Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza shukrani kwa Allah (S.W.) kwa kuniwezesha kuchangia hoja hii ya mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/2018. Nikiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya vizuri katika maeneo yafuatayo:-
(a) Kupambana na wafanyakazi hewa, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na Idara zake zote;
(b) Kuendelea na mapambano dhidi ya ufisadi uliokuwa ukifanyika katika nchi yetu; na
(c) Kupambana na kuzuia mfumuko wa bei katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mpango kuandaliwa vizuri na kitaalam, bado kuna upungufu ufuatao:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza msingi wenyewe wa viwanda ni jambo linalohitaji maandalizi makubwa na mapema. Kwa kweli, dhana ya viwanda inataka fedha za kutosha kama mtaji, rasilimali watu wenye ujuzi na miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mawazo yangu, Serikali bado haijawa kwenye wakati mzuri kutoa fedha kwenye viwanda. Badala yake fedha zipelekwe kwenye miundombinu ya kuwezesha viwanda, badala ya kuanzisha viwanda na hasa ukizingatia Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha kwenye sekta hii ya viwanda.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kuwa na mahusiano mabaya na wafanyabiashara wakubwa na wadogo, hatuwezi kujenga nchi bila kushirikiana kati ya Serikali na wafanyabiashara.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wafanyakazi wa Serikali ni watu muhimu sana kwa ujenzi wa Taifa letu. Naomba Serikali yetu iwaangalie kwa jicho la huruma.
(d) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na mkakati wa kubadilisha watendaji wake. Jambo hilo ni zuri, lakini linahitaji umakini na hasa watendaji wawe na weledi wa kutosha na hasa wasiwe wakereketwa wa Chama, bali wawe watu wanaoweza kufanya kazi bila ya kuathiriwa na siasa na upendeleo wa kivyama.
(e) Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu amejikita katika usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali za kila siku. Kwa mawazo yangu, kazi hii inaweza pia ikafanywa na Waziri Mkuu na hasa baada ya Rais kuonesha nini anataka katika utendaji wa Serikali na Waziri Mkuu ameona nini Rais anataka ili naye aige.
(f) Mheshimiwa Naibu Spika, demokrasia ni dhana kubwa katika maendeleo ya nchi. Mfano Uchaguzi wa Meya, Tanga, Kinondoni na uchaguzi wa Zanzibar. Kama demokrasia ikiheshimiwa itaongeza mahusiano ya ndani, pia itatoa fursa ya kupata fedha za MCC za Marekani, mfano Dola milioni 698.1 kwa mwaka.
(g) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kodi ya majengo kukusanywa na TRA. Jambo hili lilikuwa linafanywa na Manispaa vizuri sana, hivyo tunaiomba Serikali jambo hili la Kodi ya Majengo lirejeshwe kwa Manispaa na Halmashauri, kama ilivyokuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri kwa Serikali yetu:-
(a) Kujenga miundombinu ya viwanda na siyo kujenga viwanda na kuendesha mashirika ya ndege;
(b) Pesa ya Sekta ya Kilimo kufikia 10% ya bajeti ya nchi;
(c) Serikali ihakikihe mchango wa madini kwa pato la Taifa mpaka kufikia 10% ya pato la Taifa;
(d) Kuleta utengamano wa kisiasa kwa Zanzibar, Tanga na Kinondoni;
(e) Ajira kwa vijana, hasa tuongeze fedha kwenye mabenki, kilimo, uvuvi na ufugaji; na
(f) Kuondoa VAT katika mizigo ya nje na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.