Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2017/2018 pamoja na Mwongozo wake.
Ningependa nianze moja kwa moja na upungufu wa mizigo kwenye bandarii yetu ya Dar es Salaam. Nilikuwa nafikiri ni vizuri zaidi Serikali hii ikajikita kukubali kushauriwa na Waheshimiwa Wabunge wanavyotoa ushauri wao, na pia niwashauri sana Wabunge wetu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tujikite kwenye majukumu yetu ya kuishauri Serikali na kuisimamia Serikali. Kazi ambayo inafanyika sasa hivi kwenye Bunge hili ninaifananisha sana na picha za zamani za kihindi ambazo wakati bosi anatembea, alikuwa anatembea na watu walikuwa wanaitwa masuzuki, yule suzuki alikuwa anakaa pembeni kwa bosi na bosi akigeuka tu hata akikohoa yeye anaondoa miwani kwenye macho akifikiri ameitwa au anaagizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri sana tukapunguza uoga na tukasimama kwa miguu yetu kama Wabunge ili kulisaidia Taifa hili. Taifa hili lina watu wengi ambao wamepewa majukumu, ni wasomi wazuri, lakini pia ni wataalam ambao tumewaweka kwenye Wizara mbalimbali kuhakikisha kwamba wanaisaidia Taifa. Wataalam hawa tumefika mahala sisi wanasiasa tumeanza kuwaingilia, wameshindwa kutekeleza wajibu wao kufuatana na utaalam unaowaruhusu waweze kufanya kazi hizo. Jambo hili tukubaliane kwamba Taifa hili haliwezi kwenda kwa mtindo huu kama wanasiasa tutaingilia shughuli zote za kitaalam na sisi tukawa kwenye maagizo badala ya kuangalia ni namna gani tunaweza tukaishauri Serikali na kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza wajibu wake ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi huwezi kuamini, nchi imebaki ni nchi ya matamko kila mmoja anatoa matamko pale anapoweza, hakuna mwongozo unaoonesha kwamba ni nani anatakiwa kufatwa hapa. Wataalam wetu sasa hivi wameshashuka thamani na utaalam wao haueleweki tena kwa sababu ya sisi wanasiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka sana wakati Mheshimiwa Rais ameapishwa na wakati anaanza kutembelea wadau mbalimbali kujaribu kupata mawazo alikutana na wafanyabiashara katika nchi hii. Wakati anakutana na wafanyabiashara kwenye nchi hii jambo la kwanza alilolizungumza aliwauliza ni nani mmoja wenu aliyenichangia hata shilingi moja wakati wa kampeni. Swali hili lilikuwa ni swali gumu sana kwa wafanyabiashara ambao waliitwa wakitegemea kabisa kwamba Mheshimiwa Rais angeweza kuwashukuru pia kwa kazi kubwa waliyoifanya kuhakikisha kwamba wanaendeleza viwanda vyao, wanaendeleza biashara zao na wanalipa kodi katika Taifa hili mpaka alipolikuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini aliwauliza swali tu kwamba nani ambaye amewahi kunichangia wakati niko kwenye kampeni aseme hapa, tafsiri yake ni nini? Alikuwa anaweka gape, anatengana na wafanyabiashara na sasa hivi ndio maana baada ya muda mchache alitangaza wafanyabiashara wengi ni watu ambao wanaihujumu Serikali, ni wezi na ikaonesha kabisa kwamba Taifa hili linaonesha kabisa kwamba wafanyabiashara wote katika nchi hii ni watu ambao hawaaminiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lolote duniani kama halitawathamini wafanyabiashara na kukaa na wafanyabiashara na kubadilishana na wafanyabiashara mawazo ni namna gani Taifa lao liende, Taifa hilo haliwezi kupiga hatua hata siku moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilichokuwa nataka kukizungumza hapa nilikuwa nataka kusema kwamba ni lazima sasa Mheshimiwa Rais, lakini pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kurudi kukaa na wafanyabiashara, hakuna Taifa lolote linaweza likaendelea kwa sababu ya kutangaza kwamba yeye anapenda maskini, hakuna maskini anayependa kuwa na njaa, si siku nyingi maskini huyo akiwa na njaa akikosa dawa atamgeuka Mheshimiwa Rais kwa sababu hawezi kukubali kuendelea na mateso wakati anajua ana haki ya kupata maisha bora katika nchi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni mara nyingi sana wadau mbalimbali wanajaribu kutoa ushauri. Ninakumbuka sana Bandari ya Dar es Salaam tumezungumza mimi ni mjumbe wa Kamati ya PIC, tumezungumza sana tukiwa na Katibu wa Uchukuzi tukamweleza athari ambazo zimetokea kwenye Bandari ya Dar es Salaam, wateja ambao walikuwa wakitumia Bandari ya Dar es Salaam wakubwa ilikuwa ni Kongo pamoja na Wazambia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Tunduma niko pale Tunduma, kwa takwimu za mwaka 2014/2015 kwenye nchi hii asilimia 71 ya mizigo inayoshuka kwenye Bandari ya Dar es Salaam inapita kwenye mpaka wa Tunduma, lakini leo hii ukienda kuangalia tulikuwa na foleni ya malori karibuni kilometa nane ili kuvuka mpaka lakini leo huwezi kukuta gari hata moja liko barabarani limepanga foleni wanasema hali ni nzuri wakati hali bado ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wana Tunduma tumeathirika lakini pia Taifa tunaliona linaathirika kupita kiasi sasa wadau mbalimbali wanajaribu kutoa ushauri nakumbuka Mheshimiwa Sugu hapa alisema ndani ya Bunge hili akasema mtindo huu ambao Serikali imeanza kufanya kazi ya kuikusanyia Serikali ya Kongo kodi ni jambo ambalo linasababisha wateja wengi wa bandari yetu wakimbie waende Beira, waende Mombasa lakini pia wengine wameenda hadi Durban wanapitia kule japokuwa ni mbali lakini wameona afadhaili wapitie kule, hatukuweza kusikiliza tukaendelea kukomaza shingo zetu mpaka bandari inataka kukatika hapa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ndugu zangu, ninakumbuka sana wafanyabiashara pamoja na wadau wa bandari tuchukulie watu wa TATOA. Watu wa TATOA wamejaribu kuishauri Serikali mara nyingi, wameishauri Kamati ya Viwanda na Biashara, wakawaeleza wakasema tatizo kubwa la upungufu wa mizigo hapa ni tatizo la Serikali kutokusikiliza ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo walizungumza walijaribu kutoa mfano wa kampuni moja tu ya Impala ambayo ilikuwa ikipitisha kwa mwezi mzima tani laki tano kwenye bandari ya Dar es Salaam. Wakasema magari ambayo yalikuwa yakipakia mzigo na kwenda kupakuwa mzigo Kongo yalikuwa ni zaidi ya 30,000 kwa mwezi na magari haya yalikuwa yakitumia lita 2,500 kutoka Dar es Salaam kwenda Lubumbashi kwenda kuchukua copper na kila lita moja ya mafuta Serikali ilikuwa inachukua shilingi 600 kwa ajili ya kodi, lakini pia wakasema kwamba copper tani moja walikuwa wanalipa dola 600 kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam lakini leo hii hakuna kinachoendelea na juzi kwenye takwimu za Durban imeonesha Kampuni ya Impala imesafirisha tani laki saba kutoka Kongo na Zambia wamekwenda kupita kule kwa sababu ya ukiritimba tuliokuwa nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana mambo ya uchumi hayana utani, nchi za wenzetu zilizoendelea tunazoziona zina maendeleo mazuri si kwamba zinacheza na uchumi, uchumi sio jambo la kucheza nalo, leo watu wanasimama, Mheshimiwa Rais anasimama, Waheshimiwa Mawaziri wanasimama wanasema hata ikija meli moja, kauli hizi kwa kweli zinafika mahala zinawakatisha tamaa Watanzania na wanafikiria hawa ni viongozi kweli ambao tumewatanguliza kwa ajili ya kuleta ustawi wa Taifa hili. Ndugu zangu haitawezekana ukipata meli mbili au tano badala ya kupata meli 20 mpaka 30 huwezi kufananisha hata ungepandisha ushuru kiasi gani ni lazima tutakuwa na hasara katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana leo tunazungumzia uchumi kushuka kwenye Taifa hili watu wanakomaa hapa wanasema uchumi haujashuka wakati huduma za jamii, fedha katika Halmashauri zetu hazijafika leo watu wanasema uchumi haujashuka katika Taifa hili. Tunataka tuseme ni lazima Serikali ifike ikubaliane na ushauri mbalimbali unaotolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni kuhusiana na wafanyabiashara katika nchi hii. Wafanyabiashara wengi sasa wamekuwa na wasiwasi wameanza kuhamisha biashara zao wanakwenda Kongo, Zambia, Malawi na maeneo mengine wanahamisha biashara kwa sababu hawana uhakika wa biashara zao katika nchi hii. Kuna wafanyabiashara ambao wamekamatiwa mizigo yao, kuna wafanyabiashara ambao tayari wamefungiwa akaunti zao bila sababu za msingi na bila taarifa za msingi na wanafunguliwa akaunti bila kuambiwa nini kilichoendelea, jambo hili wafanyabiashara wamekuwa na wasiwasi wameona kabisa Serikali hii inaonesha kabisa haiwezi kuwatendea tena haki na wanaamua kuhamisha biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nikwambie tu takwimu zilizopo ukienda nchini Zambia kuna Watanzania zaidi ya milioni tatu wameamua kwenda kufanya biashara Zambia, lakini Malawi kuna Watanzania zaidi ya milioni moja na laki tano wanafanya biashara kule Malawi. Serikali imekaa kimya wanalipa kodi kule wananemesha nchi ya Malawi na Zambia kule Serikali imekaa kimya kwa sababu ya masharti magumu ambayo Serikali imeweka. Nataka nitoe mfano mmoja wa masharti ambayo Serikali inatakiwa iyatazame. Mimi niko mpakani mwa Zambia na Tanzania ukilipia mzigo wako eneo la custom pale ZRA - Zambia ukiondoka kwenda kufika Lusaka mzigo ule watu wa ZRA wanakuja kuchunguza risiti zako kama umelipia vizuri na mzigo ndio ule uliolipia, wakikuta mzigo ndio uliolipia wanachokifanya wao ni kukuruhusu ushushe mzigo na uendelee kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Tanzania mtu anatoa mzigo nje akishafikisha kwenye Bandari ya Dar es Salaam analipa ushuru, akishauchukua ule mzigo anafika Kariakoo watu wa TRA walewale wanakwenda kuchukua kodi, anatoka pale anakuja mtu wa Mbeya ananunua mzigo watu wa TRA walewale wanakwenda wanachukua mzigo ule kodi, anatoka pale anapeleka; mtu ananunua Mbeya pale anapeleka Sumbawanga watu wa TRA walewale wanakwenda kuchukua kodi, mzigo unatoka Sumbawanga mtu wa Nkasi anakwenda kununua mzigo mtu wa TRA yule yule anakwenda kufata mzigo Nkasi, ni sheria za wapi za kukusanya kodi katika dunia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndiyo vikwazo vikubwa vya wafanyabiashara katika nchi hii, ni lazima tufike mahali nchi yetu tunaipenda na hatuna nchi nyingine ya kukimbilia zaidi ya nchi hii; na sio nchi ya mtu mmoja ni nchi ya Watanzania wote tunahitaji kuipigania na lazima Wabunge tushikamane kwa jambo hili tuzungumze kwa nguvu zetu zote ili kuboresha uchumi wa nchi hii wananchi wetu waweze kupata madawa watoto wetu waweze kusoma na shughuli zingine ziweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa najaribu kujiuliza elimu bure Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaonesha ni jinsi gani ilivyofeli kwenye elimu bure. Wakati tunafanya mahesabu imeonesha kabisa kwamba karibuni shilingi bilioni 15.7 zinakwenda kila mwezi kwa ajili ya kulipia gharama za elimu bure kwa watoto 8,340,000; tafsiri yake ni kwamba kila mtoto anapewa shilingi 1,884.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inasema kwamba kila mtoto wa shule ya msingi anatakiwa kulipiwa shilingi 10,000 tunataka kujua shilingi 8,116 zinakwenda wapi na zitapatikana namna gani (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama kweli bajeti ni shilingi bilioni 15.7 tafsiri yake ni kwamba ukifanya mahesabu ya haraka haraka kwa watoto 8,342,000 utakuta ilihitajika fedha bilioni 83 kwa mwezi lakini inapelekwa bilioni 15 leo mnatuambia kwamba huduma za watoto mashuleni zinakubalika, kazi hiyo haipo, Serikali imeshindwa na iwaambie wananchi kwamba imeshindwa na mzigo huu wananchi waendelee kuubeba mzigo huu. Ndio maana madarasa sasa hivi hayajengwi, ndio maana ukienda ukiona msongamano wa watoto unazidi kuongezeka kwa sababu Serikali imewadanganya wananchi na kazi haifanyiki hata kidogo katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tulikuwa Bungeni humu, tukaishauri Serikali tukasema kitendo cha kuwaambia watumishi wakusanye ushuru kwenye Halmashauri zetu manpower ya watumishi wetu ni wachache katika Halmashauri zetu, tukasema hili jambo litakuwa ni gumu, leo katika Mji wa Tunduma ambapo kwa kipindi hiki cha mavuno tulikuwa tunakuwa na asilimia 40 mpaka 45 ya makusanyo leo tuna asilimia 18 tu, leo hii tumekaa hapa vyanzo 42 havijakusanywa hata shilingi moja ukimuuliza Mkurugenzi anasema watumishi ni wachache siwezi kuwagawa watumishi katika Halmashauri yangu. Serikali ikafidia fedha hizi ili tuweze kufanya maendeleo katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kuhusiana na kilimo, nilikuwa najaribu kuangalia kwenye Mpango huu naona kabisa kwamba kilimo kinaendelea kushuka…
MWENYEKITI: Ahsante.