Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami nipate kuchangia Mpango wa Taifa wa Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu, muumba mbingu na ardhi kwa kunipa kauli na pumzi ya bure ninayopumua kwa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mara yangu ya kwanza kusimama kuchangia. Nakishukuru sana chama changu na viongozi wangu wa Kitaifa kwa kunirejesha tena huku ndani kwa awamu ya pili. Mwenyezi Mungu awabariki sana na awape umri katika maisha yao na utendaji wao wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu nitajikita sana kwenye masuala ya ulinzi na usalama. Tunapeleka vijana kwenye makambi ya Jeshi, kwa mfano JKT, vijana wanaenda kupata mafunzo mbalimbali ya kijeshi, lakini imekuwa katika kundi hili wanachukuliwa vijana wachache sana na vijana wengine wanakuwa hawana ajira. Sasa naomba huu Mpango uelekezwe kwenye Wizara ya Ulinzi na Usalama waangalie ni namna gani ya kuboresha na kuwajengea vijana wote kwenye makambi ya JKT kuhakikisha kunapatikana viwanda vya ujasiriamali kwa ajili ya hawa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia haya makambi, pia kuna baadhi ya makambi mengine ambayo yamepakana na bahari, mengine yamepakana na maziwa. Pia hawa vijana wanaohitimu mnaweza mkawajengea na mkawapa angalau uvuvi wa bahari, wakaenda zao kujiajiri wenyewe. Sasa mnavyowarudisha vijana hawa mitaani, vijana hawa wamekuwa wanakuja mitaani hawana kazi, ndio hawa mnakuja tena kuwarubuni kwa mambo mengine na ndio wanaokuwa majambazi sugu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnajikuta mnawatumia kwenye vikundi ambavyo havieleweki! Mnawatumia sana kwenye mambo ya siasa! Sasa nawasihi ndugu zangu Chama Tawala, mhakikishe mbegu mnayoipanda, ndiyo mtakayoivuna.
Leo hii mmesahau vikosi vya ulinzi na usalama mnawawezesha kipindi cha uchaguzi. Mkishawawezesha, basi, lakini leo hii vikosi hivi wengi hawana sehemu za kukaa, wanakaa uraiani. Angalieni ni namna gani Mpango huu kuhakikisha vikosi vya ulinzi na usalama vinapata makazi bora ya kuishi na vinaboreshewa mishahara yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia yanayoendelea sasa hivi huko Zanzibar, kila kiongozi atakumbukwa kwa matendo yake. Kiongozi na uongozi ni dhamana kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Leo hii sisi kama watu waliotokea Zanzibar tutamkumbuka sana Rais Amani kwa mambo yake aliyoyafanya mazuri kutuunganisha na tukaja tukapiga kura ya umoja wa Kitaifa na tukasikilizana na tukazikana na tukawa tunafahamiana. (Makofi)
Leo hamtaki kusikia la mwadhini wala mchota maji kanisani, mnakwenda tu. Tukumbuke amani tuliyokuwa nayo ni tunu ya Taifa, lakini amani hii tunaichezea, ni kama vile shilingi ikishadondoka chooni, kwenda kuiondosha shilingi ile unapata taabu sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmeona kimya; ukimya wa Wazanzibari, lakini siyo ukimya. Siasa ya Zanzibar uliza waliopita Zanzibar. Tulikuwa Wabunge wengi sana ndani ya Bunge hili waliotokea Zanzibar, wengi hawakuweza kurejea. Hawakuweza kurejea! Wabunge walioweza kurejea kama akina Mheshimiwa Masauni watajua ni kwa nini hawakurejea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamwona Dkt. Mwinyi anakuwa mtulivu na mwenye hekima na busara, tunapomwambia fuatilia jambo fulani, anafuatilia. Ndiyo maana mnamkuta kila siku anarudi kwenye kiti chake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wasizibe masikio yao, wayazibue. Naomba viongozi wote wa Jamhuri ya Muungano, Rais Kikwete alianza sana mambo mazuri ndani ya Zanzibar, lakini sijui ni shetani gani aliyekuja akaingia katikati akatupa mkono Wazanzibari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuhakikishe kunakuwa na Serikali ya umoja wa Kitaifa ambayo ina maridhiano bila kupigana, bila bughudha. Miaka mitano siyo mingi, mtarudia tena uchaguzi na wananchi wa Zanzibar watataka kumpa wanayemtarajia. Niondoke hapo, hilo somo litakuwa limeeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kanda zote za Pwani, tuseme mpaka kule kwetu; ukishika Zanzibar na Pemba, bado kuna umaskini, kuna watu ambao hawawezi kujenga nyumba za kisasa. Tuangalie kama mji wa Bagamoyo ni mji wa kitalii, lakini Mji wa Bagamoyo mpaka sasa hivi umesahaulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani kuendeleza mji wa Bagamoyo ili uweze kuwa ni mji wa Kimataifa kwa utalii na kuhakikisha majengo yote ya Bagamoyo yanaboreshwa? Magofu yote yale ya utalii na yale ya zamani yaboreshwe ili kutangaza mji wa Bagamoyo upate kuwa mji wa kitalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, hata Hospitali ya Bagamoyo, bado hospitali ile mashuka hayakidhi haja; wagonjwa ni wengi na jengo lile ni chakavu. Kwa hiyo, naomba muupe Mji wa Bagamoyo kipaumbele kutokana na kwamba ni mji wa kitalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe ni namna gani tunatangaza Mji wa Bagamoyo, kwa sababu ukitoka Bagamoyo kuna majumba ya Mji Mkongwe ambayo na Bagamoyo yapo; ni majumba ambayo yanakuwa ni kivutio sana kwa utalii. Majumba haya sasa mengine yamekuwa chakavu na mengine hata katika kujengwa ramani zile zinabomolewa, zinajengwa ramani nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusimamie Mji wa Bagamoyo utangazwe katika sekta ya kitalii na majumba ya makumbusho pia yajengwe na vitu vya kale vyote vienziwe ili tupate watalii wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,…
MWENYEKITI: Ahsante sana.