Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Na mimi kwa kuwa ni mara ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, namshukuru Mwenyezi Mungu, nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kuniteua kuwa mgombea wa chama hiki katika Jimbo la Manyoni Magharibi pia nawashukuru wananchi wakazi wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwa kuniamini na kunipa nafsi hii na leo nasimama mbele yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza tu moja kwa moja kwa sababu muda huu siyo rafiki sana, nianze na suala zima la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo haya ya Mpango yameonesha maeneo ambayo wataelekeza katika jamii yetu kusaidia maji. Jimbo langu ni miongoni mwa Majimbo machache sana ambayo maji hayapatikani kwa asilimia ya kutosha; ni chini ya asilimia 10.
Naomba sasa kwa Waziri husika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi walimpa kura nyingi, zaidi ya asilimia 80 na alipokuja pale aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi na Mji wa Itigi kwamba atasaidia maji katika kipindi kifupi kijacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Waziri mhusika alione hili ili kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa mpango wa elimu bure. Mpango huu una tija na wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi wamenituma niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kufanya mpango huu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo langu wana tatizo kubwa sana la afya. Tuna Kata 13 lakini Kata zenye vituo vya afya ni mbili. Tunategemea sana Wamisionari; na bila Wamisionari, wananchi wa Jimbo langu wasingekuwa wanaongezeka kwa kiasi hiki ambacho wanaongezeka kwa sababu hata watoto wangekuwa wanakufa mapema. Jiografia yake ni ngumu, lakini vituo vya afya hakuna, zahanati zipo chache; kwa kushirikiana na TASAF zilijengwa lakini hazina matabibu. Naomba sana, Mheshimiwa Waziri yuko hapa, alifanyie kazi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi pia ya Mheshimiwa Rais. Tunaitegemea sana hospitali ya Wamisionari ya Mtakatifu Gaspar. Hospitali ile ina gharama kubwa sana. Wakati alipokuja katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka wa 2015 aliwaahidi wananchi wa Jimbo langu kwamba atalipa mishahara yote ya watumishi wa hospitali ile, atatoa ruzuku kwa ajili ya vifaa tiba na ataleta Madaktari Bingwa. Pia atafanya mgao kutoka MSD ili tu kusaidia wananchi wa Jimbo lile ambao hawana hospitali mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya iko mbali; naomba sana ahadi ya Mheshimiwa Rais itekelezwe, tena katika kipindi kifupi. Wananchi tuna taabu na tunakufa kwa sababu ya gharama ni juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuunganisha mikoa kwa barabara za lami; Mkoa wa Singida umeunganishwa na mikoa mingine; lakini Mkoa wa Singida kuunganisha na Mkoa wa Mbeya, ni kitu ambacho kinashangaza. Mimi kama kiongozi ambaye nimetokana na wananchi wale, leo hii nimepokea message nyingi kwamba barabara baina ya Itigi na Rungwa, imekatika, hakuna barabara. Kikosi kazi kiko pale lakini hakuna kinachofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii jana amenipa barua kwamba wanatafuta fedha katika barabara hii ya Mkiwa – Rungwa hadi Makongorosi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe kwamba barabara hii amekuwa akiisemea toka Mbunge wa wakati ule Mheshimiwa Iwvata. Mheshimiwa Lwanji katoka hapa miaka kumi, bado ni ahadi zile zile. Naomba sasa mtekeleze ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyowaambia wananchi wa Itigi na Jimbo la Manyoni Magharibi kwamba katika utawala wake, atajenga barabara ile kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuwa una-wind-up hapa atuambie ni lini barabara ya kutoka Mkiwa – Itigi – Rungwa itajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Wabunge walioongelea kuhusu reli ya kati, nami Jimbo langu reli inapita pale na wananchi wangu wananufaika sana na reli inapopita pale. Sisi tunatumia usafiri ule wa reli kwa ajili ya kwenda maeneo jirani, lakini pia hata kwenda Kigoma. Mji wa Itigi ni mji ambao tumechanganyika, kwa hiyo, tunatumia sana reli kwa maslahi ya jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kilimo, tufike mahali sasa tuondokane na kilimo hiki cha mvua. Wakati mwingine mvua zinakuja kidogo wakati mwingine zinazidi. Maeneo ya Itigi ni mazuri, tukiweka miundombinu tu ya Irrigation Schemes yoyote, deepwell ikifanyika pale, maji yatapatikana ya kutosha na tunaweza tukaanzisha irrigation scheme, tukaondokana na utaratibu huu wa kutegemea mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mpango wa matreka ambao ulikuwepo katika awamu iliyokwisha. Wananchi wa Jimbo langu hakuna hata mmoja aliyefaidika na manufaa ya Serikali yao; na wao ni waaminifu na ni watiifu, hawajawahi kufikiria kuchagua chama kingine zaidi ya CCM. Hivi tunavyozungumza Halmashauri ya Itigi ni mpya, lakini Madiwani wote ni wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi walione hili kuwasaidia wananchi. hawa ambao ni waaminifu! Waswahili wanasema, chanda chema huvikwa pete. Sasa tunavikaje pete ambacho siyo chanda chema? Tuwaone hawa wananchi ambao ni waaminifu kwa Serikali hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo; kuna changamoto kubwa sana kwa bei ya mitamba katika mashamba ya Serikali. Bei ya mitamba ni kubwa kuliko bei ya ng’ombe ambaye unamuuza mnadani. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alifuatilie hili ili mitamba ishuke bei, watoe ruzuku ili wananchi tununue, lakini pia madume ya kuhamilisha mifugo ili tutoke katika…
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Hii ya kwanza eh!
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.