelea kukupongeza kwamba wewe ndiyo nyota wa mchezo, ahsante kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja.