Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kabla sijaanza kuchangia kumsifu sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuratibu kazi hii ya kuandaa Mpango wa Miaka Mitano na hatimaye ameuwasilisha leo mbele ya Bunge hili.
Natoa shukrani nyingi kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi ambazo imefanya mpaka sasa hivi. Ni kazi nyingi na nyingi zinaonekana kwa macho sio lazima kuambiwa.
Kwa hiyo, napongeza sana kazi ambazo zimefanyika mpaka sasa hivi. Kuanzia Awamu ya Kwanza, ya Pili, ya Tatu na sasa hii Awamu ya Tano ya hapa kazi tu naamini inajenga matumaini makubwa kwamba tuendako sasa kutakuwa na mafanikio na maendeleo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili viwanda vijengwe, viendeshwe kwa mafanikio na vistawi nchini, vinahitaji sana miundombinu ya barabara kuu za lami, za Mikoa, za Wilaya, za Kata hadi kwenye Kijiji ili malighafi iweze kufikishwa kiwandani au viwandani unahitaji miundombinu hiyo iweze kupitika muda wote wa mwaka. Kwa hiyo, kwenye Mpango nimesoma, nimeona kuna mipango mingi imepangwa mle, nachohitaji ni kuhakikisha kunakuwa na usimamizi madhubuti ili tuweze kufanikiwa. Kama usimamizi utalegalega itakuwa ni taabu, bidhaa haziwezi kufika sokoni vizuri na bei inaweza ikawa kubwa kama miundombinu hai-support bidhaa kufika sokoni kwa urahisi. (Makofi)
Nataka nikumbushe tu eneo moja ambalo liko kwenye Mpango ambalo linahitaji macho mengi kuangalia na kujua. Kati ya Chunya hadi Mkiwa, wapo takribani watu 1,500,000 ambao wanafanya shughuli nyingi sana za kiuchumi katika maeneo hayo. Ile barabara iliamuliwa tangu mwaka 2005 kwamba ijengwe kwa kiwango cha lami. Imechelewa na mimi nahitaji umadhubuti mkubwa katika kusimamia na kukumbuka. Nilikuwa nataka nipaze sauti kali ili Mheshimiwa Profesa Mbarawa huko aliko asikie lakini kwa sababu atakuja kusoma kwenye Hansard basi siwezi kupiga kelele hapa. Naomba sana hiyo barabara ikumbukwe kwa sababu kuna kazi nyingi sana za kilimo na maliasili nyingi sana katika maeneo hayo ambazo zikivunwa na zikafikishwa viwandani zinaweza kusaidia sana uchumi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa njia yoyote ile wataalam wa barabara wanatumia aina mbili za models kwa ajili ya kuamua barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami au isijengwe. Wanatumia HDM (Highway Development Model) au wanatumia RED (Road Economic Decision). Zote hizi ukizifanyia ukaguzi utagundua kwamba barabara hii inafaulu kwa model zote mbili.
Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Waziri wa Ujenzi mwongeze jicho lenu kwenye hii barabara ili kusudi watu wa maeneo hayo waweze kupata unafuu. Miundombinu mingine ambayo inahitajika kwa ajili ya viwanda na umeme mijini na vijijini; vijijini unahitajika zaidi umeme, tuwashukuru REA kwa kazi wanayoifanya. Awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu naomba ikamilike kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pesa ambazo zimepangwa kwenye Mpango ziwe zinafika kwa hawa watu wa REA ili kusudi utekelezaji ufanyike kwa wakati. Bila kufanya utekelezaji kwa wakati, hatutafanikiwa malengo yetu. Kwa sababu hata kama utajenga kiwanda halafu kikakosa umeme, hakitazalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana hiyo miundombinu wezeshi itiliwe mkazo kweli kweli katika kuisimamia na hii ni pamoja na mitandao ya simu. Katika maeneo yetu mengi hasa kwenye Wilaya yangu ya Sikonge, tuna-coverage ya asilimia 45 tu ya mitandao ya simu. Sasa watu watapashana vipi habari? Watapeana vipi habari za masoko? Watauza vipi bidhaa zao bila kuwasiliana? Kwa hiyo, hili la mitandao ya simu nalo naomba liwekewe mkazo sana katika usimamizi ili kusudi tuweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ambacho ndiyo kiwezeshi kikubwa kinachohitajika kwa ajili ya viwanda; kazi ya Serikali popote duniani huwa ni tatu. Kwanza, ni utafiti wa mbegu, miundombinu ya mazao na kadhalika; ya pili ni huduma za Ugani; na ya tatu ni kumlinda mkulima apate haki ya jasho lake. Hizo kazi ndiyo kazi za msingi za Serikali popote duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mpango yameandikwa mengi, lakini naomba sana mkazo utiwe kwenye hayo maeneo matatu. Ni lazima utafiti ufanyike kuanzia Mtwara huko kwenye korosho mpaka kwenye tumbaku; kuna kilio kuhusu uwekezaji mdogo kwenye utafiti. Naomba sana Serikali ikumbuke suala la utafiti ni kazi yake ya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni huduma za ugani. Viko vijiji vingi havina Maafisa Kilimo ambao wanawajibika kuwashauri wakulima kuhusu kilimo bora. Sasa hili nalo linahitaji umakini wa hali ya juu wa Wizara ya Kilimo ili kusudi wananchi waweze kusaidiwa walime kilimo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ni kumlinda mkulima apate haki ya jasho lake na hapo ndipo kuna matatizo makubwa. Mifumo ya pembejeo ina matatizo makubwa; wakulima wanapata madeni makubwa. Naomba sana Serikali ifanyie kazi suala la mifumo ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kwa njia rahisi kusudi watu wetu waweze kulima bila usumbufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo ya masoko nayo ni tatizo kubwa ambalo linatakiwa lifanyiwe kazi. Wakulima wanapunjwa bei na kuchelewa kulipwa. Hayo inatakiwa yafanyike ili kusudi kilimo chetu kiweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa elimu kwa ajili ya kusaidia viwanda, tunahitaji shule maalum za kilimo na ufundi stadi zirejeshwe au zirejeshewe makali yake kama ilivyokuwa zamani. Zirejeshewe hadhi yake na zijengwe na nyingine mpya kwenye maeneo mbalimbali. Hii ni pamoja na kila Wilaya kuwa na VETA, hiyo itasaidia kupatikana nguvu kazi ambayo inahitajika viwandani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo ningependa nizungumzie hapa, limetajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi, lakini kwenye Mpango sijaliona vizuri; suala la vikundi kazi vya kijamii vya vijana; vikundi kazi vya ujenzi, mafundi seremala na vya uzalishajimali. Tunajua Mipango ipo lakini ni muhimu sana tusisitize hili kusudi hivi vikundi kwanza vipate kazi kwenye Halmashauri zetu, vijiimarishe kiuchumi ili baadaye vyenyewe viweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo napenda kulizungumzia ni ufuatiliaji na tathmini. Ufuatiliaji na tathmini unaanzia kwenye mapato na matumizi. Naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, inafanya kazi nzuri sana ya kufuatilia mapato ili kuhakikisha kwamba Serikali inapata kile ambacho inastahili kukipata kutoka kwenye kodi na vyanzo vingine ambavyo siyo vya kodi. Ni muhimu sana suala hili liendelee kutiliwa mkazo isijekuwa baada ya miaka mitatu tukarudi kule kule tulikotoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la kudhibiti matumizi; ilipoanzishwa MTEF mwaka 1999 ilikuwa matumizi yanaruhusiwa tu kwenye vile vipengele ambavyo vilipitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kadri ambavyo tumeendelea mpaka sasa hivi, matumizi yamekuwa yanabadilika, baada ya miezi sita watu wanaomba reallocation nyingi Wizara ya Fedha. Sasa matumizi lazima yadhibitiwe kwenye vifungu ambavyo vimepitishwa na Bunge kusudi baadaye tuboreshe mipango yetu ili izingatie uhalisia. Hapo tunaweza tukafanikiwa vizuri kutekeleza malengo yetu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mianya ya wizi, mikataba na usimamizi wake iendelee kudhibitiwa ili kusudi yale ambayo yamepangwa kwenye mkataba yaweze kutekelezwa kama yalivyopangwa. Vile vile flow ya fedha inatakiwa isimamiwe vizuri ili kusudi fedha ambayo imepangwa kwa ajili ya mkataba fulani ifike kutekeleza huo mkataba. Nadhani tukifanya hayo, huu Mpango wetu utatekelezeka vizuri na tutapata mafanikio makubwa na nchi yetu itafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, yangu yalikuwa ni hayo tu.