Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni

Hon. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kuleta Azimio hili hapa Bungeni, kwa sababu najua jambo hili ni jambo lenye manufaa makubwa sana kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa Kiongozi mwenye dhamana katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Azimio hili kwetu tunalipokea kwa mikono miwili, nikijua wazi kwamba vijana wetu wanaosoma shule za msingi na sekondari, hivi sasa tunapojielekeza katika suala zima la michezo mashuleni, sasa Azimio hili linatupa nafasi nzuri sana ya kuwaandaa vijana wetu katika michezo bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia kuhusu vijana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na timu yake. Juzi tuliwashuhudia vijana wetu wa Serengeti Boys kule India wakifanya maajabu makubwa sana. Mheshimiwa Naibu Waziri, ikikupendeza sana vijana wale inapaswa tuwalete hapa Bungeni tuwatie moyo, walifanya kazi kubwa kwa kushiriki michezo ile, katika michezo yote hakuna mchezo waliofungwa, walifanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jana vilevile nilishuhudia katika vyombo vya habari, timu yetu ya Azam ya Vijana, walipokuwa wakishirikisha timu za Uganda, Kenya na hapa Tanzania, katika timu yao ni kwamba michezo yote wameweza kufanikisha, wameshinda michezo yote na kupata kombe lile, imeleta heshima kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Ofisi ya Rais, TAMISEMI ina jukumu la michezo ya UMISETA ambayo inaendelea hivi sasa, naomba tulipokee Azimio hili kwa moyo mkunjufu, nikijua kwamba katika michezo yetu hii, sisi kama Serikali tunaoasisi michezo mashuleni, vijana wetu hawa tukiwaandaa vizuri katika Azimio hili sasa, maana yake tutaweza kupata vijana bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, siku za usoni tujue vijana hawa ndiyo tunatakiwa sasa tuwalee vizuri katika suala zima la taaluma, huko baadaye tukapate Madaktari na Professors. Kama tusipokuwa na usimamizi mzuri katika eneo hili maana yake vijana leo hii wanaposhiriki michezo wataweza kutumia madawa haya, mwisho wa siku wanapofika sasa katika kutumia akili yao katika taaluma inawezekana tukawa na vijana wengi ambao watashindwa kufanya vizuri kimasomo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nampongeza sana, Azimio hili limekuja katika muda muafaka. Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba nimhakikishie wazi, kwa sababu tuna mtandao mpana wa vijana katika shule zote, tutahakikisha tunashirikiana na Wizara ya Habari na Michezo kuhakikisha kwamba jambo hili linatelekezwa vizuri katika shule zetu zote ili vijana wetu wanapokwenda kushiriki katika michezo, kwanza iwe ni ajenda ya kudumu katika michezo yote; kwamba wafahamu utumiaji wa dawa hizi siyo sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kwamba, kutoa maelekezo ya kutosha kwamba wao wawe Mabalozi wazuri kuhakikisha kwamba tunalea kizazi cha vijana ambao watakuwa wazuri wa kuelewa jambo hili la utumiaji wa madawa ya kuongeza nguvu katika michezo siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, langu lilikuwa ni commitment katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwamba tutashirikiana vema kuhakikisha kwamba Serikali yetu inakuwa ni Serikali ya mfano, kwa suala la utumiaji wa dawa katika kuongeza nguvu katika michezo halitoruhusiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia zote mia moja.