Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Bukombe kwa kunichagua na kunituma niwe mwakilishi wao katika nyumba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana aliyewasilisha Mapendekezo ya Mpango ambao tunaujadili hivi sasa. Mapendekezo ya Mpango huu tumeletewa ili tuweze kuyaboresha, nami naomba niboreshe katika maeneo kadhaa kwa sababu ya muda, ili tuweze kuboresha zaidi Mpango huu kwa masilahi ya watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, naomba sana, tunapokuwa tunaangalia namna ya kukuza uchumi wa nchi, ni lazima tuangalie zaidi upatikanaji wa ajira kwa vijana. Nchi hii ina vijana wengi sana, asilimia zaidi ya 40 ni vijana ambao wanaweza kuajiriwa au ni nguvu kazi ya nchi hii. Hawa wasipowekwa maalum kwenye Mpango, namna gani watapatiwa ajira na tukafanya projection ni wangapi watapata ajira kwa Mpango huu, tutakuwa tunachelewesha kukua kwa uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna pekee ya kuweza kuwapatia vijana hawa, mathalan wa Bukombe ili uweze kuwapatia ajira, ni lazima uwatengee maeneo ya kuchimba dhahabu. Bukombe ndilo eneo pekee katika Mkoa wa Geita ambapo maeneo mengi yana dhahabu nyingi, lakini vijana wa Bukombe hawajapatiwa maeneo ya kuchimba dhahabu. Vijana hawa hawawezi kuielewa Serikali kama hawajapatiwa maeneo ya kuweza kufaidi rasilimali za nchi ambazo Mungu amewapatia na wamezaliwa wamezikuta hapo. Wakati umefika Mheshimiwa Waziri tuje na Mpango wa kuangalia namna gani vijana wanapatiwa maeneo ya kuchimba dhahabu katika Mpango wetu huu tulionao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la umeme. Watu wengi hapa wamezungumza, wamepongeza uwepo wa umeme wa REA. Sisi tuna REA I na REA II, mpaka sasa, lakini Wilaya ya Bukombe haijawahi kupata hata awamu moja ya umeme wa REA.
Nakuomba sana Mheshimiwa Profesa Muhongo na Naibu Waziri wako, nafahamu ninyi ni watu wasikivu, mtusaidie Bukombe na sisi tupate umeme wa REA. Haina maana nimesimama hapa kama Mbunge, wenzangu wanashangilia umeme na wewe Mheshimiwa Profesa Muhongo ulisema, sitaenda REA III mpaka viporo vya REA I na REA II viishe, wakati mimi hata REA I na REA II sijawahi kuiona! Mheshimiwa Profesa Muhongo nakusihi sana, Bukombe uitazame kwa jicho la huruma. Tunahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Uyovu kuna Kituo cha Afya, kinafanya huduma kubwa ya kuhudumia watu, kinahudumia Wilaya ya Bukombe, kinahudumia Wilaya ya Chato, kinahudumia Wilaya ya Biharamulo, lakini hakuna umeme pale. Madaktari wangu pale wanafanya operation kwa tochi. Jana nimepigiwa simu, wanazalisha mama mmoja wanatumia tochi. Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana utusaidie umeme kwa ajili ya watu wa Bukombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba niipongeze sana Serikali kwa kuja na Mpango wa elimu bure kwa Watanzania. Mpango huu kwa maoni yangu naona kama ukichelewa. Kuanzia sasa watoto kuanzia darasa la kwanza mpaka la kumi na mbili watapata elimu bure. Ninafahamu wako watu wengine ambao wanaweza wakapuuza Mpango huu kwa kuona kwamba ni siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikisheni, tulipoanza na Mpango wa kujenga Shule za Kata, watu walitokea hapa wakapuuza namna ile ile, lakini leo ninavyosimama hapa na kuongea mbele yako, Shule za Kata ndiyo zimetusaidia kupata Wataamu wengi wa nchi hii. Nitakupa mfano kwenye Wilaya yetu ya Bukombe, Shule ya pili kwa kufanya vizuri Kidato cha Sita ni Shule ya Kata ya Lunzewe Sekondari, ambayo watu wakati tunaanza walianza kupuuza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, tusukume na namwomba sana Mheshimiwa Simbachawene, endelea kutuelimisha Watanzania. Tunavyoanza siyo rahisi! Siyo rahisi tunavyoanza tukaenda na mafanikio ya moja kwa moja. Tutapata setbacks hapa na hapa, lakini kadri tunavyoendelea ndivyo tutakavyokuwa tuna-improve ili twende mbele zaidi kwa maslahi ya Watanzania.
Mheshimwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Mawaziri, naomba sana, sasa tumeshafanya vya kutosha; tumejenga madarasa, sijawahi kuona Mpango wa kuwasaidia Walimu, kuwa-motivate Walimu kufanya kazi vizuri. Walimu wa Tanzania wanafanya kazi katika mazingira magumu. Walimu wa Tanzania bado wanalipwa kwa viwango ambavyo havikidhi maisha yao kwa siku 30. Walimu wa Tanzania bado wana waajiri wengi na wanawajibika kwa watu wengi wakati wao ni watu wale wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeomba na tumelia kwa muda mrefu Walimu wapatiwe Tume ya Utumishi wa Walimu. Wamepatiwa, sasa ninaomba Serikali iharakishe mfumo wa kurekebisha Kanuni hizo zinazotengenezwa ili Tume ya Utumishi wa Walimu ianze kufanya kazi tuwahudumie Walimu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mfumo wa Elimu ndugu zangu umegawanyika katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni Mtaala, sehemu ya pili ni udhibiti wa ubora na sehemu ya tatu ni Examiner au Mtahini yule anayeangalia matokeo ya kile walichojifunza Wanafunzi. Upande wa mtaala ambako Mwalimu ndiko yupo, hakuna nguvu kubwa iliyowekwa kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaangalia madarasa, ndiyo! Tunaangalia madawati, amina! Tunaangalia chaki, sawa! Lakini lazima tumwangalie Mwalimu ambaye ndiye mhusika Mkuu na msimamizi mkuu wa Mtaala wa Elimu katika nchi hii. Walimu hawa wanapokuwa wanalalamika na kulia, msitarajie tutapata matokeo ya uhakika. Tunaweza tukawalazimisha wakae darasani, watafanya kazi lakini nataka niwaambieni, motivation ya Walimu wa nchi hii bado iko chini. Iko kazi tunapaswa kufanya, tuje na Mpango Waziri wa Fedha, mpango maalum wa kutengeneza frame work ya motivation ya Walimu. Nchi nyingine zimeshafanya jambo hilo na zimefanikiwa sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, jambo hili tuliangalie kwa jicho la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pale Bukombe kuna zao maarufu sana. Asali bora nchi hii inatoka Bukombe. Asali inayovunwa Bukombe na watu wamejiunga kwenye vikundi, wanafanya kazi kama yatima. Wako kwenye Vikundi watu 6,000, wanavuna asali zaidi ya lita milioni moja kwa mwaka, lakini hakuna hata Kiwanda kimoja cha kusindika asali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na tulishazungumza, tuangalie namna ya kupata Kiwanda cha Kusindika Asali ya watu wa Bukombe ili asali yao ipate bei kubwa, ipate soko la uhakika, tubadilishe maisha yao kwa kuwapatia fursa ya kuendeleza maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, vile vile Wilaya ya Bukombe tuna mifugo mingi, lakini mifugo hiyo haichangii kwenye pato la Taifa. Nchi hii ina mifugo milioni 25, lakini ukiangalia takwimu kwa hali ya uchumi, kwa taarifa ya hali ya uchumi ya Juni, 2015, utaona nchi hii pamoja na kuwa na mifugo milioni 25, tumeuza nje ya nchi mifugo 2,139 na tumepata Shilingi bilioni 34 peke yake. Tuna mbuzi milioni 15, lakini tumeuza mbuzi 264; tumepata Shilingi bilioni 1.7.
Nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, utakapokuja kujumuisha, uje na Mpango wa kutusaidia wafugaji hasa wa Kanda ya Ziwa, wafugaji wa Tanzania, tupate malisho, tumechoka kukimbizana na Wahifadhi wa Wanyamapori, ma-game kupigana kila siku na kuanza kuhangaishana kutozana vifedha vidogo vidogo hivi, wakati tuna uwezo wa kuchangia kwenye Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, nimekuwa na Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Ramo, mtu msikivu sana. Alikuja Jimboni kwangu, akazungumza na wafugaji pamoja na Waziri wa Mifugo, walituambia mambo mengi ya kufanya, lakini cha ajabu, baada ya kauli zao kutoka, siku mbili, tatu, kauli ile ikabadilika kabisa. Wale wafugaji sasa hivi huko ninavyoongea wanatimuliwa kama wakimbizi kwenye nchi yao. Naomba Serikali tuangalie namna ya kuwasaidia watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tatizo la maji, Wilaya ya Bukombe bado tuko nyuma sana. Watu wanaweza kusema kwenye makaratasi asilimia 30 ya watu wanapata maji, hapana. Wanaopata maji Bukombe ni chini ya asilimia 30 na actually ni chini ya asilimia kumi. Miradi iliyopo mingi imeshasimama. Mradi wa Msasa haufanyi kazi, Mradi wa Kilimahewa haufanyi kazi ipasavyo, pale Ruhuyobu tuna miradi miwili; mradi mmoja peke yake ndiyo unaofanya kazi, mradi mwingine umesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ni kazi ambayo tunahitaji tuione. Nami namwomba Mheshimiwa Waziri wa Maji, unapokuwa na kale kampango ka kupeleka maji Tabora, Nzega, Bukombe pale ni karibu, ukipitia Mbogwe, tunapata maji ya Ziwa Victoria, biashara hii inaisha. Nitakapokuwa nikisimama hapa, Mheshimiwa Waziri wa Maji, nitakuwa nazungumza mambo mengine, siyo maji. Saa imefika, naomba mtusaidie wananchi wa Bukombe tuweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, najua muda wangu umekwisha.