Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na nimshukuru Mheshimiwa Silinde ku-share na mimi dakika chache ili na mimi niweze kutoa maoni yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niunge mkono asilimia mia moja hotuba za Kamati zetu zote mbili. Wamezungumza mambo mazuri ya kujenga na naamini Mawaziri wanasikiliza ili wakayafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pale Mheshimiwa Silinde alipoishia kuhusu TIB Bank kwamba hawa wadaiwa wanatukwamisha, fedha hizo zisitufikie maeneo mengine. Basi sasa kama Bunge tuazimie kwa nguvu zote kwamba hili litekelezwe na tuwafahamu hawa watu na waweze kulipa hizi fedha ili ziendelee kusaidia maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala ambalo nilitaka kulizungumzia siku ya leo, ni asilimia tano ya akina mama na vijana. Naungana na maoni ya Kamati kwamba walete marekebisho ya sheria kwa vile ule ni mwongozo umeshashindikana. Nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI kipindi kilichopita tulilisimamia hili sana lakini Wakurugenzi hawapeleki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na upungufu huo, jambo ambalo nahitaji kuishauri Serikali siku ya leo ni kwamba kwanza ule mwongozo una upungufu. Kwa mfano, wazee wa jinsia ya kiume wao hawapati zile fedha, akina mama wazee wanapata upande wa wanawake na vijana pia wanapata lakini wazee wa jinsia ya kiume (me) hawapati. Nimepita kwenye Jimbo langu na kila nilipopita wazee walilalamika kwamba hawanufaiki kabisa na mfuko huu na wenyewe wanaomba wapate hizo fedha kwa sababu sio wazee wote wenye wake na wenye watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono mapendekezo ya Kamati kwamba marekebisho yafanyike au ule mwongozo sasa tuuache. TAMISEMI kupitia miscellaneous amendment kama ni muswada mzima mtuletee ili na hao wazee wapate fedha hizo tofauti na sasa ambavyo wanahangaika kupata upande wa TASAF wakati TASAF haifiki maeneo yote. Pia mnafahamu TASAF kila baada ya miaka mitatu ndiyo wanabadilisha zile kaya maskini kwa hiyo hawa wazee hawatafikiwa. Kwa hiyo, hili mtuletee na naunga mkono kabisa mapendekezo ya Kamati ili na wazee wa jinsia ya kiume (me) waingie wapate hizo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kukazia siku ya leo ni suala la safari za Wakurugenzi. Kwa kweli Wakurugenzi mliotuletea hawakai kwenye Halmashauri zetu, akitoka kwa DC yuko kwa Mkoa wa Mkoa, akitoka kwa Mkuu wa Mkoa yuko kwa RAS. Ametoka kwa RAS anarudi kwa DAS ametoka hapo anaenda kwa OCD, ametoka kwa OCD yuko kwenye safari anasafiri Dar es Salaam au Dodoma, hawakai kabisa kwenye vikao vyetu. Wizara upande wa TAMISEMI muwaandikie basi muwape miongozo kwa sababu hawakai na ndiyo maana baadaye wanapoanza kutumbuliwa wanashangaa kama yale madudu yalifanywa na watu ambao waliwakaimisha wao. Kwa hiyo, niunge mkono maoni ya Wabunge wenzangu ambao jana walizungumza kwamba kuna tatizo kubwa sana kwa Wakurugenzi wetu, muwape mafunzo lakini wakae kwenye vikao vyetu vya Halmashauri waweze kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kuzungumza siku ya leo ni suala la madeni katika Halmashauri zetu. Mlivyotuletea Waraka wa Elimu Bure, kiukweli Serikali hampeleki pesa. Shule ya watoto 300 au 400, mnapeleka shilingi 200,000, huko huko wanunue mipira kwa ajili ya michezo, huko huko fedha za administration. Niliuliza swali kwa Waziri Mkuu jamani hiki kitu mfanyie review kwa hali ya kawaida shule zetu kuna madeni na Halmasahuri hizi zinadaiwa wakati huo huo mmechukua vyanzo vikubwa vya mapato. Kodi ya ardhi sasa inakusanywa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina hata zile asilimia 30 hamrudishi tena na ndiyo maana juzi nikasema kama ninyi ni waungwana kaeni chini muangalie zile asilimia 30 ambazo mlitakiwa kuzirudisha na mnafahamu zaidi shilingi bilioni 50 hamkuzirudisha, ni shilingi bilioni 4 tu mmerudisha juzi, basi leteni vifaa vya upimaji ardhi katika maeneo yetu kwa sababu huko kwenye Halmashauri zote kwa hali ya kawaida hawana vifaa hivyo.
Mimi niishauri Serikali acheni kuua Halmashauri zetu, kwanza mmepeleka sasa eti bima ya afya wazee tukawalipie kwa fedha gani? Kodi ya majengo mmechukua, TRA mpaka sasa hawakusanyi mnapoteza tu muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kodi ya majengo ndiyo hiyo tena inakusanywa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Wakati huo kuna madeni, Waraka wa Elimu Bure unataka tulipie madeni ya walinzi, maji katika shule zetu yameshakatwa kwa sababu Halmashauri haina fedha na fedha hampeleki hebu kaeni chini muangalie hizo Halmashauri mnaziweka upande gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nisisitize, kama mnahitaji kujenga hizi Halmashauri mkumbuke mlifanya decentralization kwa sababu wakusanye, walipe na wasimamie. Leo mnapochukua fedha hizo zote, mnatubakisha na ushuru tukimbizane na mama lishe, bodaboda na bajaji, kwa nini? Mtuachie hizo kodi ndiyo zilikuwa zinatusaidia tuendeshe hizo Halmashauri. Muwa-empower hao Wakurugenzi na Madiwani wetu wasimamie hizo fedha muone kama kazi hazitoenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho jamani leteni pesa za maendeleo, hakuna fedha kabisa. Halafu mnategemea hizo barabara tutachonga na nini? Pia kwenye miscellaneous mnazotuletea kila siku mtuletee ile ya TANROADS asilimia 70 tuiondoe, asilimia 30 ziende kwenye Halmashauri zetu kuchonga hizo barabara haiwezekani. Nilisema kwenye Bunge hili kwamba TANROADS watusaidie kwenye zile asilimia 70 ili tuchonge hizo barabara lakini ile ni wao wenyewe wapende au wasipende. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.