Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Awali ya yote niwashukuru akinamama wa Mkoa wangu wa Morogoro kwa kunipa fursa ya kuwa mwakilishi wao. Hali kadhalika nikishukuru Chama changu kwa kuniona kwamba nafaa kuwakilisha katika Bunge hili, bila kuwasahau wapambanaji wenzangu wa ITV. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia vizuri sana Mpango ulioletwa mbele yetu. Yako mambo mengi sana, lakini hakika mambo haya nilikuwa nikijiuliza tu, mikakati na mipango mingi kiasi hiki tunaifanya kwa ajili ya watu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikapata jibu ni kwa ajili ya wananchi na maendeleo ya Taifa lao, lakini hivi tunavyojadili mambo haya muhimu ambayo yanakwenda kulenga kuleta maendeleo ya wananchi, tukiwa tumejifungia, lakini wananchi hawajui ni kitu gani kinachoendelea, kwa kuzuwia chombo cha umma kutangaza matangazo haya moja kwa moja, naona kama hatuwatendei haki wananchi. Hali kadhalika naona kama tutakwama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mataifa mbalimbali yaliyoendelea ni yale ambayo yametumia vizuri vyombo vya Habari. Mfano Malaysia, ukienda ukimuuliza hata dereva tax, National Goal ni ipi na ni njia gani ya ku-achive National Goal? Watakueleza kwa sababu wako informed na wanatumia vyema vyombo vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunakuja na Mpango hapa tunasema ni kwa ajili ya wananchi na maendeleo ya Taifa, lakini wananchi hawa hawana fursa ya kupata na kuelewa tunajadili nini! Tumezungumza mambo mbalimbali ambayo ni ya vyanzo vipya vya mapato, tumezungumza habari ya mambo ya retention, lakini mambo hayo hamuoni kama wananchi wangepata fursa ya kufuatilia moja kwa moja kujua na sisi tunafanya nini, ingeweza kutusaidia pengine mipango hii ikaweza kutekelezeka kwa uzuri na kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata taarifa hapa kwamba, TBC Chombo cha Umma ambacho kilianzishwa kwa lengo la kutoa huduma kwa umma; TBC inasema ni gharama kuendesha matangazo haya ya moja kwa moja! Hata hivyo, tumekwenda mbali zaidi kuangalia mchakato, ukiaangalia Air Time kwa TBC kwa kipindi cha saa moja gharama yao ni 7,080,000/=, lakini tukiangalia saa ambazo tumekuwa tukizitumia hapa kuanzia masaa sita mpaka saba kuendesha Bunge live. Pia tumejaribu ku-calculate kwa vipindi vinne vya Bunge kwa maana ya vipindi vitatu vifupi na kipindi kimoja cha Bunge la Bajeti ambacho ni kirefu, tukapata ni sawa na saa 290 za kurusha Air Time na ukizidisha unapata 2.2 billion na siyo 4.2 kama tulivyoelezwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika tunakumbuka Serikali, kamera tunazoziona huku zilifungwa na Star TV enzi hizo, lakini hivi sasa ikatokea mambo mengine mengine hapo wakasema siyo vema ni lazima taarifa hizi zirushwe na vyombo vya umma. TBC ikajengewa uwezo kwa kupewa bilioni 4.6 inunue vyombo vya kisasa na kutumia kamera hizi ambazo zimefungwa na Star TV, lakini matokeo yake hiyo 4.6 haijafanya chochote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii TBC wanakuja na crew ya watu 20 kurusha live hapa, kitu ambacho kinaongeza gharama. Hamuoni sasa ni wakati wa kuruhusu hivi vyombo binafsi vifanye kazi vizuri, kuhakikisha vinasaidia kusukuma mipango hii kama TBC imeshindwa? Hamuoni kama sasa ni wakati wa Serikali kupunguza hivi vikwazo kwa vyombo hivi binafsi na kupewa hizi ruzuku ambazo TBC inashindwa kufanya kazi? Ruzuku zielekezwe kwa vyombo binafsi vifanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niende kwenye mipango mbalimbali niliyoiona kwenye kitabu hiki; nimeona habari ya reli, miundombinu, barabara, lakini sijaona mahali popote ambapo tumezungumza jinsi ya kusaidia wananchi ambao wameathirika kutokana na miundombinu hii. Nikizungumzia Kilosa hivi sasa kuna wananchi wanaishi kwenye mahema kwa zaidi ya miaka mitano, wameathirika kwa sababu reli ya kati ilikatika katika eneo la Godegode, tuta la Kidete lilivunjika ambalo nimeona mpango mnalitengeneza, lakini kuvunjika kwa tuta lile ambalo lilisababisha mafuriko kwa wananchi hamjaweka mpango wa kuwapa hata viwanja wananchi leo hii, tangu 2010 wanaishi kwenye mahema, wakiwemo wananchi wa Kidete, wananchi wa Mateteni na wananchi wa Magole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni wakati umefika wakati tunaandaa mipango hii tuwafikirie na wananchi hawa ambao waliathirika kutokana na kuharibika kwa miundombinu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mna mpango wa kufanya Tanzania kuwa ni Tanzania ya Viwanda. Tunavyozungumza hivi Morogoro viwanda vilikuwa vingi, leo hii viwanda mbalimbali vimekufa, lakini hamjatueleza kwamba, viwanda hivi vitafufuliwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha Canvas, kiwanda cha UNAT cha matunda ambacho akina mama walikuwa wanatumia kwa ajili ya matunda yao! Leo hii akinamama ndiyo wanaotembea na mabeseni kichwani, haikuwa kazi yao! Kiwanda cha Asante Moproko, Kiwanda cha Ceramic, Kiwanda cha Tanarries, ambavyo vyote hivi vilikuwa vinatoa ajira kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye suala la maji; limezungumzwa kila mahali, lakini Mkoa wa Morogoro ni Mkoa ambao una mito mingi sana, lakini Mkoa wa Morogoro ndiyo unaoongoza kwa kukosa maji. Nikianza katika Manispaa ya Morogoro pekee, ambayo kwa sasa inategemea Bwawa la Mindu ambalo limejengwa mwaka 1984 wakati huo idadi ikiwa ndogo sana; leo hii Serikali imekuja na mkakati mpya wa kujenga Bwawa la Kidete, hatukatai! Imekuja na mpango mpya wa kujenga mabwawa mengine ya Vidunda, hatukatai! Lakini kweli mipango hii ni kwa manufaa ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii inatumia mito ya Morogoro ambayo maji yatakwenda sehemu nyingine, sisi wana-Morogoro wenye mito yetu tunabaki bila maji! Nenda katika Manispaa nimesikia majibu ya Naibu Waziri leo asubuhi, Kihonda, Area Five, Kilakala, kote huko hakuna maji japo anasema kwamba, mpango wa MCC ulisaidia, lakini tunavyozungumza hivi sasa huo mpango wa MCC wananchi hivi sasa ni kuandamana kila wakati wakienda MORUWASA kudai maji! Kwa nini sasa kwa mito hii mingi wasifikirie kujenga bwawa jipya kwa kutumia hii mito yetu iliyopo, ili kuhakikisha kwamba wanamaliza tatizo hili la maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye masuala ya migogoro ya wakulima na wafugaji, nazungumza hili kwa masikitiko makubwa. Hivi karibuni kupitia vyombo vya habari tumesikia jinsi mauaji ya mifugo na wananchi yakiendelea katika Wilaya ya Kilosa na Mvomero.
Hivi karibuni nimetembelea vijiji vya Kunke kule Mvomero, wananchi wa vijiji sita wamechangishwa shilingi mia tano kila mmoja eti kwa ajili ya kufanya operation ya kuwaondoa wafugaji. Kazi ya kufanya operation ya kuwalipa Polisi ni kazi ya wananchi? Wananchi kila mmoja alitozwa shilingi mia tano ili wawaondoe wafugaji, zoezi ambalo linapaswa kusimamiwa na Serikali kupitia Wizara husika, lakini leo hii wananchi wanaambiwa kama ninyi hamtaki migogoro hii basi wachangie ili wafugaji waondolewe. Hii ni kuendelea kuongeza uhasama katika makundi haya mawili kwa kuwa yote yanafanya shughuli halalli ambazo zinachangia pato kwa Serikali.
Tukirudi kwenye suala la Mpango wa NFRA wa kuuza mazao, hivi sasa Serikali imeanzisha soko la Kibaigwa ambalo linatoa huduma kuwezesha wakulima wa Morogoro, Dodoma na Manyara kufanya biashara ya mazao, lakini hivi sasa wakulima wa Morogoro hawapeleki mazao yao pale kwa sababu ushuru...
MWENYEKITI: Nakushukuru sana.
MHE. DEVOTHA MATHEW: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.