Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi. Niseme kwamba mimi ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani la Jiji. Kwa hiyo, baada ya kuona suala la UDA limeingizwa hapa na mambo yanayohusiana na Jiji yanatajwa ninawajibika kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nataka niweke rekodi sawa. Jana kuna mtu mmoja alikuwa anazungumza hapa, zamani tulikuwa tunawaita manjuka lakini siku hizi sijui tutawaita jina gani, wakasema kwamba hoja ya kutaka Jiji livunjwe ni kwa sababu ya kashfa ya Kiwanda cha Nyama, lakini anasahau kwamba kashfa hii ya Kiwanda cha Nyama ilitokea wakati Jiji likiwa chini ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Kashfa hii ya UDA tunayozungumza leo imetokea wakati Jiji likiwa chini ya Chama cha Mapinduzi. Wakati sasa Jiji liko chini ya UKAWA tunataka tulisafishe ili Halmashauri zile zilizokuwa tatu na sasa hivi zimeongezeka tano ziwe sehemu ya kuboresha lile Jiji. Hawa wezi wanaotajwa kwenye ukurasa wa 31 na 32 wa hii Kampuni ya Nyama na UDA ni makada wao na wanawajua na hatujaona popote walipofikishwa mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hivi, baada ya UKAWA kupata dhamana ya Jiji tumekwenda kubatilisha maamuzi yenye dhuluma yaliyopoka umiliki wa UDA Jiji na nitasema kwa nini?
Niliambie Bunge hili, msije mkathubutu, maana jana nilisikia wanasema kuna ile shilingi bilioni tano aliyolipwa Simon Group tuipangie matumizi, sisi kama Jiji tunatambua mamlaka yetu. Sasa kama sisi hapa hatujitambui Serikali inatuingilia sisi tunatambua mamlaka yetu. Tulisema hatuwezi kutumia hii shilingi bilioni tano kuhalalisha haramu kuwa kitu kitakatifu. Siyo kwamba haina matumizi, Halmashauri zetu zina changamoto nyingi sana, lakini tulisema hatuwezi kuwa sehemu ya haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa bahati mbaya sana TRA baada ya kuona Azimio la Baraza la Madiwani linasema hii shilingi bilioni tano ya Simon Group hatutaitumia kwa sababu kuna ushenzi umefanyika kinyume kinyume kwa kutumia upungufu wa kisheria, wakaenda wakavuta kodi. Kwa hiyo, hayo makusanyo mnayosema yameongezeka miongoni mwao ni fedha za kifisadi za kuiibia nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la UDA, nitazungumza kihistoria tu. Hili shirika lilianzishwa mwaka 1974 ambapo Serikali ilikuwa na hisa asilimia 100. Mwaka 1985 Serikali iliamua kugawa hisa zake, asilimia 51 ikaipa Jiji na yenyewe ikabakia na asilimia 49. Ni muhimu mkaelewa, hisa kiujumla wake zilikuwa milioni 15 lakini katika hizo hisa milioni 15, hisa milioni 7.1 ndiyo zilikuwa zimelipiwa ama zimekuwa allotted hizo nyingine milioni 7.8 zilikuwa hazijalipiwa. Kwa hiyo, Serikali ilivyogawa hisa, asilimia 51 Jiji na yenyewe asilimia 49, Jiji likapata milioni 3.9 na Serikali ikabakia na milioni 3.4. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, figisu lilianzia wapi? Figisu lilianzia mwaka 2011 na wakati nasema haya naomba Serikali ielewe hivi, UDA kama ilivyo mashirika mengine ilikuwa chini ya uangalizi wa PSRC ama ilikuwa specified kwa Tangazo la Serikali Namba 543 la mwaka 1997. Kwa mantiki hiyo, kisingeweza kufanyika chochote mpaka iwe despecified na siyo kwa maneno maneno ila kwa Gazeti la Serikali. Mpaka sasa PSRC ilikuwa hai ikaisha, ikaja CHC ikaisha, haijawahi kuwa despecified. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tafsiri nyingine ni nini? Miamala yote kisheria iliyofanyika kuhusiana na UDA ilikuwa ni batili. Ndiyo maana katika muktadha huo, Jiji baada ya kwenda kwa UKAWA kwa sababu tunasoma na kujiongeza na kwa sababu wengine tulikuwa sehemu ya huu mchakato tukasema hili zoezi ni batili. Nilikuwa naelezea historia nikachanganya kidogo ili kuwaweka kwenye mstari ili mjue kwamba huu mchakato ulikuwa haramu from the beginning. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2011 kupitia hao hao makada wao, sitaki kuwataja majina maana ni wazee nawaheshimu sana, nimewatajataja sana mpaka wakawa wananipigia simu Halima vipi? Kwa hiyo, sasa siwataji kwa sababu mnawajua.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2011 Bodi ya UDA ikaenda kugawa zile share ambazo hazikugawiwa na wala hazikununuliwa milioni 7.8 kwa Simon Group. Kwa aibu wamemuuzia share moja shilingi 145 yaani ile UDA yote walikuwa wanataka kuigawa nusu kwa jumla ya shilingi sijui bilioni 1.5 wakati huo huo ukaguzi ama tathmini iliyofanyika inasema shirika kwa huo unusu wake tu ina thamani zaidi ya shilingi bilioni 18 alikuwa anapewa mtu kwa sababu amehonga honga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mwaka 2011, kwa hiyo Simon Group akawa sehemu ya wanahisa wa UDA kwa kununua zile unallotted shares ambayo ni kinyume na Articles of Associations za UDA. Nina maandiko hapa ya Serikali, ya Msajili wa Hazina, yako hapa. Kwa hiyo, Waziri wa TAMISEMI tikisa tu kichwa nitakupa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo akapata uhalali kama mwanahisa kwenda kuomba kununua hisa zingine. Serikali ilitaka kuuza hisa zake, lakini vilevile Jiji kukawa kuna dhana ya kuuza hisa. Serikali ikaachia pembeni lakini Jiji kwa rushwa hizi hizi ikapitisha Baraza la Madiwani, wakapitisha kinyume na utaratibu. Tunajua vilevile hata kama Baraza la Madiwani likipitisha lazima Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI ambapo kipindi hicho ni Waziri Mkuu aridhie. Hakuna sehemu hata moja ambayo Waziri wa TAMISEMI ameridhia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na huo ubovu wake sasa Simon Group akatakiwa alipe hiyo hela. Pamoja na ubovu wa mkataba ikakubaliwa mwisho wa kulipa fedha hiyo ni Septemba, 2014 kwa sababu hapa kuna fedha za unallotted lakini vilevile kuna fedha za Jiji baada ya Baraza kukaa, bilioni 5.4 hazikulipwa. Tukakaa kama Kamati ya Fedha, ni kwa bahati mbaya sana Kamati ya Fedha ya Jiji na Baraza tukaazimia mkataba ule ukabatilishwe mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa masikitiko na nasema hivi kwa sababu Kamati ya LAAC wakati Baraza lenye mamlaka linasema huu mkataba haramu tunaenda kuubatilisha, LAAC, sitaki kuamini LAAC ilihongwa kipindi kile, ikaja ikasema msibatilishe huu mkataba wakaelekeza Jiji waendelee na makubaliano na Simon Group. Kamati ya LAAC, kuna maelezo hapa na kibaya zaidi, kesho yake baada ya Kamati ya LAAC ilivyokuja kutoa ushauri kwenye Jiji, yale maneno waliyokuwa wanasema LAAC ndiyo hayo hayo maneno ambayo Simon Group aliandika kwenye barua kuhalalisha kwa nini aongezewe muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hivi, kwanza, fedha za hizo hisa zimekuja UKAWA tumeingia. Fedha iliyotakiwa ilipwe mwaka 2014 imelipwa mwaka 2016, tukasema huu mchakato ulikuwa batili kisheria kuanzia mwanzo. Hata kama Baraza la Madiwani la kipindi kile chini ya Masaburi na CCM lilipitisha sheria inasema lazima Waziri aridhie, Waziri hakuridhia na hii UDA ilikuwa iko chini ya PSRC, miamala yote ilikuwa ni batili. Kwa mantiki hiyo, ili kuondoa mzizi wa fitina kwa sababu TAKUKURU ilifanya kazi yake, CAG alifanya kazi yake, nitaomba Bunge hili kupitia Kanuni ya Bunge ya 120 tuunde Kamati Teule ili hili suala lifanyiwe uchunguzi, tujue kinagaubaga, tujue mbivu ni zipi, tujue zilizoiva zipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu eti tunasikia hapa watu wanazungumza, basi zile hisa ambazo Simon Group alikuja kukubali kuzirudisha milioni 7.8 tupewe Halmashauri tugawane. Hivi tunagawanaje wakati hivi tunavyozungumza, Simon Group wamekopa bilioni 50 NMB kwa ajili ya magari haya ya DART. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa eti Serikali inaitetea wakati ripoti ya Msajili wa Hazina hapa analalamika yeye mwenyewe kama mbia ambaye hakuuza hisa zake alikuwa hajui kama kuna kakampuni kingine kadogo cha uendeshaji wa magari ya mwendokasi kalikoundwa na Simon Group. Yaani Msajili ni mbia analalamika hajui halafu anatoka mbele anatetea huo upuuzi. Sisi UKAWA tunaoongoza lile Jiji hatutaruhusu. Hatutaki mtuingize kwenye choo cha kike na choo cha kiume kwa kutulazimisha. Eti twende kuwa mwanahisa wakati kuna huyu jamaa kivyakevyake ameenda kukopa shilingi bilioni 50 ambazo zenyewe hatujui kazifanyia nini, kuna vibasi pale vya Kichina tu vya kizushi, kwa hiyo tuingie tuwe wanahisa tuwe sehemu ya huo mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hivi kesho kutwa Baraza la Madiwani tunaenda kukutana kwa sababu hiyo ni mandate yetu, yaani ninyi hapa mnatushauri tu. Kwa hiyo, msije mkajidanganya kwa wingi wenu, hasa ninyi upande wa huku, maana nasikia sijui Jiji linavunjwa, sijui sasa share tupewe, sisi wenye mali ambao tunaongoza Jiji ndiyo tunaenda kuamua siyo ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuongea hayo na nitaomba niungwe mkono kwenye kifuncgu cha 120 nitakapokileta hapo baadaye.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee suala la Lugumi, nitaomba Mwenyekiti akirudi atuambie Lugumi walienda kufanya nini? Kwa sababu tunajua mliomba mkataba ambao ndiyo unaweza kuainisha haki na wajibu wa kila pande. Tunavyozungumza, na wewe Naibu Spika unajua nawe ulisaidiasaidia kulifunikafunika kuisaidia Serikali, unajua kwamba Bunge linapohitaji mkataba wa aina yoyote linatakiwa kupewa. Kamati yako imeomba mkataba kwa sababu CAG alisema vifaa vimefungwa 14 baada ya hoja ya Mheshimiwa Zitto alipokuwa Mwenyekiti wa PAC, mwezi Mei, 2016 CAG aliitwa tena na hawa kasema vimefungwa 14. Hivi ni miujiza gani imetokea tunaambiwa leo eti vimefungwa 153, ni miujiza gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunataka tujibiwe hapa kwa sababu imekuwa ni utamaduni wa nchi hii tunatumia Usalama wa Taifa, tunatumia Polisi, Ulinzi na Usalama excuse kuiibia nchi. Sasa leo Mwenyekiti…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Halima, malizia sentensi muda wako umekwisha.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Unajua leo nilikuwa na mizuka sana kwa sababu ya UDA hadi mbavu zinauma.