Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kwa mara ya kwanza ili niweze kutoa mchango wangu katika Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha kuwepo katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Kumi na Moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukue nafasi hii pia kwa sababu nimesimama kwa mara ya kwanza kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngara ambao wameniamini na kunipa nafasi hii; kwani hii ni mara ya nne nagombea; na wananchi wa Ngara wamekuwa na imani, Jimbo la Ngara limeshinda kwa kishindo; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepata kura nyingi, Mbunge wa CCM amepata kura nyingi tofauti ya kura 18,000 dhidi ya Mpinzani wa CHADEMA, lakini pia Madiwani wote wa Kata 22 ni wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuonyeshe ni jinsi gani ambavyo wananchi wa Jimbo la Ngara lakini na Watanzania kwa ujumla walivyo na imani na Chama cha Mapinduzi na Serikali yake. Nachukua nafasi hii pia kupongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais. Sikupata nafasi ya kuchangia, lakini ni hotuba ambayo ilijaa weledi ambayo ilileta matumaini mapya kwa Watanzania.
Nachukua nafasi hii pia Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa Mpango huu ambao mmeuleta mbele yetu ambao pia unaleta matumaini. Ndugu zangu mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nje ya Bunge hili nilikuwa nikiangalia yaliyokuwa yakiendelea, wakati mwingine nilikuwa nachelea kujua kwamba ni nini, hususan upande mwingine. Ndungu zangu, ninajua kwamba maendeleo ni mchakato. Miaka 54 inayotajwa kwamba ni miaka 54 ya Uhuru ni muda mrefu, naamini ukilinganisha na yaliyofanyika ni mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanasahau kwamba tayari wanayo zaidi ya miaka 29 tangu mwaka 1992, lakini mpaka leo huwezi ukapima. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika kuchangia mpango huu. Vipo vipaumbele ambavyo vimeainishwa katika Mpango huu ikiwa ni pamoja na kipaumbele cha kilimo, kipaumbele katika Sekta ya Madini. Naomba niwarejeshe katika Mpango huu hususan katika ukurasa ule wa 34. Naanza kuchangia upande wa Utawala Bora. Nina uhakika kwamba huu nao ni msingi katika kutekeleza Mpango huu na msingi ambao unaweza ukatupeleka katika mafanikio katika Mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua zimekuwepo jitihada kubwa na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais alijaribu kuangalia akaona kwamba upande huu ni lazima tuushughulikie, ndiyo maana ameanza kuboresha sekta hii upande wa TAKUKURU kama chombo ambacho kinaweza kikasimamia na kuhakikisha kwamba pia utawala bora unafanyika, Mahakama na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze dhahiri kwamba pale ambapo Serikali itaweza kwenda sawasawa na kusimamia Mipango hii kwa umakini kwa kuzingatia Utawala Bora nina uhakika kwamba tunaweza kufanikiwa. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais kwa kutambua kwamba ipo mianya ambayo inasababisha tusiweze kupata mapato vizuri, lakini kwa lengo la kutaka kuimarisha utawala bora kwa maana ya kuziba mianya ya rushwa, kwa makusudi na kwa dhamira ya dhati akasema kwamba lazima sasa aanzishe Mahakama ya Mafisadi ya kushughulikia mafisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mkakati mahususi ambao utakapoenda kutekelezwa tuna uhakika kwamba Tanzania mpya itaonekana na Mpango huu utaweza kutekelezwa kwa umakini. Kwa sababu kwa kuziba mianya ya rushwa maana yake ni kwamba pia makusanyo ya Serikali yataweza kuongezeka. Makusanyo yatakapoongezeka, maana yake ni kwamba mipango hii itaweza kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaaminishe Watanzania na ninyi mtakubaliana na mimi kwamba kazi ya kiongozi ni kuonyesha njia na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tayari ameonyesha njia kwamba anayo dhamira ya dhati ya kuonyesha kwamba makusanyo yanapatikana, anayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba mipango hii inatekelezeka. Tunaongelea siku 100 za utendaji kazi wake, lakini matokeo tumeyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongeze Baraza la Mawaziri ambalo ameliunda, kwa sababu kwa kipindi hiki kifupi cha miezi miwili, mitatu tumeona matokeo ya kazi wanayoifanya Mawaziri hawa. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuwapongeza kwa sababu hii inaonyesha mwelekeo tunakokwenda kwamba itaweza kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika suala zima la madini. Tunajua kwamba eneo hili ni eneo ambalo ni nyeti na ambalo tuna uhakika na kuamini kwamba likisimamiwa vizuri linaweza likaendelea kuboresha na kuinua uchumi wa Tanzania.
Katika jimbo langu la Ngara yako madini adimu, madini ya Nickel, madini ambayo yanaifanya Tanzania iingie kwenye ramani ya dunia kuwa na deposit kubwa ya Nickel duniani kama siyo ya kwanza itakuwa ni ya pili. Ndiyo maana naunga mkono ujenzi wa reli ya kati pamoja na reli inayotoka Dar es Salaam kuja Isaka, kwenda Mwanza, Tabora, Kigoma, lakini pia mchepuko wa kutoka Isaka kuja Ngara ili kusudi mradi huu uweze kutekelezeka na nickel hii iweze kusafirishwa kwa ajili ya kupelekwa sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu tunategemea kwamba ni mkubwa lakini ambao wananchi wa Ngara kwa muda mrefu wamekuwa wakiuangalia kama tumaini lao kwa ajili ya kusababisha ajira. Tangu mwaka 1973/1974 exploration ilianza. Tulitegemea miaka ya 2010/2012 kwamba mradi huu ungeanza lakini mpaka sasa hivi haujaanza. Kulikuwepo na excuse ya kwamba hakuna umeme. Nampongaza Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Profesa Muhongo, na timu yake akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wamejitahidi kuhakikisha kwamba sasa umeme unasambazwa katika Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naongea na Meneja wa Kanda, TANESCO mchana huu akahiadi kwamba tayari Ngara inaunganishwa kwenye grid ya Taifa na bahati nzuri kwa Mpango ambao unaanza Januari mwaka huu, Ngara imepewa kipaumbele kwenye kuunganishwa kwenye grid ya Taifa. Bado pia tuna mradi mkubwa wa umeme katika maporomoko ya Rusumo, mradi ambao unashirikisha nchi tatu; Rwanda, Tanzania na Burundi. Kwa hiyo, naamini kwamba Ngara itaweza kupata umeme wa kutosha na ni eneo ambalo linaweza likawekezwa. Naomba mgodi huu wa Kabanga Nickel uangaliwe na uweze kuanza mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye suala la afya. Tuna hospitali moja tu ya Wilaya ambayo inahudumia zaidi ya watu takriban 400,000 lakini kipo Kituo cha Afya ambacho tangu mwaka 2006 Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara iliweza kuomba kupandishwa kuwa hospitali na Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, mwaka 2008 alitangaza kiwa hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeandika barua mara kadhaa kwa ajili ya kuomba usajili wa kituo hiki kiweze kuwa hospitali; ni hospitali inayotegemewa kwa sababu ina vigezo vyote vya kuitwa Hospitali na barua ya mwisho ilikuwa ni ya mwaka 2013. Nimebahatika kukutana na Naibu Waziri wa Afya na amekubali kulishughulikia hili, naomba liweze kushughulikiwa haraka iwezekanavyo ili kuweza kunusuru afya za wana-Ngara ili Hospitali hii ya Nyamiaga iweze kutambulika kama hospitali na iweze kupata mgao ili iingizwe kwenye bajeti kwa ajili ya kuhudumia wananchi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni pamoja na Kituo cha Murusagamba ambacho Mheshimiwa Rais alishatangaza rasmi kwamba sasa kianze kupanuliwa kwa ajili ya kuwa hospitali kulingana na jiografia ya Jimbo la Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze pia katika suala la maliasili. Tunajua kwamba Halmashauri zina vyanzo vyao vya mapato. Kwa mujibu wa Sheria ya Maliasili, Jimbo la Ngara lina hifadhi mbili; Hifadhi ya Burigi na Hifadhi ya Kimisi. Hifadhi ya Burigi imeingizwa kwenye gazette la Serikali tangu mwaka 1974; Kimisi imeingizwa kwenye gazette la Serikali mwaka 2005. Kwa mujibu wa sheria hiyo kuna tozo ya asilimia 25 ambayo inatakiwa ingie kwenye Halmashauri kama own source, lakini kwa miaka yote hiyo kwa hifadhi zote hizi mbili hakuna hata senti tano ambayo imeingia kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri husika kwamba tozo hii ya asilimia 25 ianze sasa kuingia kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, lakini pia hata arrears kwa miaka yote hiyo ambayo haikuweza kutolewa kama tozo kwa ajili ya kuimarisha Halmashauri ya Wilaya ya Ngara iweze kutolewa kwa ajili ya kuongeza pato la Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nangana na waliotangulia, kwamba lazima retention hii iweze kukusanywa kwa ajili ya kuweka kwenye mfuko…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Gashaza, ahsante.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)