Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachangia Mpango huu au Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya mwakani yaani 2017/2018 ni vema sasa tukafika mahali tukaongea uhalisia ambao utatupeleka katika maendeleo ya kuisaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma vizuri sana Mpango huu, unaonekana kwa kweli ni mzuri, lakini mimi nina walakini kwa kuangalia mipango ambayo ipo na imeandikwa hapa hasa katika maeneo ya uzalishaji wa viwanda vidogo vidogo. Pia kuna mipango mikakati ambayo imeelezwa hapa katika mpango huu ambayo kimsingi nimekuwa nikisikia mimi kabla sijawa Mbunge na sasa nimeingia humu bado naendelea kuisikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kuna mpango huu kwa miradi hii ya Kinyerezi, mipango hii ya Special Economic Zone, ni kweli Tanzania tunahitaji umeme na tunaona maeneo mengi yana ukosefu wa umeme. Lakini tunaona kabisa hapa mpango huu unaonesha kwamba utakuwa na faida ya kuongeza megawati 600, lakini tumekuwa na mipango mingi hatuoni utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia miradi hii ambayo imeoneshwa kwenye mpango wa Serikali hapa, vituo vya biashara vya Kurasini imekuwa ikisemwa muda mwingi, lakini sasa ukiangalia fidia imeshatolewa na mamilioni yako hapa yanaoneka sitaki kuingia in detail, lakini hoja yangu ni hii tu Serikali imeshaweka fedha nyingi hapa sasa na muda unaanza kwenda, ituambie basi ni lini inaanzisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina wasiwasi unaweza ukabeba mpango huu ukaelekea tena mwakani kwa sababu naamini kwenye mpango uliopita ulikuwepo, Kurasini, Kinyerezi, viwanda vidogo vidogo ambavyo vimekuwa vikielezwa hapa na hii SEZ, tunapiga maswali kwa wale wengine ambao tunakaa mbali na maeneo haya. Umeme tunahitaji kweli, viwanda tunahitaji kweli lakini ni lini sasa unaanza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila tunapoona mipango tunategemea kwamba Serikali itakwenda kuifanya, tunaposoma vitabu hivi tunaamini kabisa mipango hii ya Serikali inakwenda kutekelezwa, lakini kinachotutia kichefuchefu ni kwamba tuna tatizo moja hapa kwetu la kutenda, tunatenda lini? Maamuzi tunayafanya lakini wakati wa kwenda kutenda hapo ndio tunaanza kuona danadana, leo, kesho, kesho kutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vizuri upande wa kilimo unaona kabisa mipango mizuri, ipo katika vitabu vyetu hivi na unaisoma vizuri sana, kwa mfano ukiangalia mpango wa kilimo umeiandika vizuri sana Mheshimiwa Mpango, je, wakati wa kwenda kutekeleza tunatekeleza kama tulivyoandika? Hilo ndilo tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiangalia kwa uhalisia wa mwaka huu, tunaposema tunakwenda kusaidia sekta ya kilimo wananchi wetu wanajua tunakwenda kweli kusaidia tukiwa tumeamua kwa sababu mpango huu umeelezwa humo, na Wabunge kazi yetu kubwa ni kuishauri Serikali, hapa tunaposhauri naomba ushauri huu uchukuliwe, na ukafanyiwe kazi wakati tumeamua kushauri, kwa sababu sisi ni Bunge na wao ni Serikali tunaamini ya kwamba tunafanya kazi katika three pillars of the one government (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tufanye kazi moja rahisi tu, tunapoingia huku tunaingia kama tuna vyama, lakini tunapokuja huku tunawakilisha wale wasiokuwa na vyama, na wale wenye vyama. Mimi naomba lingine niwashauri ndugu zetu wa upinzani mara chache tunapoingia humu, tunaanza kukashifiana kwa lugha ambazo sio nzuri, hizi lugha zinatuondoa kwenye mood wa kuangalia fact issues ambazo zinafanya sisi Watanzania kule waone kwamba tumekuja huku kuwatetea. Tunapojadili habari hii kwa mfano kilimo sasa, hali halisi mpaka sasa hivi kwa sisi Wabunge tunaotoka maeneo ya kilimo hakuna pembejeo, hakuna ruzuku sijui ni lini tutapata. Sasa tukianza kuongea hatuna maana ya kusema jambo lolote mbadala na hili, ni hali halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo kwa mfano, mimi kule nategemea kilimo, tunategemea mifugo, pembejeo za kilimo hazipo, Serikali imekwisha kuahidi, Mheshimiwa Rais alikwisha kusema je, hebu tuambiane mpango huu unaeleza pia, kuna fedha imetengwa, je tunapatiwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali halisi mvua zimeaza kunyesha je, hizi pembejeo tutakapopeleka baada ya mvua kunyesha; kwa mfano ukipeleka mahindi au ruzuku yeyote na pembejeo hizo, mbolea wakati msimu umeshapita unampelekea nani? Je, tukipata mwezi wa pili inafaa kupikiwa kande? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naomba tu tufike mahali tuende kwenye uhalisia wenyewe, lakini hata mkulima huyu, ukiangalia takwimu zinaonesha asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, angalia leo kilimo hiki hakimsaidii na leo kuna maswali mengi yameulizwa asubuhi kuhusu kilimo na hali inaonekana kabisa kilimo ndiyo tegemeo. Lakini ukiangalia miradi yote ya umwagiliaji imesimama tatizo ni hela hakuna, hapa imeandikwa vizuri sana, sasa nina-declare tunafanyaje ili kuisaidia nchi yetu kama tunashauri halafu yale ambayo tunashauri hayatekelezwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali yetu tunaipenda sana ninaona kabisa jitihada za Waziri, naona jitihada za Rais, naziona kabisa jitihada zinazofanyika, tukafanye kazi ya kufanya kazi ambayo tumeamua kuifanya kweli. Angalia wakulima sasa hivi wamechoka, sisi vijana ambao tumekuja kuwatetea vijana tumeanzisha SACCOS zetu kule lakini utaangalia nimshauri sana ndugu yangu Waziri Mpango, kuna kodi ambayo imeanza kuua katika maeneo yetu kule. Kodi hii inaenda kuwalenga wakulima wadogo wadogo wanaochajiwa VAT, tumeanzisha SACCOS, AMCOS katika maeneo yetu kule, lakini kodi hii ukiangalia ndiyo kodi ambayo Mheshimiwa Rais amesema kodi kero tuondoe. Hivi leo mkulima mmoja mmoja anadaiwa zuio la kodi hii haistahili na hii siyo sahihi.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali iangalie maeneo ya kuweka kodi na maeneo ambayo hayapaswi kuwekwa kodi. Tuliingia huku tukisema habari ya kodi kwa watalii kwenye maeneo yetu ya kule, lakini tazama leo tunaona athari zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu wakati mwingine tunaposhauri kama Wabunge Serikali ichukue ule ushauri ikaufanyie kazi, bahati nzuri Tanzania tuna wasomi leo, tufanye research tuone kabisa je haya tunayoshauriwa na Waheshimiwa Wabunge ndiyo hasa yale ambayo wanaona kwa ushauri wao na kama wanakataa wakatae kwa hoja na sisi tunapoeleza tunaeleza kwa hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye suala la miundombinu imeelezwa hapa, uboreshaji wa miundombinu, imeelezwa habari ya ATCL, imeelezwa habari ya TAZARA, imeelezwa habari ya ndege na yameelezwa mambo mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine naangalia ninapoingia huku kule maeneo ya kwetu hatuwezi kukutana na hiyo ATCL, hatuwezi kukutana na hiyo TAZARA, hatuwezi kukutana na meli kwa sababu hatuna maziwa, hatuwezi kukutana na chochote ambacho mnasema, standard gauge ndio kabisa huku kwetu haipiti, sina maana ya kujitenga katika Tanzania, lakini nina maana ya kuuliza swali moja tu kama hamtatusaidia sisi barabara zetu zikaonekana kwenye huu mpango tutakuwa tumeingia kufanya nini huku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa maeneo ya pembezoni tuangaliwe kama tunagawa rasilimali ya nchi hii tuigawe kwa usawa, haiwezekani maeneo fulani yanaonekana miradi mikubwa imeenda huko na maeneo fulani yamenyimwa kabisa. Ninajua wazi kwamba tutafaidi wote lakini tufaidi basi hata barabara. Sisi kwa Mikoa yetu ya Kaskazini ukiacha barabara hatuna kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine napenda kuishauri Serikali, hasa hili la mabenki ambayo kwa kweli sasa hivi tunaona crisis imetokea mimi sio mtaalamu wa uchumi lakini katika study yangu nime-study kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia tumekuwa tukishauri hapa habari ya vyanzo vya mapato, tunapenda sana kukusanya mapato, lakini naomba nishauri Serikali iangalie hii habari ya kukopa ndani ya nchi Serikali iangalie kwa sababu kuna fursa ya kukopa nje, kwa nini Serikali isitumie nafasi hii ambayo inayo ya kukopa nje ya nchi kuliko ndani kwenye mashirika ya kwake yenyewe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie basi kwa sababu ninaamini kwamba Serikali ina nafasi ya kukopa nje, Serikali inaweza kufanya jambo lingine ione kama kukopa ndani na kukopa nje ipi nafuu. Lakini kwa sababu nimesikia kengele ya mwisho niseme kidogo katika suala la fluctuation hili suala la kufanya fixing rating. Tufanye utafiti wa kweli, tunaweza kuangalia tukaishauri Serikali ikaamua kubadilisha mtindo wa sasa wa kuangalia soko la dunia katika upandaji wa dola na kushuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali moja tukiamua kubadilisha mfumo huo, je, Benki Kuu ya Tanzania inaweza kweli kuhimili mapigo ya kushuka kwa uchumi hasa inaposhuka itapata wapi fedha ya kufidia ile sehemu na ile gape? Kwa hiyo, naomba Wizara ijipange, Serikali iangalie kama imekuwa tayari kweli kuingia katika mtindo huu, ikiingia hapa lazima nayo Benki Kuu imejiandaa katika kuziba gape la kiuchumi, vinginevyo uchumi wa dunia ukishuka, Tanzania hatupo nje ya dunia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba kuchangia hoja.