Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye taarifa za Kamati ya PAC na LAAC. Nianze kwanza kuishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali ambayo imekuwa ikizichukua ili kuweza kupunguza yale mapungufu mengi ambayo yalikuwepo kipindi cha nyuma. Tumeshuhudia kumekuwa na reforms mbalimbali hususani financial management reforms zenye lengo la kuleta udhibiti wa matumizi ya Serikali, lakini pia kuondoa mapungufu mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza siku za nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kumpongeza CAG na wafanyakazi walioko chini yaOfisi ya CAG kwa sababu taarifa hizi ambazo tumeletewa ni matokeo ya kazi nzuri ya CAG ambayo ameifanya. Wachangiaji wengi wamekuwa wakizungumza juu ya mapungufu yaliyokuwepo, kikubwa yanasababishwa na ule udhibiti wa ndani, lakini kama nilivyosema kwamba Serikali imeanzisha pia Ofisi ya Internal Auditor General kwa nia hiyo ya kuleta udhibiti madhubuti kwenye taasisi zetu na mashirika yetu na hasa hata kwenye Serikali zetu za Mitaa. Kwa hiyo, naona Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa na naamini kwamba kadri tutakavyokwenda mambo yataendelea kuwa mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa ya ukaguzi ni kututhibitishia kwamba rasilimali za umma, zile asset za umma ziko katika hali nzuri, lakini pia tunapata ushauri kutokana na ukaguzi na matokeo yake ndiyo kama hivi kwamba Kamati zetu zimepata input ya kuweza sasa kuliletea mapendekezo Bunge ninaunga mkono mapendekezo yote ambayo yapo kwenye Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite zaidi kwenye mashirika ya umma. Niko kwenye Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Nilitaka nizungumze machache kuhusu ufanisi ambao utatekeleza saa nyingine haya mashirika ya umma kuweza kupunguza matatizo yaliyokuwepo lakini pia kuweza kuongeza mapato, non-tax revenue katika Serikali. Kwa sababu ukiangalia bado ule mchango ambao unakwenda kwenye Serikali kwenye mapato bado uko mdogo, ukiangalia kwenye bajeti ya 2016/2017, mchango huu ambao ni non-tax revenue ukijumlisha pamoja na Halmashuri uko asilimia 11.3; lakini ukiona kwenye mwaka huu ambao tunakwenda kuzungumzia kipindi kijacho projection iko asilimia 12.35. Kwa hiyo, bado mchango uko mdogo kwa hiyo, ninaamini kwamba kuna mambo mengi yakishughulikiwa hasa hasa kuboresha mashirika yetu, mchango utakuwa mkubwa katika Pato lile la Taifa.
Mhesimiwa Naibu Spika, nizungumze mambo mawili, jambo la kwanza nilitaka niseme kuhusu kuwezesha Ofisi ya Msajili wa Hazina. Utakuja kuona kwamba Msajili wa Hazina amekuwa akifanyakazi kubwa kwa upande wa Mashirika ya Umma lakini pia kwenye upande wa PAC naamini kwamba amekuwa kitoa mchango wao kuwezeha kazi za Kamati kufanyika vizuri. Lakini bado liko jambo la kumwezesha huyu Msajili ili aweze kupata uwezo mkubwa wa kufanyakazi na kuweza kusimamia mashirika haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwamba kazi ya kwake ya kushauri mashirika juu ya uanzishwaji na hata saa nyingine kufutwa baadhi ya mashirika ambayo hayana ufanisi lakini liko jambo pia la kuangalia ule utendaji wenye tija katika mashirika. Kupitia mipango na bajeti za mashirika na hata jana umeshudia tumepitisha mabadiliko ya sheria kwa nia ya maana kusaidia katika mashirika haya ili kuwa na uwiano ule wa matumizi na mapato yanayotoka kwenye mashirika haya hii itaiwezesha Serikali kuweza kupata gawiwo au fedha kutoka kwenye mashirika yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini anayo majukumu mengi, hii ni pamoja na kuweka viwango vya mashirika yetu kuweza kufanya makusanyo, lakini pia kuweza kuzisimamia hizi Bodi za Mashirika, kusimamia management na Kamati zake. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiria nipendekeze tu kwamba Serikali iitazame hii ofisi ya Msajili wa Hazina ili iweze kusaidia kuleta tija na kupunguza mambo ambayo yamejitokeza katika mashirika yetu ambayo yana changamoto nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika mashirika yetu ukiingalia sura ya mitaji iliyoko kwenye mashirika yaliyo mengi sura yake siyo nzuri inahitajika ifanyike uchambuzi wa makusudi wa nguvu na kushauri ili tuweze kuona zile capital structure kwenye mashirika yetu zinakuwa ni nzuri lakini kunahitaji pia kuweza kuona kwamba kuna mambo ambayo yameonekana kwenye report hii kwamba kuna madeni mengi kwa mashirika ambayo yanakusanya mapato yameshindwa kukusanya mapato vizuri, ipia utakuja kuona kwenye mizania kuna matatizo kwamba kuna rasilimali au asset za mashirika haya hazijafanyiwa evaluation muda mrefu, utaona matatizo yako mengi, iko ile mikakati ya kuweza kudhibiti vihatarishi (risk management) katika haya mashirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nafikiria niliseme hili kwamba Serikali iangalie sana hii ofisi. Ofisi inayo majukumu mengi na kama itawezeshwa kwa maana ya kuweza kuhakikisha kwamba wamekuwa na rasilimali za kutosha ili kuweza kushughulikia mashirika haya, tutaona kwamba tutaweza kuongeza ufanisi katika haya mashirika ambayo yapo kwa sababu ukija kuangalia mashirika yaliyo mengi hawana investment plan, mashirika yaliyo mengi utaona hakuna risk strategy za kuweza kuondosha hatari ambazo zinafanya mashirika haya yasiwe na ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haya yote haya Msajili wa Hazina anatakiwa kuyatazama na kwa kasi kubwa ili tuweze kuondokana na hayo matatizo ambayo yapo. Utakuja kuona hata kuna taasisi zingine za kifedha ziko chini ya Msajili wa Hazina na zenyewe zimekumbwa na matatizo haya ya kutokupata faida. Kuna mikopo chechefu, lakini pia ule uwekezaji lazima usimamiwe vizuri ili tuone kwamba mashirika haya yanaweza kufanya vizuri. Kumekuwana pia kutokuwa na record nzuri kwenye hesabu, kuna over statement za asset au under statement kwa hiyo haya mambo hayo ni muhimu sana yaweze kutazamwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la internal control, udhibiti wa ndani ni muhimu sana kutazama katika maeneo yote ili tuweze kupunguza hizi hoja lakini kikubwa tuweze kuwa na ufanisi mzuri katika kusimamia hizi rasilimali. Kwa hiyo, nilitaka nishauri tu kwamba jambo la kwanza Serikali isisitize sana kuhakikisha kwamba kunakuwa na Kamati za Ukaguzi ambazo zinatakiwa ziimarishwe, ziwe na watu wenye weledi lakini kama itawezekana pia kwenye mabadiliko ya sheria zetu tuzitazame ili Wajumbe wa Kamati hizi za Ukaguzi waweze kutoka nje ya taasisi husika ili ule ushauri uweze kusaidia kuboresha mashirika yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la lingine; wakaguzi wa ndani utakuja kuangalia hata katika Halmashauri zetu wakaguzi wa ndani ni wachache. Unakuta wakati mwingine wakipata fursa ya kwenda kwenye mafunzo ofisi zinafungwa zina wakaguzi wawili, zina wakaguzi watatu na hawa wakaguzi wa ndani ni jicho kwenye management iweze kusaidia kurekebisha mambo mapema kabla mambo hayajaharibika.
Kwa hiyo, ni muhimu Serikali itazame, imuwezeshe Mkaguzi mkuu wa ndani lakini pia wakaguzi wa ndani walioko kwenye taasisi zetu waweze kupata mafunzo lakini pia waweze kuongezwa ili waweze kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kuangalia pia kuwezesha mashirika yetu yana upungufu wa fedha, Serikali kama inaweza kwa sababu imekuwa ikiongeza makusanyo tuanzishe huu mfuko wa uwekezaji ili uweze kusaidia mashirika na taasisi ambazo ziko chini ya TR ili ziweze kuweza kupata fedha kutoka kwenye mfuko huu. Tuyaimarishe haya mashirika ili mwisho wa siku yaweze kuongeza gawiwo upande wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kukushukuru kwa kunipa nafasi hii kilio changu kikubwa ilikuwa ni kuhakikisha kwamba Ofisi ya TR inawezeshwa ili ikiungana na taasisi nyingine zinazoshughulikia masuala ya uadilifu, masuala haya ya tija, ziweze kufanya vizuri ili mwisho wa siku hoja zipungue lakini kikubwa ziweze kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.