Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2016/2017. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili, nachukua nafasi hii kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ambao walinipa kura za kishindo ili niweze kuwawakilisha vyema katika vikao hivi vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawashukuru sana wanawake wenzangu wa Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nachukua nafasi hii kuwashukuru wapigakura wote wa Mkoa wa Ruvuma ambao wamehakikisha kwamba Chama cha Mapinduzi kinashinda Majimbo yote ya Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala la umeme. Kwa kuwa kwenye Mpango huu kimsingi tumejipanga kuhakikisha kwamba tunakua kiuchumi hasa kupitia viwanda; na kwa kuwa viwanda vyetu haviwezi kuendeshwa bila kuwa na umeme wa uhakika; sijaona mpango mzuri ambao umewekwa kuhakikisha kwamba umeme wa grid ya Taifa kutoka Makambako kuelekea Songea unasimamiwa vizuri ipasavyo na kuhakikisha kwamba mradi huu wa umeme unatekelezwa kwa haraka ili kurahisisha ujenzi huu au Mpango huu wa Viwanda ambao Taifa kwa ujumla limejipanga hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mashaka yangu ni kwamba, inawezekana kabisa Mkoa wa Ruvuma tukaachwa nyuma kwa kuwa bado umeme huu wa grid ya Taifa haujafika huko. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati ahakikishe kwamba katika bajeti hii, suala la kuhakikisha kwamba umeme wa grid ya Taifa unafika Mkoani Ruvuma ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba nizungumzie suala la maji. Kwa kuwa suala la maji ni muhimu sana katika ustawi wa maisha ya binadamu hasa wananchi wetu na kwa ujumla nchi nzima, naomba leo niongelee eneo moja la shida ya maji ambayo inaukumba Mkoa wa Ruvuma. Katika Wilaya ya Tunduru, Namtumbo, Songea Mjini, Songea Vijijini, Madaba, Wilaya ya Nyasa pamoja na Wilaya ya Mbinga, kiukweli kuna shida kubwa sana ya maji. Katika Mpango huu wa utekelezaji wa mwaka 2016/2017 sijaona mkakati madhubuti ambao utapelekea kupunguza adha ya maji kwa wanawake wa Mkoa wa Ruvuma.
Kwa hiyo, nadhani ni vizuri Wizara hii ya Maji ione umuhimu katika kuhakikisha kwamba endapo hakutakuwa na uwezekano wa kupata maji ya mtiririko kwa mwaka huu, basi wanawake wale waweze kuchimbiwa hata visima virefu wakati wanaendelea kusubiri mpango wa maji ya mtiririko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, kimsingi Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma zina shida hiyo na wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ni wanawake ambao ni wajasiriamali, lakini pia ni wakulima. Kwa hiyo, wanatumia muda mwingi sana kwenda kufanya shughuli ya kutafuta maji badala ya kwenda kufanya shuguli zao za kilimo na hata nyingine za ujasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee pia suala la bandari kama Mpango ulivyoainisha suala la kuboresha bandari. Katika Wilaya ya Nyasa tuna ziwa Nyasa lakini pia kuna gati la Ngumbi. Zabuni ya ujenzi wa Gati ya Ngumbi ulikamilika tangu Januari, 2015, lakini ujenzi mpaka sasa hivi haujaanza na wala hakuna matumaini yoyote. Katika Mpango huu sijaona kama kuna fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya mwendelezo huo, ni maneno tu yanaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Mpango huu wa ujenzi wa Gati hii ni wa muda mrefu sana takribani miaka 20 sasa. Kwa kuwa katika Mpango huu pia bado halijaingizwa hili suala, ni mashaka yangu kwamba inawezekana tunaingiza vitu kwa maana ya mpango lakini utekelezaji unakuwa sivyo. Naomba sana, Gati hili la Jimbo la Nyasa litengewe fedha kwa ajili ya utekelezaji na siyo maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la kilimo. Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa ambao unashika nafasi ya nne Kitaifa kwa suala la kilimo. Pamoja na mazao mengi yanayozalishwa katika Mkoa wa Ruvuma, lakini leo naomba niongelee zao ambalo linazalishwa katika Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma ambalo ni zao la mahindi. Hili ni zao la chakula katika Mkoa wetu lakini pia ni zao la biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mpango Mzuri wa Serikali wa kuhakikisha kwamba unatoa Ruzuku ya Serikali kwa ajili ya pembejeo za kilimo kwa maana ya voucher, niseme tu kwamba vouchers hizi kimsingi hazimnufaishi mwananchi wa kawaida wa pato la chini. Badala yake kumekuwa na vurugu, yaani kutokuelewana baina yao wenyewe; wananchi wao kwa wao pamoja na wanaosimamia. Tatizo ni kwamba voucher ni kidogo na hitaji ni kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiria kwamba ni vizuri basi Mpango huu wa Serikali ungekuja na Mkakati maalum namna gani unamwezesha mwananchi ili aweze kupata pembejeo za kilimo kwa bei nafuu baada ya kuondoa kodi ili kila mwananchi aweze kuchukua pesa yake kununua pembejeo za kilimo kwa bei nafuu badala ya kuwa baadhi wanapata voucher na wengine hawapati. Matokeo, mnatusababishia ugomvi ambao siyo muhimu kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani Mpango huu ungekuja na Mkakati wa kuona namna gani kodi inaondolewa na wananchi wale waweze kufikiwa, mmoja baada ya mwingine aweze kujikimu mwenyewe kununua pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mpango Mzuri wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wananchi wanawezeshwa kwa maana ya Shilingi milioni 50 kila Kijiji na kila Mtaa, ni mpango mzuri sana wa kuhakikisha kwamba uchumi wa mwananchi mmoja mmoja unakua. Naipongeza sana Serikali kwa kuona umuhimu wa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango huu pia sijaona mkakati madhubuti ambao umewekwa kuhakikisha pesa hii inayoenda kwa ajili ya kumwinua mwananchi mdogo, inatengeneza mazingira ya kumwondolea kodi zisizokuwa za lazima au ushuru usiokuwa wa lazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, pesa hii inalenga kabisa kuwainua watu wafuatao: kwa mfano, vijana, mama lishe, bodaboda, wauza matunda na wauza mboga mboga. Sasa ushuru ambao wanatozwa kwenye masoko yao ni ushuru mkubwa. Haiwezekani mtu ana fungu tano za nyanya anatozwa Sh. 1,000/= kutwa! Hiyo ni shida! Kwa hiyo, Mpango huu uende na mkakati wa kuona ni namna gani wataondoa huo ushuru usiokuwa na umuhimu ili kumfanya mwananchi huyu, kweli kile anachokipata aweze kukizungusha na kujikimu katika maisha yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Benki ya Kilimo. Ni jambo jema Serikali kuanzisha Benki hii ya Kilimo, lakini ndani yake nimeona kuna vitu ambavyo siyo sahihi. Benki hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kumwinua mkulima, lakini kwenye utekelezaji iko ndivyo sivyo kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma vizuri kwenye mapendekezo ya Mpango huu na nimeona kwamba kuna baadhi ya mikoa ambayo imetengwa kwa ajili ya majaribio na imeshaanza kupelekewa fedha. Baadhi ya hiyo Mikoa ni Iringa; sina shida, wananchi wa Iringa wanalima, lakini pia Mkoa wa Njombe sina tatizo nao, wanalima vizuri tu; Mkoa wa Morogoro nao pia ni wakulima wazuri; hata Pwani, wanalima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vitu vya kushangaza sana eti Mkoa wa Dar es Salaam nao umepangwa kwa ajili ya watu kupata pesa ya kilimo. Jamani, tuseme ukweli, hivi Dar es Salaam kuna mashamba ya kulima? Mbona hatujaona hayo mashamba, wanalima wapi? Ina maana kuna mashamba Mikocheni, Oysterbay na hapo Sinza Mori? Haya ndiyo mambo ambayo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayataki na ndiyo anayamulika. Haya ni sehemu ya majipu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Serikali imejipanga kumwinua mkulima wa kawaida wa hali ya chini, ni vizuri basi malengo haya yakaenda moja kwa moja kwenye maeneo ambayo wananchi wapo na wanalima kweli, badala ya kwenda kuwanufaisha tu watu wamekaa tu maofisini, wengine wamekaa kwenye magari yao, full viyoyozi, wanapata pesa za kilimo ilhali hawalimi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee kuhusu suala la Uwekezaji. Mpango wa Serikali juu ya suala la uwekezaji naona ni mzuri, lakini pia nadhani uende sambamba na kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yalikuwa yamechukuliwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza viwanda kwa maana ya ardhi ya wananchi ambayo imechukuliwa, basi Mpango huu wa Serikali wa kuendeleza viwanda uende sambamba na kulipa fedha za fidia kwa wananchi ambao wamechukuliwa maeneo yao, ikiwemo eneo la Mwenge Mshindo katika Wilaya ya Songea Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sana wawekezaji hawa EPZ wamechukua maeneo makubwa sana ambayo mpaka sasa hivi inakaribia miaka 15 au 16 wananchi hawajalipwa pesa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba kwenye suala la miundombinu, barabara inayotoka Makambako kwenda Songea…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ngonyani!
MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Nayo pia ifanyiwe marekebisho ni mbaya sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ngonyani, muda wako umekwisha.
MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.